Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Shein, Ajumuika na Vijana na Wanafunzi Katika Chakula Maalum Aliowaandalia

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  leo ameungana pamoja na vijana na wanafunzi walioshiriki katika Maadhimisho ya Sherehe za kutimiza miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika chakula cha mchana alichowaandalia kutokana na ushiriki wao katika sherehe hizo zilizofanyika Januari 12 mwaka huu.

Hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya Makao Makuu ya KVZ, Mtoni mjini Unguja, na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akiwemo makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pamoja na baadhi ya viongozi wa vikosi vya SMZ.

Katika shukrani zake Dk. Shein kwa vijana na wanafunzi hao zilizotolewa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi Gavu, alitoa pongezi kwa kushiriki kikamilifu sambamba na kufanikisha vyema sherehe hizo zilizofanyika Januari 12, 2018 katika uwanja wa Amaan mjini Unguja.

Waziri Gavu alitoa shukurani za dhati kwa walimu, wakufunzi, wasimamizi na washiriki wote walioshiriki katika shuhuli za halaiki na kuzipamba sherehe hizo ambazo zilifana kwa kiasi kikubwa kutokana na ushiriki wao.

Alieleza kuwa ushiriki wao katika sherehe hizo ni dalili njema na mwenendo mzuri wa uzalendo kwa nchi yao huku akieleza imani yake kuwa vijana hao wataendelea kuyaenzi na kuyalinda Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 kutokana na umuhimu wake mkubwa katika maisha ya Wazanzibari na Watanzania wote kwa ujumla.

Alisisitiza haja ya kuendelea kuilinda amani na utulivu mkubwa uliopo hapa nchini ikiwa ni kielelezo madhubuti cha kuendelea kuyalinda na kuyaenzi Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964.

Ni utamaduni aliouweka Dk. Shein wa kuwaandalia chakula cha mchana vijana na wanafunzi walioshiriki katika sherehe za Mapinduzi kwa kila mwaka ambapo hapo kesho atawaandalia chakula kama hicho Vikosi vya Ulinzi na Usalama vilivyoshiriki katika Maadhimisho ya Sherehe za kutimiza miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika eneo hilo la viwanja vya Makamo Makuu ya KVZ, Mtoni mjini Unguja.

Rajab Mkasaba, Ikulu

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.