Habari za Punde

Rais Dk Shein azindua soko jipya la Tibirinzi Chake Chake Pemba ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 54 ya MapinduziSTATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                                                               5.01.2018
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa miongoni mwa malengo ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 ni kufanya hali za maisha ya Wazanzibari kuwa bora na ujenzi wa soko la Tibirinzi ni miongoni mwa malengo hayo na sio kichocheo cha kubaguana kwa vyama, dini, jinsia au mahala mtu anapotokea.

Dk. Shein amesisitiza kuwa jengo hilo jipya la soko ni ukombozi kwa wakulima, wafanyabiashara, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali pamoja na wananchi wote kwa jumla kwa  kuweza kuongeza kipato chao ili maisha yao yaweze kuwa bora.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kulizindua soko jipya la Tibirinzi Chake Chake Pemba.

Dk. Shein alisema kuwa soko hilo si vyema likahusishwa na masuala ya kisiasa kwani ni soko la watu wote wa vyama vyote, dini zote na jinsia zote huku akiwataka wafanyabiashara watakaolitumia soko hilo kuleta bidhaa zenye ubora zitakazolingana na hadhi ya soko hilo.

Alisema kuwa ujenzi wa soko hilo ni katika hatua za kutafsiri Mapinduzi ya mwaka 1964 kwa vitendo kwa kuwaletea wananchi maendeleo zaidi bila ya ubaguzi.

Alieleza kuwa  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatekeleza Sera mbali mbali zikiwemo zinazolenga kuinua kipato cha wananchi na kupunguza umasikini…

Sambamba na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kulitunza na kulienzi soko hilo ikiwa ni pamoja na kudumisha usafi wa soko hilo kwani usafi ni jambo la lazima na halina mbadala.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza mafanikio sambamba na azma ya Mapinduzi Matukufu ya Januri 12, 1964 ambayo yamewakomboa wananchi wa Zanzibar na kukata minyororo ya chuki na udhalimu sambamba na kunyanyaswa.
Alieleza madhumuni makubwa ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuwa huru na hatua ambayo imepekea kupanga mambo bila ya kuingiliwa na mtu na kuweza kuongoza nchi sambamba na kuandaa mipango ya muda mrefu na muda mfupi na wakati.

Alieleza kuwa Zanzibar imepata maendeleo makubwa katika kukuza uchumi wake ndani ya kipindi cha miaka 54 huku akieleza kuwa  mabadiliko makubwa ya kiuchumi, sera ya serikali maisha ya watu ambayo yote hayo ni maendeleo.
“Leo naambiwa ndege zinazokuja Pemba hivi sasa hazitoshi, meli hazitoshi watu wanasafiri kila leo hayo yote ni maendeleo na kukua kwa uchumi.. jengo hilo ni lazima tulipe heshima yake” Alisema Dk. Shein.

Nae Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Hamad Rashid Mohammed alieleza kuwa kuna kila sababu ya kumuenzi na kumuombea dua Rais Dk. Shein kwa maendeleo makubwa sambamba na juhudi anazozichukua katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.

Waziri Rashid alisema kuwa maendeleo yanayoonekana na kwa mara ya kwanza katika historia wafanyakazi wameweza kulipwa mshahara mara mbilili wanaopata, kuzalisha mpunga tani 39 elfu, kuwepo na mchele kutoka Zanzibar pamoja na maendeleo mengineyo ikiwemo kuimarika kwa miundombinu.

Aliongeza kuwa Rais Dk. Shein kuwa Zanzibar imebaki salama kutokana na hekima yake na hakuna mpasuko na kumekuwa na amani kubwa kwani huwezi kupata maendeleo kama hakuna amani ya nchi.

Alieleza kuwa Dk. Shein ni kiongozi anaetaka kila mmoja kutoa maamuzi na kumshirikisha kufanya hivyo na ndicho kilichomfanya Dk. Shein kuweza kuwatumikia watu tena bila ya ubaguzi.

“Kina mzee Karume wasingeweza kupindua nchi kama wasingekuwa na nia nzuri… Mwenyezi Mungu peke yake ndie anaechagua kiongozi.. kwani katika mazingira haya nani angelijua kuwa Hamad Rashid angekuwa Waziri wa Kilimo…unapomkuta kiongozi anajenga fitna kwa watu anajenga fitna kwa watu, unapomkuta kiongozi anajenga makundi hata salamu alaykum haitikiii ni kweli huyu mtu wa peponi?”,aliuliza Hamad Rashid.

Waziri Rashid aliwataka baadhi ya wananchi kisiwani humo kuwacha siasa na badala yake washughulikie mambo ya msingi na yenye kuleta maendeleo huku akieleza kuwa Serikali inalengo la kujenga masoko makubwa mawili huko Malindi mjini Zanzibar na soko jengine litajengwa huko kiswani Pemba.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Joseph Abdalla Meza alieleza kuwa soko hilo ni kati ya masoko manne yaliojengwa Zanzibar kupitia Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVAP) inayogharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aliongeza kuwa program hiyo inasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kwa Zanzibar na kueleza kuwa ujenzi wa soko hilo ulianza mwezi wa Aprili 2016 ambapo wazabuni 12 waliomba kufanya kazi hiyo na baada ya tathmini Kampuni ya ZECCON LIMITED ya Zanzibar ndiyo iliyoibuka mshindi na kupata tenda hiyo na kuingia mkataba wa ujenzi kwa gharama za TZS Milioni 972.2 ambapo kati ya hizo milioni 48.6 zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema akuwa soko hilo lina vibaraza 76 vitakavyokabidhiwa kwa wafanyabiashara ambapo soko hilo lina chumba cha baridi kwa ajili ya kuhifadhia samaki na chumba maalum kilichotengwa kuwekewa mtambo wa kutengenezea barafu ambao utawasaidia wavuvi kutumia barafu hizo wakati wakiwa baharini.

R
ajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.