Habari za Punde

Mpanda vespa afariki, mwengine ajeruhiwa


NA HAJI NASSOR, PEMBA

MTU mmoja aliekuwa akiendesha Vespa ambae ni mkaazi wa Mwambe wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba, Juma Mohamed Juma (70), amefariki dunia na mwengine kujeruhiwa, baada ya kugongana na gari ya abiria.

Tukio hilo lilitokea juzi majira ya 1:30 eneo la Majenzi shehia ya Kengeja wilaya ya Mkoani Pemba, wakati wapanda vespa huyo akitokea Mwambe kuwenda Mtambile, ndipo walipogongana na gari hiyo ya abiria, iliokuwa ikitokea Mtambile kwenda Mwambe.

Mashuhuda wa tukio hilo, walisema mpanda vespa ambae alifariki hapo hapo, aliacha eneo lake na kwenda eneo lililokuwa likipita gari hiyo, na kugongana uso kwa uso.

Mashuhuda hao walisema, mwili wa marehemu Juma, ulivurugika eneo hilo kutokana na ajali ilivyokuwa kubwa , ingawa aliekuwa amempakiwa  kwenye vespa hiyo, kijana Zaidu Khalfan Faki (25), alipata majeraha na kukimbizwa hospitali.

“Baada ya ajali na mzinga niliousikia kufika tu naona mwendesha vespa ameshafariki, na baadhi ya mifupa imeganda kwenye gari, lakini mwenzake alichukuliwa baadae na kukimbizwa hospitali kwa matibabu”,alisema shuhuda huyo.

Nae shuhuda mwengine aliejitambulisha kwa jina moja la Mohamed, alisema yeye muda mfupi wakati anatembea kwa miguu, alipitwa na muendesha vespa huyo kwa mwendo usiokuwa wa kawaida.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa kusini Pemba, Shehan Moahemd Shehan, alisema chanzo za ajali hiyo, kwanza ni mwendo kasi wa mwendesha vespa.

Alisema aidha wamegundua kuwa, mpatwa na kifo hicho ambae alikuwa dereva, aliacha sehemu anayopaswa kupita na kuifuata gari na kutokezea kwa ajali hiyo.

“Ingawa uchunguuzi wa kina unaendelea, lakini kwa huu wa awali, basi tumegundua mambo kadhaa yaliiopelekea kutokezea kwa ajali hiyo, likiwemo mwendesha vespa kuifuata gari”,alieleza.

Hata hivyo alisema bado wanamshikilia dereva ambae hakumtaja jina  lake, wa gari hiyo ya abiria yenye namba za usajili Z 464 DT namba 315, inayofanya kazi zake Chakechake-Mwambe, kwa mahojiano zaidi.

Alifafanua kuwa, wakati wowote taratibu zitakapokamilika atafikishwa mahakamani, kujibu tuhuma zitakazomkabili, kutokana na ajali hiyo.


Hivyo ametoa wito kwa madereva wa gari, waendesha vyombo vya magurudumu mawili, na waenda kwa miguu, kuwa waangalifu wanapokuwa barabarani, kwani kila moja na aina ya matumizi ya barabara hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.