RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi
Duniani (Mei Mosi), zinazotarajiwa kufanyika Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Katika maadhimisho hayo, Dk. Shein
anatarajiwa kupokea maandamano ya wafanyakazi wa sekta za umma na sekta binafsi
ambapo pia, salamu mbali mbali zitatolewa zikiwemo kutoka Shirika la Kazi
Duniani (ILO), Jumuiya ya Waajiri Zanzibar (ZANEMA), salamu za Waziri, Mkuu wa
Mkoa, risala ya wafanyakazi na hatimae, Rais atatoa zawadi na kuwahutubia wafanyakazi.
Kila ifikapo Mei Mosi ya Kila mwaka,
Zanzibar huungana na nchi nyengine duniani katika kuadhimisha Siku ya
Wafanyakazi Duniani ambapo hapo mwaka jana maadhimisho hayo yalifanyika katika kiwanja
cha Mpira Mahonda, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kauli mbiu ya mwaka huu katika
maadhimisho hayo inasema ‘Njia Pekee ya Kukuza Uzalishaji na Kuimarisha Huduma
ni Kujadiliana na Kujali Ushirikishwaji”.
Katika hotuba zake mbali mbali anazotoa
Rais Dk. Shein amekuwa akisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itaendelea na utaratibu wake wa kuzilinda haki za wafanyakazi na kuimarisha
maslahi ya wafanyakazi hatua kwa hatua.
Katika hotuba yake ya kuzindua Baraza la
Nane la Wawakilishi tarehe 11 Novemba mwaka 2010 Rais Dk. Shein alieleza bayana
mtazamo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba kuhusu wafanyakazi ambapo
alisema “Rasilimali moja kubwa ya nchi ni wafanyakazi ambapo ndio msingi wa
kujenga uchumi na maendeleo yote ya nchi”.
Aidha, katika kutilia
mkazo suala la umuhimu wa kushirikiana na vyama vya wafanyakazi alisema kuwa “
Maslahi bora ya wafanyakazi popote ni ajenda yetu na tutahakikisha mashirikiano
na chombo chao ‘Shirikisho la vyama huru vya wafanyakazi’ na kukuza mahusiano
mema”.
Kama inavyofahamika
kuwa wafanyakazi ni muhimu katika maendeleo ya Taifa lolote lile kwani ni
rasilimali inayotegemewa katika kuzalisha mali na kunyanyua uchumi wa nchi.
Kwa kutambua hilo
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikichukua hatua mbali mbali kujenga
mazingira mazuri kwa wafanyakazi ili waweze kuzalisha zaidi na kuongeza pato la
Taifa.
Siku hii ya Mei Mosi
inatokana na historia ya maandamano yaliyotokea
Chicago nchini Marekani mnamo mwaka 1886 ambapo zaidi ya wafanyakazi
300,000 waliandamana wakidai haki zao za msingi.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment