NA/
ASHA BAKARI --- PEMBA
Wajasiriamali
wa kikundi cha ushirika cha Tekeleza
waliopo Mavungwa Shehia ya Mbuzini Mkoa wa Kaskazini Pemba, wamesema kutokana
na hali za kimaisha zilivyo hivi sasa ni kheri kwa akina mama kushiriki katika
vikundi mbalimbali vya ushirika kwani manufaa ni makubwa kiasi ambacho hata
baadhi ya wanaume wanaweza kupata msaada kutoka kwa wake zao.
Wajasiria
mali hao waliyaeleza hayo mbele ya Waandishi wa habari waliofika katika
ushirika huo kwa lengo la kuwatembelea na kutazama mafanikio na changamoto
mbalimbali wanazokabiliana nazo katika uendeshaji wa shughuli zao.
Walisema
kupitia ushirika wa Tekeleza, ambao ndio kituo kikuu cha ushirika
Mavungwa, wamefanikiwa kufungua miradi
yao mbalimbali na hivi sasa wanaiendeleza vizuri na hali za kiuchumi zinazidi kuimarika.
Bi Sharifa
Khamis, ambae ni Mwanachama wa kikundi
hicho kilichojikita zaidi katika ufugaji na kilimo, alisema kupitia
Tekeleza amefanikiwa kupata elimu ya ujasiriamali na kuamua kuifanyia kazi na
hadi sasa ameshafungua mradi wa kufuga bata mzinga akishirikiana na wananchi
wengine .
''Nashuruku
tunapata pesa , hali sio kama mwanzo, sasa naweza kujipatia mahitaji muhimu
katika maisha , nimeshanunua makabati yangu ya kuwekea nguo na cherahani'',
alisema mama huyo.
Akielezea
mafanikio zaidi aliyayapata, alisema jambo kubwa na la msingi mpaka hivi sasa
anamudu kuwasomesha watoto wake kwa kuwalipia ada za Skuli na huduma nyengine
jambo ambalo alisema kwake ni faraja kubwa.
Mwanachama
mwengine ambae anaonekana kufurahia uwepo wa kikundi cha Tekeleza, Bi Lela Seif
Khamis, alisema mara tu ulipokuja mradi wa kujifunza mambo mbalimbali ya
ujasiriamali katika kikundi hicho aliungana na wenzake kutekeleza majukumu ya
kikundi huku akipokea taaluma tofauti zilizokua zikimletea mwanga katika
maisha.
Alisema
kutokana na upeo wa maarifa waliokua wakipatiwa hivi sasa ameshajiwezesha
mwenyewe na hali za kimaisha zinakwenda vizuri tofauti na ilivyokua awali.
''Sasa
naweza kumlipia mwanangu kila mwaka shilingi 15,000/= za Skuli, nimenunua friji
nauza juisi, nimejenga banda nauza uji ,
nilikua sina uwezo wowote kipindi cha nyuma lakini hivi sasa mambo yanakwenda
vizuri , maana muda mwengine hata mumewangu huchachiwa na akataka nimuazime
chochote na nikampatia '', alisema Lela.
Lela,
alieleza ukiachilia mbali mafanikio hayo
lakini pia hivi sasa anaona ndoa yake ipo salama kwani ikitokea mume amekosa,
chakupika hakikosi ndani ya nyumba na akirudi chakula tayari wanakula na mambo
yanaendelea kama kawaida.
Kwa
upande wake, Katibu wa kikundi cha
Tekeleza Muhammed Bakar Omar, alisema lengo la kikundi chao ni kuondosha utegemezi
wa kimaisha kwa wananchi na kila mmoja
awe na nyenzo ya kujipatia kipato katika maisha.
Alifahamisha
kituo chao cha Tekeleza ni katika mradi wa ASSP
ambao umelenga kuwakomboa wananchi kiuchumi na hadi hivi sasa harakati
za kuwaelemisha zinaendelea vizuri ikiwamo katika sekta ya Kilimo na ufugaji.
'' Tunawafundisha
mbinu bora za kilimo na ufugaji , yoyote atakaekuwa tayari nasi huwa tayari
kumwelekeza na kisha anaona matunda yake'' ,alisema katibu huyo.
Katibu
huyo, alieleza ingawa mafanikio ni mengi katika kikundi hicho kama vile kutoa
wanachama wengi ambao wanajitegemea lakini pia wanakabiliwa na changamoto
mbalimbali kama vile ukosefu wa pesa za kumalizia jengo pamoja na kutokuwepo kwa
huduma ya umeme ambayo ni muhimu sana kutokana na kazi zao.
Hivyo
aliwaomba wadau wa maendeleo na washirika wengine kujitokeza kusaidia katika
utatuzi wa changamoto hizo ili yale malengo yaliyokusidiwa yafikiwe kwa wepesi
zaidi.
No comments:
Post a Comment