Habari za Punde

RC TANGA AAGIZA KOROGWE KUWA NA STENDI MOJA YA MABASI


Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela (kulia) akiteta jambo na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Godwin Gondwe kwenye kikao na wadau wa Korogwe juu ya hatma ya matumizi ya stendi mbili katika Mji wa Korogwe. Kikao hicho kilifanyika jana Juni mosi, 2018 kwenye Ukumbi wa Halmashsuri ya Mji Korogwe (Picha na Yusuph Mussa).


Na Yusuph Mussa, Korogwe                                                                                                    
MKUU wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela ametengua maamuzi ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji Korogwe ya kuruhusu kutumika kwa stendi mbili katika Mji wa Korogwe.

Na badala yake, ameagiza stendi itakayotumika ni ile ya Kilole ambayo Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli aliifungua Agosti 7, 2017, na kuachana na stendi ya zamani ya Manundu.

Aliyasema hayo jana Juni mosi, 2018 kwenye Mkutano uliofanyika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Korogwe na kuwashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo madiwani, wakata tiketi za mabasi, wafanyabiashara, watumishi na kamati za ulinzi na usalama za wilaya ya Korogwe na mkoa wa Tanga, na kufanya mikutano ya hadhara kwenye stendi hizo.

Pamoja na marufuku hiyo ya stendi ya zamani, pia ameagiza vituo vya maegesho ya magari kwenye barabara kuu ya Dar es Salaam kwenda Arusha kuanzia Mtonga, Mwembeni, Uwanja wa Sokoni, CRDB, Majengo na Kilole viondolewe.

"Kuanzia tarehe ya leo (Juni mosi) stendi ya mabasi itakuwa moja nayo ni Kilole. Na hiyo ni kutokana na kuongeza mapato ya Halmashauri ya Mji Korogwe. Lakini ni lazima turejee kwenye makusudio yetu ya kujenga stendi mpya, nayo ni kukidhi mahitaji ya wananchi kuweza kupata eneo nzuri na la kisasa katika kutoa huduma.

"Uwepo wa stendi ya zamani (Manundu) kufanya kazi, kunaharibu utaratibu tuliojiwekea, kwani badala ya mabasi kuingia Stendi ya Kilole, yanabaki stendi ya zamani, hivyo kuathiri ufanyaji wa shughuli kwenye stendi mpya. Lakini pia stendi zote zilizopo pembeni ya barabara kuu ziondolewe, zinachangia abiria na mabasi kutoingia stendi mpya" alisema Shigela.

Shigela alisema Stendi ya Manundu itumike kama daladala kwa magari yanayotoka kwenye kata za Halmashauri ya Mji Korogwe, bodaboda na bajaj na si vinginevyo, kwani hata idadi ya magari yanayoingia stendi ya zamani iliyoelezwa na madiwani kuwa hayazidi 10, siyo ya kweli, kwani zaidi ya magari makubwa 40 yanaingia stendi ya zamani kwa siku.

Hata hivyo, kabla ya kutoa maamuzi hayo, kwanza aliwasikiliza wadau mbalimbali kuhusiana na sakata hilo, ambalo limeleta mvutano mkubwa kati ya wanasiasa, watendaji na wananchi, huku akiwatanabahisha kuwa ni kweli stendi zote za zamani huwa hazifi, bali zibatumika kwa matumizi ya ndani kama daladala, na kutolea mfano Stendi mpya ya Mabasi Kange jijini Tanga, na ile ya zamani ya Ngamiani ambayo inatumika kwa daladala na mabasi ya shamba.

Awali, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Korogwe Hillary Ngonyani alijaribu kutetea hoja kwa nini madiwani kwenye Baraza Maalumu la Madiwani la Mei 25, 2018 waliamua kuweka stendi mbili zitumike.

Ngonyani alisema kila abiria kulazimisha aingie Stendi Kuu ya Mabasi Kilole ikiwemo wagonjwa na wafanya biashara na hasa kutoka vijijini, huko ni kuwaonea, kwani wanatumia gharama nyingi na kupoteza muda, hivyo busara iliwatuma wafungue stendi ya zamani ili magari kutoka vijiji vya wilaya ya Korogwe waweze kuitumia.

"Tuliona wananchi wetu wanapata shida kwa kuweka stendi moja ya Kilole, na hasa wagonjwa kutoka vijijini. Pia kuna wafanya biashara na watu wengine ambao wanakuja mjini Korogwe kwa shughuli mbalimbali, lakini wanalazimishwa kwenda hadi stendi mpya.

"Hivyo tukaona kwa vile halmashauri na Chama Cha Mapinduzi, na hata Rais Magufuli anasema ni Rais wa wanyonge, ni lazima tuangalie maslahi ya wananchi, basi tukaona tuwaruhusu watumie stendi ya zamani kwa mabasi ambayo hayazidi kumi. Na hata hivyo tulijiridhisha kuwa kuwepo kwa stendi ya zamani hakupunguzi mapato ya stendi mpya" alisema Ngonyani.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji (TD) Korogwe Jumanne Shauri alisema kutumika kwa stendi mpya na ya zamani kwa wakati mmoja kunachangia kushuka mapato ya halmashauri, kwani stendi hizo zinategemeana.

"Nataka niseme kweli mbele ya Mungu na kikao hiki. Na hapa ninapozungumza nimefunga. Kuendelea kutumika kwa stendi mpya na stendi ya zamani kunapunguza mapato ya halmashauri, kwani stendi hizo zinategemeana.

"Ili stendi mpya iweze kufanya kazi ni lazima mabasi ya shamba (vijijini) yaingie stendi hiyo, ambapo wakati wanasubiri mabasi ya kuwapeleka mikoa mbalimbali, watakula chakula na kununua bidhaa mbalimbali, hivyo kuifanya migahawa ndani ya stendi kupata wateja.

"Lakini kama mabasi hayo yataishia stendi ya zamani, wapiga debe watawashawishi abiria kusimama kwenye parking (maegesho) kwenye barabara kuu na kuwatafutia usafiri, hivyo halmashauri kukosa mapato. Na hiyo siisemi mimi, bali kamati mbili zilizoundwa zimeonesha hivyo, na mapato ya stendi mpya yameshuka kutoka sh. milioni 41 Oktoba, mwaka jana na kufikia sh. milioni 26 Aprili, mwaka huu" alisema Shauri.

Hivyo Shauri alimueleza Mkuu wa Mkoa kuwa ili mapato yaweze kupatikana ni vema stendi ikabaki moja, nayo ni ya Kilole, kwani ndani ya stendi hiyo kuna watu wamekodisha vibanda kwa ajili kukata tiketi, kuuza bidhaa na maduka. Lakini kuna uhakika wa kituo cha polisi, eneo la kupumzikia wasafiri na usalama wa abiria.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe (DED) Dkt. George Nyaronga alisema makusudio ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuongeza mapato ili kutoa huduma kwa wananchi. Lakini pia kwa kuruhusu stendi mbili, mapato ya halmashauri katika stendi hiyo na fedha zilizotumika kujenga stendi hiyo sh. bilioni 4.2 hazitaweza kupatikana.

Diwani wa Kata ya Majengo Mustapha Shengwatu alisema Serikali haifanyi biashara bali inatoa huduma, hivyo Serikali isilazimishe kuwakamua wananchi wake kutoa fedha nyingi kwenye kupata huduma ili kurudisha sh. bilioni 4.2 zilizojenga stendi hiyo, kwani hayo siyo malengo waliyokusudia, na ndiyo maana waliamua kuruhusu stendi mbili ili kuwapunguzia wananchi mzigo wa gharama.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.