STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
24.10.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ameupongeza uongozi wa Wizara ya Ardhi, Maji,
Nishati na Mazingira kwa kutekeleza vyema majukumu yao na kuutaka kutotumia
muda wao mwingi kukaa ofisini na badala yake waende kwa wananchi wakawasikilize
changamoto zinazowakabili kwani Wizara hiyo imegusa mambo muhimu katika maisha
yao.
Hayo aliyasema leo, Ikulu mjini Zanzibar
alipokutana na uongozi wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira wakati ilipowasilisha
utekelezaji wa Mpango Kazi wa Mwaka 2016/2017, Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa
mwaka 2017/2018 na Utekelezaji wake kwa
kipindi cha robo ya kwanza ya Julai hadi Septemba, 2017.
Dk. Shein alieleza haja kwa uongozi huo kuyakabili
na kuyasimamia majukumu yao na kuueleza uongozi huo kuwa kuwasikiliza wananchi changamoto
zao ndio sifa moja wapo kubwa ya uongozi kwani kiongozi ni lazima awasikilize
wananchi pamoja na wale wote anaowaongoza.
Aidha, Dk. Shein alisisitiza suala zima la
kuwajibika katika utekelezaji wa kazi zao, kwani kila mmoja ana wajibu wake
kazini kwake na katika cheo chake kwa kufuata taratibu, kanuni, sheria na
misingi yote ya kazi. “uwajibikaji utakuja kwa kujituma… Pia, ni vyema kufanya
kazi kwa kufuata wakati”.alisisitiza Dk. Shein.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa
uongozi na wafanyakazi wote wa Wizara ya hiyo kwa kutekeleza vyema majukumu yao
na kufanya kazi kwa pamoja hali ambayo imedhihirika baada ya uwasilishaji wa
Mpango Kazi wao na kuwataka kuendeleza utamaduni huo.
Alieleza matumaini yake katika usimamizi wa sekta
zilizomo katika Wizara hiyo ikiwemo sekta ya ardhi na kusisitiza mashirikiano pamoja
na kusaidiana katika kutekeleza majukumu yao ya kazi huku akitoa pongezi kwa hatua
zinazochukuliwa katika kupeleka umeme kwenye visiwa vidogo vidogo kupitia
Shirika lake la (ZECO).
Dk. Shein alieleza kuridhishwa na hatua
zilizofikiwa katika kupata taarifa za upatikanaji na uhifadhi wa mafuta hapa
Zanzibar kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa
Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) pamoja na utaratibu mpya wa ununuzi
wa mafuta kwa lengo la kuondosha usumbufu wa nishati hiyo kwa wananchi.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alifurahishwa na azma ya
Wizara hiyo katika suala zima la Mipango Miji hasa kwa mji wa Zanzibar sambamba
na azma ya kurejesha haiba na jina la Uwanja wa Farasi uliopo mjini Unguja ambao
hapo miaka ya nyuma uwanja huo ulitumika na kuwa maarufu kwa mchezo wa farasi.
Katika kikao hicho, Makamo wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Idd nae alihudhuria na kutumia fursa hiyo kusisitiza
haja ya kuwepo kwa uhakika wa upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi
wa Unguja na Pemba.
Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza kazi nzuri ya uwasilishaji
iliyofanywa na Wizara hiyo huku akisisitiza haja ya kuwepo kwa usimamazi mzuri kwa
watendaji wa Wizara hiyo kutokana na sekta zake kuwagusa wananchi moja kwa
moja.
Nae Waziri wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na
Mazingira Salama Aboud Talib alieleza kuwa Wizara hiyo inaendelea na jitihada zake za
kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za maji, nishati, Mazingira ya
kuishi pamoja na kuimarisha matumizi bora ya ardhi.
Waziri Salama alieleza kuwa kwa upande wa Mkoa wa
Mjini Magharibi, utekelezaji wa mradi wa maji safi na usafi wa mazingira ambao
unatarajiwa kukamilika ifikapo 2018 umeanza kuonesha mafanikio katika maeneo ya
uimarishaji wa miundombinu ya maji unaohusisha ukarabati na uchimbaji wa visima
vipya 9, ujenzi wa matangi matatu ya juu yenye jumla ya ujazo wa lita milioni 5
sambamba na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 68 yenye upana tofauti.
Kwa upande wa program ya usambazaji maji vijijini,
Wizara hiyo imo katika hatua za kukamilisha mradi wa uchimbaji visima na
usambazaji maji unaofadhiliwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
Hii ni kwa lengo lakuimarisha huduma za maji
katika maeneo makuu matano ambayo ni Chaani, Donge na Kisongoni kwa Mkoa wa
Kaskazini Unguja na Kiboje na Miwani kwa Mkoa wa Kusini Unguja.
Nao uongozi wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na
Mazingira ulieleza kuwa hali ya mifuko
ya plastiki hivi sasa ni nzuri licha ya kuwepo kwa baadhi ya watu wachache waliokuja
na mbinu mpya za kuuza mifuko milaini ya plastiki ambayo hutumika kwa kufungia bidhaa
mbali mbali vikiwemo viungo masokoni lakini hata hivyo waliahidi kupambana na watu
hao.
Uongozi huo ulieleza marufuku iliyowekwa kutokana
na sheria zilizopo ni kuwa mifuko ya plastiki yenye mikono na isiyo na mikono
yote hairuhusiwi kutumika hapa Zanzibar.
Uongozi huo pia, ulieleza kuwa hadi mwishoni mwa
mwaka huu itakuwa imeshachimba visima 50 kwa Unguja na Pemba na kueleza kuwa
azma ya kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inafanikiwa kwa wananchi wote
wa Unguja na Pemba.
Pia, ungozi huo uliahidi kuendelea kutoa taarifa
kwa wananchi juu ya utekelezaji wa majukumu yake kwa sekta zake zote zilizomo
katika Wizara hiyo sambamba na kutoa elimu kwa wananchi.
Wakati huo
huo, Dk.
Shein alikuna na uongozi wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko chini ya
Waziri wake Balozi Amina Salum Ali ambapo Waziri huyo alieleza kuwa thamani ya
uzalishaji viwandani katika mwaka 2016-2017 imeimarika na kufikia 4,879 milioni
kwa mwaka 2016 ikilinganishwa na milioni 4,170 mwaka 2015.
Aliongeza kuwa ukuaji huo umetokana na kuimarika
kwa uzalishaji katika viwanda vya usagaji nafaka, kiwanda cha maziwa cha Azam, Kiwanda
cha Sukari Mahonda, usarifu wa matunda na mboga mboga, viwanda vya maji ya
chupa pamoja na viwanda vya kokoto na matofali.
Pia, uongozi huo ulieleza majukumu yaliotekelezwa
na Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS),
hatua zilizochukuliwa katika utoaji na upatikanaji wa leseni kupitia
Baraza la Kusimamia Mfumo wa utoaji Leseni (BLRC) pamoja na majukumu ya Wakala
wa Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar (BPRA).
Nae Dk. Shein kwa upande wake aliupongeza uongozi
wa Wizara hiyo kwa kutekeleza vyema majukumu yake pamoja na kuendelea kusimamia
vyema masuala ya biashara, viwanda na masoko kwa lengo la kuimarisha uchumi na
maendeleo hapa nchini.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment