Habari za Punde

HABARI KUTOKA BARAZA LA WAWAKILISHI
Na Khadija Khamis – Maelezo     14/05/2018
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mhe, Mohamed Aboud  Mohamed amesema serikali inathamini asasi zisizo za kiserikali kama ZAPHA+ katika kusaidia mapambano dhidi ya ukimwi ili kuhakikisha  maambukizi mapya yanapungua hasa kwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24.
Hayo ameyasema wakati akijibu suala la  Mhe.Omar Seif Abeid  wa Jimbo la Konde huko katika kikao cha Baraza la Wawakilishi Chukwani  aliyetaka kujua  Serikali ina mpango gani wa kuzisaidia jumuiya kama ZAPHA+  ambazo zinajitolea kuhamasisha vijana kwenye mapambano na maambukizo ya virusi vya ukimwi ?
Amesema kuanzishwa kwa klabu maalum za Wilaya Micheweni na ZAPHA+ zenye lengo la kuwasaidia vijana wanaoishi na VVU ni jambo la kupongezwa na la kupigiwa mfano hii itasaidia kwa  serikali na asasi zisizo za kiserikali kupata takwimu sahihi ya maambukizi mapya ya ukimwi.
Aidha alisema kupitia Tume ya Ukimwi na Wizara ya Afya inashirikiana pamoja na Jumuiya ya  ZAPHA+ katika kuhakikisha kuwa inawajengea uwezo vijana ambao wanaoishi na virusi vya ukimwi  kwa kuwapatia elimu ya ujasiriamali ,kuwapa  fedha kwa ajili ya kuanzisha miradi midogo midogo ,elimu juu ya  ushauri nasaha  matumizi sahihi  ya   kupunguza makali ya VVU pamoja na kuwapa misaada ya chakula pale fursa zinapojitokeza  .
Wakati huo huo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za  SMZ Haji Omar Kheir amesema kasi ya engezeko la Idadi ya watu katika Wilaya ya Magharibi A na  B Iinasababisha kukosekana kwa huduma za kijamii ikiwemo  elimu, maji, miundombinu ya barabara na huduma nyenginezo .
Amesema ongezeko hilo la watu haliendi sambamba na ukuwaji wa uwekezaji katika miundombinu iliyopo na kushindwa kukidhi mahitaji halisi ya wananchi waliyopo katika wilaya hizo serikali baada ya kulitambua hilo ikaendelea na hatua za kuimarisha upatikanaji wa huduma za kijamiii kwa kuzingatia mipango na mipaka ya utawala iliyopo.
Aliyasema hayo wakati akimjibu Mhe. Machano Othman  Said  Jimbo la Mfenesini aliyetaka kujua jinsi ya ongezeko la watu wasiopungua 350,000 kwa mujibu wa sensa za 2012 idadi ambayo inaengezeka kila siku, Je Serikali haiyoni kwamba wakati umefika sasa wa kuanzisha mkoa wa kiserikali kama kilivyoamua Chama cha Mapinduzi?
 Aidha alisema hakuna mikakati mahsusi ambao serikali imeiweka kwa ajili ya kuondoa kero za wananchi wa wilaya hizo  badala yake serikali inaendelea kutatua kero za wilaya hizo kwa kuzingatia dira ya 2020 ya mpango mkuu wa kitaifa mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini MKUZA  na ilani ya uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi ya 2015 -2020 .
Alifahamisha kuwa  katika utekelezaji wa mikakati hiyo ya kitaifa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaimarisha huduma za kijamii kwa wilaya zote za Unguja na Pemba katika sekta ya elimu ,Afya pamoja na miundombinu ya barabara.
MWISHO
IMETOLWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.