MAKAMO Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk.Ali Mohamed
Shein amewaeleza viongozi wa CCM wakiwemo Mabalozi
kuwa njia pekee ya kuendeleza amani, utulivu na mshikamano ni kuwepo kwa
uongozi wa CCM madarakani.
Dk. Shein aliyasema hayo
katika mkutano kati yake na Mabalozi wa CCM wa Wilaya ya Dimani Kichama,
mkutano uliofanyika katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Mjini uliopo Amani mjini Unguja
huku akitumia fursa hiyo kueleza umuhimu wa ushindi kwa CCM.
Katika hotuba yake
alieleza kuwa amani, utulivu na umoja ndio Sera kubwa ya CCM na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na kusisitiza kuwa amani inadumi zaidi pale
inaposhughulikiwa na CCM, kwani viongozi wake wamekuwa wakiisisitiza amani na
kuitekeleza kwa vitendo.
Aidha, Dk. Shein alieleza
kuwa wapo viongozi wamechaguliwa na wananchi lakini wamekuwa wakiwapiga chenga
wananchi waliowachagua na hawaendi katika maeneo waliochaguliwa kwenda
kuwatumikia wananchi hao ikiwa ni pamoja na kuzitafutia ufumbuzi changamoto
zinazowakabili.
Makamo Mwenyekiti huyo
wa CCM Zanzibar alieleza kuwa iwapo hawana uwezo wa kuzitatua changamoto hizo
ni vyema wakawaeleze viongozi husika wakiwemo viongozi wa ngazi za juu wa chama
chao.
Dk. Shein alisisitiza
haja kwa viongozi wa CCM wakiwemo Wabunge, Wawakilishi na Madiwani kuwaeleza wananchi
mafaniko ya Serikali yao yaliyopatikana yakiwemo kuimarika kwa huma za jamiio
zikiwemo elimu, afya, biashara, mazigira na nyenginezo.
Aliwaeleza viongozi hao
wa Wilaya ya Dimani kuwa ni lazima kanuni na maadili ya chama hicho yafuatwe hasa
pale unapokaribia uchaguzi mkuu ili wawe wamoja kwa vitendo na kujidhatiti
katika kuiletea ushindi CCM.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alieleza juhudi zinazochukuliwa na Serikali anayoiongoza katika
kulitafutia ufumbuzi tatizo la maji tokea awamu ya kwanza ya uongozi wa SMZ,
ambapo hali ya matumizi ilikuwa ndogo kutokana na idadi ya watu wakati ule na
ilivyo hivi sasa.
Alieleza kuwa changamoto
kubwa iliyopo hivi sasa ni kupungua kwa maji katika vyanzo vya maji hasa kwa
vianzio vinavyotoa maji kwa mji wa Zanzibar na kusisitiza kuwa tayari Serikali
imeanza kulichukulia hatua suala hilo.
Alieleza kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar itaweka mtandao mpya wa maji katika mji wa Zanzibar na
ule mkongwe utafumuliwa kwani tayari visima kadhaa vimeshachimbwa na baadhi
yake vimeshawekewa vifaa na bado vifaa vyengine vimeshaagiziwa hivi karibuni
vitawasili.
Alirejea kauli yake ya
kulitafutia ufumbuzi tatizo la kutuama kwa maji katika eneo la Mwanakwerekwe
ambapo alieleza kuwa eneo hilo litajengwa ili maji yaende na yakienda yatoke
pamoja na kuwekwa mabomba makubwa kuelekea baharini na kusisitiza kuwa fedha
zipo zipatazo Dola milioni 33 za mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Aidha, alieleza kuwa
sehemu ya Pili ya Mradi wa Huduma za Jamii Mjini (ZUSP) ambapo sehemu ya pili
ni barabara yenyewe kujengwa upya na kuinuliwa na kwa eneo la Kibondemzungu
barabara nayo itainuliwa na kujengwa njia mbili ya kwenda na kurudi. Pia, alieleza
kuwa barabara ya Kiembesamaki nayo itainuliwa.
Hata hivyo, aliwataka
Mabalozi kushirikiana na Serikali katika kuwaelimisha wananchi juu ya usafi wa
mazingira kwa lengo la kupambana na maradhi mbali mbali.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa
CCM Zanzibar, Dk. Abdalla Juma Mabodi alieleza majukumu ya Mabalozi na
kusisitiza kuwa Mabalozi ni jeshi kubwa katika kuipatia ushindi na kueleza kuwa
Wilaya ya Dimani hakuna makundi ya CCM bali wote ni wamoja.
Mabodi alisisitiza kuwa
ni vyema kwa viongozi wa Chama kueleza mafanikio yaliopatikana kutokana na
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM pamoja na kwenda kwa wananchi kuwa
kusikiliza changamoto zinazowakabili.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa
Magharibi Mohammed Rajab Soud alizipongeza juhudi za Rais Dk. Shein na kutumia
fursa hiyo kueleza kuwa wanasikitishwa na baadhi ya watendaji ambao wanafanya
kazi kinyume na matakwa ya Serikali na wananchi.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya
ya Dimani Hussein Ali Mjema (Kimti) alimpongeza Rais Dk. Shein kwa juhudi zake
za kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwa vitendo pamoja na
kusimamia vyema amani na utulivu kuahidi kuendelea kushirikiana nae.
Nao Mabalozi wa Wilaya
ya Amani katika taarifa yao iliyosomwa na Balozi Mwanakheir Idd Ramadhan walimpongeza Rais Dk. Shein pamoja na
Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk. John Magufuli kwa kusimamia kwa nguvu Ilani ya
CCM na hatimae kupata maendeleo makubwa na
kupunguza kero kwa wananchi.
Walieleza kuwa CCM ndio
mtetezi wao na ndio sauti yao kwani ndio chama kinachotetea haki ya ukweli na ndio
chama wanachokiona kinachosimamia na kudumisha amani na utulivu.
Walieleza kuwa ushindi
wa CCM unatokana na wanaCCM wenyewe pamoja na wananchi wanaokiunga mkono chama
hicho kutokana na Sera zake lakini pia Mabalozi ndio nguvu kazi ya CCM kwa
kuwahamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la kudumu laMpiga kura.
Sambamba na hayo,
Mabalozi hao walieleza changamoto zilizopo katika Wilaya hiyo ya Dimani ikiwa
ni pamoja na uhaba wa maji safi na salama, ubovu wa barabara za ndani,uhamiaji
na ujenziholela, kilio cha Mwanakwerekwe na Kibondemzungu, kucheleweshwa kwa
ugawaji wa viwanja kwanajili ya kujenga kwa maeneoya Fumba na Bweleo na
nyenginezo.
Hata hivyo, Mabalozi hao
walimuhakikishia Makamo Mwenyekiti huyo kuwa wataimarisha umoja na mshikamano
ndani ya Chama chao na kufanya kazi kila inavyowezekana ili CCM ipate ushindi
mkubwa na kuweza kuendeleza amani na utulivu.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment