Habari za Punde

Itapendeza kama Rais Dk Shein atakuwepo Kenya kuwashuhudia vijana wa Zanzibar Heroes kesho

(Kutoka Maktaba) Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akimkabishi Kombe la Mapinduzi mwaka 2017 Nahodha wa Timu ya Azam John Bocco jana, baada ya timu hiyo kuifunga Simba kwa bao 1-0 katika mchezo uliomalizika Uwanja wa Amaan Mjini Unguja,[Picha na Ikulu.] 14/01/2017.


Na A K Khiari

Moja katika matukio makubwa ya kihistoria katika Taifa lolote huwa yanashuhudiwa na watu wengi na kubaki kuwa gumzo kwa muda mrefu.

Pia imekuwa ni kawaida kuona viongozi wa kitaifa wakati Timu zao za Taifa zinapofika fainali ya mashindano makubwa kuona viongozi wao wa kitaifa wakiacha na kuvunja shughuli zao ili nao waende kuwashuhudia wachezaji wanaowawakilisha wakipambana kwa ajili ya kulileta hadhi taifa lao.

Kwa muktadha huu Zanzibar imepata fursa adhimu ya kutinga katika fainali za michuano mikubwa pekee ambayo Zanzibar huweza kushiriki kama Zanzibar. Michuano ya CECAFA. Fursa hii imekuja baada ya miaka 22 ya kusubiri kwani mara ya mwisho kuchukua kombe hili ilikuwa mwaka 1995.

Zanzibar  Heroes haishiriki michuano mengine zaidi ya hii ya CECAFA na iliwahi kushiriki mashindano ya Dunia ya nchi ambazo hazina uwakilishi FIFA mwaka 2012.

Kesho Jumapili macho yetu yatakuwa katika mji wa Machakos nchini Kenya tukiwasubiri kwa hamu mashujaa wetu, maheroes wetu kutoka Zanzibar wakizidi kuushangaza ulimwengu wa soka kwa kuweza kufanya kile ambacho dunia inashindwa kuamini kama kinawezekana kwa kajinchi kadogo kisicho na ufadhili wa aina yoyote hakimo katika CAF wala FIFA lakini kimeweza kuwang’oa walio katika CAF na FIFA katika mashindano haya yanayofikia tamati hapo kesho Jumapili.

Kesho Jumapili wimbo wetu wa Taifa la Zanzibar utaimbwa, itapendeza kama Rais wetu atakuwepo.

Kesho Jumapili bendera ya Taifa letu la Zanzibar itapepea, itapendeza kama Rais wetu atakuwepo

Kesho Jumapili vijana wetu wanaweza kuibuka kidedea na kutwaa ubingwa wa kombe le Chalenji, itazidi kupendeza kama Rais wetu atakuwepo na kuwa miongoni mwa watu wa kwanza kukabidhiwa kikombe (Yaa Rabb tujaalie iwe hivyo kwa uwezo wako Yaa Rahmaan).

Kesho Jumapili kila mzanzibari mwenye uchungu na nchi hi na mwenye mapenzi na nchi hii atakuwa chini ya TV akiwashuhudia mashujaa wetu wana hakikisha kulirudishia heshima Taifa letu, itazidi kupendeza kama Rais wetu ataonekana kuwa mmojawapo ambao wapo uwanjani akishangilila na kuwahamasisha vijana wake wazidi kupata moyo.

Ninaungana na Mhe Waziri wa Afya, Mahmoud Thabit Kombo pale alipokuwa Baraza la wawakilishi aligusia nukta muhimu ya kuwapa vijana kile kinachoitwa ‘Moral Support’ hasa wakiona viongozi wakuu wa nchi wapo uwanjani inawezekana ikawa ndie mchezaji namba 12 wa timu kwa kuwapa morali.

Mheshimiwa Rais! Majuzi hapa ulitupa Darsa la uzalendo na kutueleza kuwa mzalendo ni yule aliyezaliwa pahala fulani kwenye asili yake ambapo pia, ni mtu mwenye mapenzi ya dhati sana ya kuitumikia nchi yake na kueleza maana ya uzalendo kuwa ni hali ya mtu kuwa na nasaba ya asili ya nchi ambaye pia hujitolea kwa hali na mali kwa ajili ya nchi yake.

Vijana wetu ni mfano mzuri wa kujitolea jinsi walivyoweza kufanya kazi ya ziada kufika fainali ya mashindano makubwa Afrika Mashariki na kati. Kwa ufupi walielewa darsa lako la uzalendo na kuuonesha kwa vitendo.


Mheshimiwa Rais! Dk Ali Mohamed Shein, kwa heshima na taadhima nafikisha ujumbe huu mfupi waunge mkono vijana kwa uzalendo: Itapendeza ukiwapo uwanjani Machakos kesho, ni matarajio vijana hawatokuangusha hasa wakikuona kwenye jukwaa wakati wakiimba wimbo wa Taifa la Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.