Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Aweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Uwanja wa Mau Tse Tung leo.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif AliIddi akiweka Jiwe la Msingi la Uwanja wa Michezo wa Mao Tse Tung Uliopo Mtaa wa Mpirani Kikwajuni Mjini Zanzibar.kushoto Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud na kushoto Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utalii Utamaduni na Michezo Omar Hassan King na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe Zuberi Ali Maulid wakishuhudia uwekaji wa jiwe hilo.  
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Omar Hassan Kingi akitoa maelezo ya kiutendaji wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la Msingi wa Uwanja wa Mao Tse Tung.
Baadhi ya Wachezaji wa Mchezo wa Mpira wa Vinyoya waliohudhuria sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi lka Uwanja wa Maon Tyse Tung.


Na.Othman Khamis.OMPR. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ujenzi wa Viwanja vya Michezo Nchini uliomo ndani ya Programu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar unaudhihirishia Ulimwengu azma ya Zanzibar ya kutaka kukuza sekta ya Michezo Nchini ili irejee katika hadhi yake Kimataifa.

Alisema Viwanja hivyo vitakapokamilika vitaweza kusaidia uzalishaji wa Wanamichezo  bora watakaoiweka Zanzibar  katika Ramani ya Dunia kimichezo kama walivyofanya Zanzibar  Heroes na Wanakabumbu wa Soka la Ufukweni Zanzibar Beach Sand Heroes.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akiweka jiwe la msingi la Ujenzi wa uwanja wa Michezo wa Mau Tse Tung ikiwa ni muendelezo wa harakati za shamra shamra za sherehe za maadhimisho  ya kutimia Miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

Alieleza kwamba ujenzi wa Uwanja wa Mau Tse Tung ni jitihada kubwa zinazochukuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein katika kuendeleza michezo ambazo zinastahiki kupongezwa na wanapenda michezo Nchini.

Balozi Seif alisema jitihada hizo tayari zimeanza kuonekana moja kwa moja  katika Mpango wa Ujenzi wa Viwanja vya Michezo katika Wilaya zote Unguja na Pemba kwa kuanzia Kiwanja cha Kitogani ndani ya Wilaya ya Kusini katika Kisiwa cha Unguja.

Alisema Ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Mao Tse Tung ambao unagharamiwa na  Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni sehemu ya Mkakati wa Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015/2020 katika kuendeleza Sekta ya Michezo.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Uwanja huo una historia kubwa kutokana na kupewa Jina la Rais wa mwanzo wa China Marehemu Mao Tse Tung jambo ambalo Wazanzibari wana kila sababu ya kujivunia  kuwa miongoni mwa Nchi Tatu za Afrika ikitanguliwa na Senegal na Namibia zilizopata Heshima kutoka Taifa la China.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaomba Wanamichezo na Wananchi wote watakaopata fursa ya kuvitumia Viwanja hivyo baada ya kukamilika kwake kuendeleza Utamaduni wa kutunza mazingira yaliyo ndani ya Viwanja hivyo ili wafadhili wa Miradi hiyo waone kwamba misaada wanayotoa  inaendelea kutunzwa na kuthaminiwa.

Aidha aliutaka Uongozi wa vyama vya Michezo kupitia Vilabu wanavyovisimamia waanze kujipanga  namna ya jinsi ya matumizi yake hasa kwa kuzingatia Viwanja vyenyewe vinajengwa kwa ajili ya matumizi ya Jamii kwa ujumla wake.

Aliishukuru na kuipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kwa jitihada inazoendelea kuchukuwa katika kusaidia kugharamia ujenzi wa Kiwanja cha Mao Tse Tung kikitanguliwa na kile cha mwanzazo cha Amaan kilichojengwa mnamo Miaka ya 70.

Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Omar Hassan King alisema Uwanja wa Mao Tse Tung  utakaokuwa wa Kijamii zaidi tofauti na viwanja vyengine vya Michezo unatarajiwa kugharimu Dola za Kimarekani Milioni Tano sawa na shilingi za Kitanzania Bilioni 15.

Alisema Bilioni 11 sawa ya Yuan Milioni 29 zinatolewa na Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China na Shilingi Bilioni 4 zitatolewa na Sewrikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya kuendeleza ujanei huo.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utalii Utamaduni na Michezo Omar Hassan King alisema mradi wa ujenzi wa  Uwanja huo unahusisha pia uimarishwaji wa Miundombinu  ikiwa ni pamoja na  ujengaji wa viwanja viwili vya Michezo wa Mpira wa Miguu ambavyo vyote vitawekewa Nyasi Bandia kwa lengo la kuwa na hadhi ya Kimataifa.

Alisema ipo sehemu itakayokuwa na Jengo la Michezo ya ndani { Indoor Games } kwa ajili ya Mpira wa Meza, Wavu, Pete, Majengo Mawili kwa matumizi ya Ofisi pamoja na kuwekwa zana  na Vifaa vya mazoezi vitakavyohimili hali zote za Hewa ukiwemo pia uzio utakaouzunguuka Uwanja wote.

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo aliishukuru Wizara ya Kilimo, Mali Asili, Mifugo na Uvuvi kwa kusaidia Rasilmali ya Mchanga inayotumika zaidi kwenye ujenzi wa Mradi huo ambao ndio changamoto kubwa iliyokuwa ikiwasumbuwa Wakandarasi wa Ujenzi huo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Pen Yang  aliithibitishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwamba kazi ya ujenzi wa Uwanja wa Mao itaendelea kutekelezwa ili ikamilike katika kipindi kilichopangwa.

Bwana Pen Yang Uwanja wa Michezo wa Mao utaendelea kubakia katika Historia ya Uhusiano wa muda mrefu ulkiopo kati ya China na Zanzibar ulioanza mara tu baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

Mwakilishi huyoi wa Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar alisema kwamba Kiongozi wa Taifa la China alitia saini Mkataba wa ushirikiano kati ya Nchi hiyo na Bara la Afrika ikihusishwa miradi tofauti ya maendeleo ikiwemo Sekta muhimu ya Michezo.

Ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Mau Tse Tung  uliopo Mtaa wa Mpirani Kikwajuni ulioanza mapema Mwezi Mei Mwaka 2017  unafanywa na Kampuni ya Kimataifa ya Zhengtai Group ya Nchini Jamuhuri ya Watu wa China unatarajiwa kukamilika rasmi ifikapoMwezi Oktoba Mwaka huu wa 2018.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.