Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Shein: Uhaba wa Madawa Kuwa Historia Kuanzia Julai 2019


                                           

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE

  Zanzibar                                  5.01.2018

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuanzia mwezi Julai mwaka 2019, Zanzibar haitakuwa tena na tatizo la uhaba wa dawa kwa magonjwa yote yanayowakabilia wananchi wake.

Alisema hilo linawezekana, kutokana na uchumi wa Zanzibar kuimarika hatua kwa hatua, hivyo wananchi wa Zanzibar wataondoka na shida walionayo hivi sasa, kwa uhaba wa dawa uliopo kwenye vituo vya afya pamoja na hospitali kadhaa.

Dk. Shein alieleza hayo leo, huko katika uwanja mpira skuli  ya Michenzani mara baada ya kukifungua kituo kipya cha afya cha Michenzani wilaya ya Mkoani, ikiwa ni shamra shamra za miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema serikali inapotoa ahadi zake kwa wananchi huzitekeleza kwa wakati, hivyo nalo tatizo la kuondoa ubaha wa dawa kwa mujibu wa magonjwa yaliopo Zanzibar, linatarajiwa kuondoka kuanzia mwezi wa saba mwaka 2019.

Dk. Shein alieleza kuwa, zipo ahadi kadhaa amezitoa kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuipandisha hadhi hospital ya Abdalla Mzee na kuwa ya Mkoa sambamba na kuingiza vifaa vya kisasa jamboa mbalo limeshakamilika.

Alieleza kuwa, jengine ambalo ameliahidi na kulitekeleza ni kufuta michango ya elimu ngazi za msingi na sekondari, hivyo na hilo la ununuzi wa dawa zote linawezekana mara moja.

Alieleza uchumi wa Zanzibar umekuwa ukikua siku hadi siku, licha ya ongezeko la idadi ya watu na mahitaji, kutoka watu 300,000 mwaka 1964 hadi sasa kufikia milioni 1.5.

“Kutokana na kuimarika kwa uchumi, leo natoa nahidi kwenu nyinyi wananchi, kuwa kuanzia mwezi wa saba mwaka 2019, dawa zote zitapatikana katika vituo vyote vya afya na hospitali za serikali”,alifafanua.

Kuhusu matibabu, alisema serikali inadhamiria kuleta kifaa cha kisasa cha kuchunguuzia maradhi yote EMRI, kwenye hospitali ya Mkoa ya Abdalla Mzee Mkoani.

Alisema kifaa hicho ambacho kwa sasa kipo hospitali ya rufaa ya Mnazi mmoja pekee, kitawasaidia sana wananchi wa Pemba na hasa wanaotumia hospital ya Abdulla Mzee Mkoani.

Hata hivyo, kuhusu hospitali ya Chakechake, alisema serikali haijaisahau na inajipanga kuhakikisha inaifanyia matengenezo makubwa, ili iwe ya haiba na ya kisasa.

Akitoa historia fupi ya Mapinduzi  sambamba na sekta ya afya Dk. Shein alisema kuwa hadi kufanyika kwa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, kulikuwa na vituo vya afya 36 Unguja na Pemba ambapo hivi sasa vipo 189 na hospitali 12 ambapo wakati huo zilikuwa 5 tu.

Alieleza kuwa hapa Zanzibar zipo sababu kadhaa kwa kufanyika kwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964 ikiwa ni pamoja na uonevu na kusisitiza kuwa kabla ya Mapinduzi Wazanzibari hawakuwa na fursa za kuendesha shughuli zao mbali mbali za kimaendeleo na kukabiliwa na unyonge wa hali ya juuhuku demokrasia ikifinywa.

Alieleza kuwa, katika kutafuta ukombozi kutoka kwa wakoloni, mwaka 1957 kulifanyikwa uchaguzu mkuu, chini ya ASP wakiongombea viti sita, na ASP kupata viti vitano ingawa hawakupea serikali.

