Habari za Punde

Hutuba ya Mgeni Rasmin Ufunguzi wa Tamasha la 21 la Nchi za Jahazi Zanzibar Mhe. Issa Haji Gavu Ngome Kongwe Zanzibar.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Issa Haji Gavu, akizungumza na kutowa nasaha zake kwa Washiriki wa Tamasha la Nchi za Jahazi ZIFF wakati wa hafla ya kulizindua Tamasha hilo katika Viwanja vya Ngome Kongwe Forodhani Zanzibar.
Na Salum Vuai, WHUMK.
Tamasha la Kimataifa la Filamu Zanzibar (ZIFF) mwaka 2018, limefunguliwa juzi usiku huku Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikijipiga kifua kusaidia utatuzi wa changamoto zinazoikabili tasnia ya filamu nchini. 
Akizungumza kwenye ufunguzi wa tamasha hilo la 21 katika ukumbi wa Ngome Kongwe mjini Zanzibar, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi, alikiri kuwa pamoja na mafanikio yake, kuna maeneo ambayo halijafanya vizuri.
Alisema miongoni mwa upungufu huo, ni kutokufikiwa ufanisi wa asilimia 100 katika ulinzi wa haki za wabunifu na watengenezaji filamu, akisema iko haja ya kuuangalia upande huo kwa jicho la tatu ili wasanii hao wafaidi matunda ya jasho lao.
Aliiambia hadhira iliyofurika ukumbini hapo wakiwemo watalii kutoka nchi mbalimbali, kuwa Serikali ya Zanzibar ilianzisha kwa nia njema Ofisi ya Msimamizi wa Haki za Ubunifu (COSOZA), mfumo unaoendeshwa kimataifa ili kulinda haki za wasanii.
Alifahamisha kuwa tasnia ya filamu ni miongoni mwa maeneo yanayoweza kusaidia kuyapatia ufumbuzi matatizo ya kijamii hasa uhaba wa ajira, kama ilivyo katika mataifa mengine yaliyopiga hatua kubwa kifilamu na matamasha yanayotambulika kimataifa.
“Kwa upande wa serikali, naamini taasisi na vyombo husika vitaendelea kusimamia upatikanaji wa haki kwa waliopoteza jasho lao katika tasnia hii ili nao wanufaike kwa malengo waliyojiwekea,” alisema.
Waziri huyo alisema kuanzishwa kwa COSOZA ni sehemu ya msukumo wa serikali katika kutoa mchango ili kuwainua kimaisha wananchi waliojikita katika tasnia ya filamu.
“Na katika hili lazima tukiri liko eneo ambalo hatujafanya vizuri sana. Suala la uzalishaji wa filamu ni muhimu, lakini suala la miundombinu, ugawaji wake, upatikanaji wake, usimamizi, uuzaji na mgawanyiko wake bado hatujafanya vyema,” alisema Waziri huyo.

Kwa hivyo alitaka serikali ijitoe katika kuhakikisha inasimamia vyema haki za wabunifu wa filamu, kwani inaonekana bado wasambazaji wananufaika zaidi kuliko wazalishaji wake.
Hata hivyo, alieleza kufurahishwa kwake, kuwa pamoja na changamoto hizo na uhaba wa udhamini, tamasha la ZIFF limeendelea kuishi na kujiongozea umaarufu, hali inayowavutia watalii wengi wanaokuja nchini wakati wa tamasha hilo.
Mapema, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ZIFF Mahmoud Thabit Kombo, aliwashukuru wadhamini mbalimbali wanaoendelea kulibeba tamasha hilo, pamoja na wajumbe wa bodi kwa mshikamano wao kuhakakisha haliyumbi.
Alisema bila kuungwa mkono na wadhamini, Zanzibar inaweza kupoteza matamasha kama hayo na hivyo kupunguza nafasi za ajira na pato la taifa.
Akizungumzia ukuaji wa tasnia ya filamu Zanzibar, Kombo ambaye pia ni Waziri wa Habari, Utalii na Mambao ya Kale, alisema wakati umefika Zanzibar iwe na tamasha kubwa kwa jina la Zollywood, akifananisha na Hollywood (USA), Bollywood (India) na Nollywood (Nigeria).
Uzinduzi wa tamasha hilo ulipambwa na filamu ya Kiswahili iitwayo ‘Bahasha’, iliyoongozwa na Jordan Riber, ambapo miongoni mwa washiriki wake ni Ayoub Bombwe, Godliver Gordian, Omary Mrisho na Catherine Crede.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.