Na. Haji Nassor - Pemba.
OFISI ya Mkurugenzi wa Mashitaka
kisiwani Pemba, imesifia sana ushirikiano uliopo, baina yao na Kituo cha Huduma
za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, katika kuwafikia wananchi kuwapatia
elimu ya sheria, inayowapa ujasiri wa kudai haki zao.
Kauli hiyo
imetolewa na Mwanasheria wa Serikali kutoka Afisi hiyo, Juma Ali Juma wakati
akizungumza kwenye kipindi maalumu kilichorushwa na kituo kimoja ya redio,
kisiwani Pemba wakiwa na Afis Mipango wa Kituo cha hicho, Khalfan Amour
Mohamed.
Alisema ZLSC,
mewasaidia sana wao kama ofisi ya DPP, kwa vile wamekuwa wakishirikiana kutoa
elimu hata ule wakati, ambao ofisi yao haijapata uwezo wa kwenda vijijini.
Mwanasheria
huyo, alisema inatokezea Kituo cha huduma za sheria, kuwa na safari za
vijijini, hivyo watendaji wa DPP huangana nao, hivyo kuwaelezea wananchi kazi
na majukumu yao.
Alisema,
kuwepo kwa ZLSC inaonyesha sasa wananchi baadhi wameshawiva kitaaluma walau
kujua haki zao, kutokana na wengine kupata ujasiri wa kufuatilia haki zao
ofisini kwao, jambo ambalo, awali lilikuwa gumu.
“Mimi
nadhani usirikiano wetu uliopo baina yetu sisi na ZLSC, umezaa matunda sana,
maana tunaona wananchi wanapofika hata mahakamani, wanajitetea kisheria sio
maneno matupu”,alifafanua.
Hata hivyo
Mwanasheria huyo wa serikali, amewataka wananchi kuendelea kuitumia ofisi yao,
ili kupata ufumbuzi wa mambo yao ya kisheria, badala ya kusikiliza maneno ya
vijiweni.
Nae Afisa
Mipango wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, Khalfan
Amour Mohamed, alisema kituo kimekuwa na kazi kubwa ya kuwafikisha taaluma ya
sheria wananchi.
Alisema,
sasa wananchi kadhaa wamepata uwelewa mkubwa wa kuzifuatilia haki zao kwenye
vyombo vya sheria, wakiwa na uthubutu jambo, ambalo hapo awali halikuwepo.
“Sasa
wananchi wanauwelewa mkubwa wa kuzitambua haki zao, tofauti na zamani na sasa
wakienda mahakamani, DPP au kwenye taasisi nyengine za kisheria, hili tunajivunia”,alisema.
Baadhi ya
wananchi walizoungumza na mwandishi wa habari hizi, walisema taasisi za
kisheria lazima ziongeze kasi ya kuwaelimisha wananchi juu ya namna bora
kujenga uthubutu ya vyombo vya sheria.
Ali Hamza
Haji wa Machomane Chakechake, alisema pamoja na wananchi kupata, uwelewa lakini
bado, vyombo hivyo vinakumbwa na harufu ya rushwa.
Kwa upande
wake Hassina Hamad Omar, alisema wanawake lazima wajengewe uwezo wa kuvifikia
vyombo vya sheria, wanapokuwa wamedhulumiwa haki zao.
Hata hivyo
wananchi hao, waliwataka wanasheria kuhakikisha wanavitumia vyombo vya habari
kutoa elimu, ili wananchi wazidi kufahamu haki na wajibu wao.
Ofisi ya
Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar imeanzishwa mwaka 2002, sawa na Kituo cha
Huduma za Sheria kilichoanzishwa mwaka 1992 na kuanza kazi zake rasmi kisiwani
Pemba, mwaka 2002.
No comments:
Post a Comment