“Siasa ya vyama vingi hapa Zanzibar sio mpya, maana hata mwaka 1961 kulifanyika uchaguzi mwengine na ASP iliibuka na ushindi wa majimbo 10, kwenye majimbo 22 yaliokuwa yakiwania na vyama vitatu kwa wakati huo”,alieleza

Alieleza kuwa, kutokana na madhila hayo ndio maana muasisi wa mapinduzi hayo marehemu Abeid Amani Karume, aliamua kufanya mapinduzi kwa lengo la kuwakomboa wananchi.

Alisema, baada ya hayo alitangaaza huduma kadhaa kuwa bure, ikiwa ni pamoja na elimu, matibabu na suala la ardhi kutaangaza kuwa ni mali ya serikali.

“Muasisi wetu, alifanya mapinduzi, kwa lengo la kuwakomboa wananchu, na leo hii kila mmoja amenufaika na mapinduzi hayo, huduma za kijamii zote zimesogezwa karibu, na leo twamshukuru na twaendeleza”,alifafanua.

Katika hatua nyengine Dk. Shein, amewataka wananchi wa Michenzani na vijiji jirani, kuhakikisha wanakilinda na kukienzi kituo hicho cha afya, ili kiweze kidumu huku akiwasisitiza waende kutibiwa kituo humo kwani afya haina chama wala haina mbadala.

Nae Waziri wa Afya Zanzibar Mahamoud Thabiti Kombo, alisema kwa sasa wamejiwekea lengo kuwa kila mwaka wapate madaktari 40 wapya kuanzia mwaka 2018.

Alieleza kuwa, kwa sasa wanayomadaktari 150 ambapo hadi mwaka 2020 kwa mpango huo wa madaktari 40 kila mwaka watakuwa na madaktari 270, ambapo alisema kutokana na idadi ya wazanzibar milioni 1.5 dakatri mmoja atakuwa anahuwadumia watu 5880.

“Hivi sasa wapo vijana wetu wanaendelea na masomo katika vyuo vya ndani na nje ya nchi, ambapo wakimaliza watakuja serikali moja kwa moja”,alifafanua.

Kituo cha Afya cha Michenzani wilaya ya Mkoani Pemba, ambacho awali kiliwekewa jiwe la msingi na rais huyo wa Zanzibar mnamo mwaka 2012, ambapo kilianza na kwa nguvu za wananchi, ambapo pia wameshajengewa nyumba ya daktari kwa msaada wa Milele Foundation.

Mapema Naibu Katibu mkuu wizara ya Afya Zanzibar Halima Salum Maulid, alimpongeza rais wa Zanzibar kwa hatua yake, ya kuwaongezea fedha kwenye bajeti yao kuu, kutoka shilingi bilion 7 hadi shilingi bilion 10 kwa ajili ya ununuzi wa dawa.

Alisema hatua hiyo, ndio itakayowahakikishia upatikanaji wa dawa za uhakika kuanzia mwakani, jambo ambalo linawaondoshea usumbufu wananchi wa Unguja na Pemba.

“Kwa sasa, sisi wizara ya afya, hatuna tatizo kubwa la dawa, maana asilimia 95 ya dawa tunazo, na kwa kutokanana bajeti yetu kutononeka, basi hwenda ikaondoka kabisa”,alieleza.

Katika hatua nyengine, Naibu Katibu Mkuu huyo, wizara ya Afya alisema, ujenzi wa kituo hicho cha afya ambacho ujenzi wake umeanza kwa nguvu za wananchi, na serikali ambapo hatua za kuamalizia walipata ufadhili wa “Milele Foundation”.
Alieleza kuwa tayari, taasisi hiyo imeshajenga vituo nane vya afya, ikiwa Unguja na Pemba idadi ya vinne, sambamba baadhi ya vifaa husika.

“Wenzetu hawa wa Milele, wamekuwa wakitusaidia sana kwenye sekta hasa ya afya, na wameshajenga vinne kwa hapa Pemba, tunawashukuru sana”,alieleza.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.