Habari za Punde

Zanzibar New year Bonanza kuzinduliwa Rasmi kwa mechi ya Soka.

 Kikosi cha Timu ya Gulioni FC
 Kikosi cha Timu ya Jang'ombe Boys

Ni kati ya Jang’ombe Boys na Gulioni.

Mashabiki waelezea matumaini kwa timu zao.

Tamasha la kimichezo la Zanzibar New Year Bonanza lililoandaliwa na Taasisi ya Rafiki Network linatarajiwa kuzinduliwa Rasmi siku ya Jumatatu ya tar. 25 Disemba kwa mechi ya mpira wa miguu kati Jang’ombe Boys na Gulioni Fc inayotarajiwa kuchezwa katika dimba la uwanja wa Aman saa 2:00 usiku. Mgeni Rasmi katika mchezo huo atakua Kocha wa timu ya Zanzibar Heros Nd. Hemed Morocco.

Rais wa Taasisi hiyo Nd. Hamad Hamad, amesema maandalizi  ya mchezo huo yamekamilika na kuongeza kwamba tasisi yake imejipanga vya kutosha kuhakikisha kwamba inaimarisha michezo hapa Zazibar.

Nae Rais wa timu Jang’ombe boys Nd. Ali Othman Ali amesema timu yake imefarijika sana kupata mwaliko wa kucheza na timu ya Gulioni ambapo timu itakayoibuka mshindi itapata kombe na fedha taslim. Akizungumza katika kipindi cha michezo ya wiki ‘coco sport’ kinachorushwa hewani kila Jumamosi kupitia kituo cha Redio cha Coconut FM, bwana Ali amesema awali pambano hili lilipangwa kufanyika tarehe 31 mwezi huu ambapo ilitarajiwa kuwakutanisha na mahasimu wao Taifa ya Jang’ombe.

Nd. Ali ameelezea sababu za kufutwa kwa mechi hiyo kuwa ni kupisha michuano yenye hadhi na taswira ya urithi na uzalendo wa nchi maarufu kama Mapinduzi Cup. Amefafanua kwamba kutokana na kuongezeka kwa idadi ya timu zinazoshiriki michuano hiyo ratiba ya Mapinduzi cup imelazimika kuanza mwishoni mwa mwezi huu.

Nae shabiki maarufu wa timu ya Jang’ombe boys Nd. Kassim Jecha amesema anamatumaini makubwa kwamba timu yake itaibuka na ushindi na kuandika historia wakati tukielekea mwaka mpya 2018.

Nae Rais wa timu ya Gulioni fc amesema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na kwamba timu yake ipo katika hali nzuri kuweza kuibuka mshindi katika mchezo huo.


Mechi hiyo ya mpira wa miguu ni sehemu ya bonanza la kimichezo la Zanzibar New Year Bonanza ZNYB, ambapo mbali na mchezo huo kutakua na Ngoma za mitaani ‘Street dance’ na Ngoma za asili zitakazochezwa Ngome Kongwe tarehe 29 Disemba, Michezo mbali mbali ya watoto itakayochezwa kule Fumba tarehe 30 Disemba na mashindano ya baiskeli kutoka Makunduchi hadi Uwanja wa Amani tarehe 31 Disemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.