Habari za Punde

MPINA AUNDA KANDA MPYA YA ULINZI NA USIMAMIZI WA RASILIMALI ZA UVUVI ZIWA VICTORIA


  Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina mwenye koti jeupe kushoto kwake ni Mahamoud Mgimwa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo,Mifugo na Maji kulia ni Katibu Mkuu Uvuvi Rashid Tamatama na Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi Magesa Bulayi.wakiwa kpicha ya pamoja na Maofisa walioteuliwa kusimamia rasilimali za uvuvi katika kanda maalum kwenye ziwa victoria. 
Na.John Mapepele - Dodoma.
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameunda Kanda mpya ya Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Ziwa Victoria  na kuteua maafisa wapya wataokuwa na jukumu la kudhibiti na kutokomeza uvuvi haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi katika Ziwa Victoria ifikapo Desemba 2018.

Akizungumza jijini Dodoma mwishoni mwa wiki, Waziri Mpina amemteua Didas Mtambalike kuwa Mkuu mpya wa Kanda mpya ya Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Ziwa Victoria  huku akiunda kanda mbili za kiulinzi za Sengerema na Ukerewe .

Pia Serikali imeanzisha Kituo cha Ukaguzi wa Mazao ya Uvuvi mkoani Singida na kuweka vizuizi katika maeneo yote yaliyoripotiwa kuwepo matukio ya utoroshaji wa rasilimali za uvuvi hapa nchini.

Maafisa wengine walioteuliwa na Waziri Mpina kuongoza kanda zingine ni pamoja na  West Mbembati ambaye ataongoza Kanda ya Kagera, Vicenti Masui Munda Kanda ya Mwanza, Jairos Mahenge Kanda ya Mkoa wa Mara.

Wengine ni Judith Mgaya atakayeongoza Kanda ya Kiulinzi Ukerewe na Roman Mkenda Kanda ya Mkoa wa Geita,  Wencleslaus Luhasile aliyekuwa Afisa Uvuvi wa Wilaya ya Magu sasa ataongoza Kanda ya Kiulinzi ya Sengerema na Samson Mboje kutoka Kituo cha Usimamizi na Ulinzi wa Rasilimali Kanda ya Mwanza, sasa ameteuliwa kuongoza Kanda ya Simiyu/Magu.

Aidha Waziri Mpina alisisitiza kuwa katika operesheni inayoendelea Serikali inaandaa utaratibu wa kwenda na mahakama inayotembea ili watuhumiwa na wahalifu  wahukumiwe pale pale wakiwa na mashahidi wao.

Kuhusu maendeleo ya wavuvi wadogo, Waziri Mpina amesema Wizara yake kwa kushirikiana na Benki ya NMB inawafuatilia wavuvi na kuwafungulia  akaunti ambapo hadi sasa zaidi ya wavuvi 20,000 wamefikiwa.

Amesema utafiti umebaini kuwa asilimia  98 ya wavuvi ni vibarua wa matajiri ambapo mapato  yanayotokana na uvuvi kila wanapotoka kuvua hugawanywa nusu na tajiri wao ambaye ndiye mmliki wa chombo na nusu iliyobaki  kugawana  kila mvuvi aliyekuwa katika chombo hicho hali iliyowafanya wavuvi kote nchini kuendelea kuwa masikini na kuwanufaisha matajiri wachache.

Vile vile, Waziri Mpina amesema kuwa Operesheni Sangara awamu ya tatu itaendelea na kwa maji baridi yote ikiwemo Ziwa Tanganyika, Nyasa, Rukwa, Nyumba ya Mungu na Mtera na mito ili kuhakikisha rasilimali hiyo inalindwa na kunufaisha taifa.

Mbali na hatua hiyo Waziri Mpina ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) kufanya utafiti ili kujua kiasi cha samaki waliopo katika Ziwa Victoria  baada ya kuendesha Operesheni Sangara kwa  miezi sita sasa.

Kuhusu viongozi waadilifu na wanaosimamia kikamilifu ulinzi wa rasilimali uvuvi Waziri Mpina amesema Wizara yake itaendelea kuwatambua na kuwapongeza wananchi na viongozi wanaofanya vizuri kwenye usimamizi wa raslimali za uvuvi nchini.

Alisema katika kipindi hiki Wizara yake inatambua mchango wa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Kipole na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Mkoa wa Mara, Dkt. Vicenty Anney pamoja  na Afisa Mtendaji wa Kata ya  Kagya Wilaya ya Bukoba, Beatrice Lugemalila.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo na Maji, Dk. Christine Ishengoma alisema  mawaziri waliopita katika wizara hiyo walifanya kazi nzuri lakini ubunifu wa kipekee uliofanywa na Waziri Mpina umeiwezesha sekta ya uvuvi kuongeza mapato kutoka sh bilioni 18.5 katika mwaka wa fedha 2016/2017 hadi kufikia sh bilioni 26.3 mwaka wa fedha 2017/2018 fedha ambazo zitasaidia uboreshaji wa huduma za kijamii katika maeneo yote nchini.

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji, Katani Ahmad Katani alipongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya kulinda rasilamili za Taifa na kutaka juhudi hizo kuwa endelevu kwani pamoja na kuwa na eneo kubwa la maji bado uvuvi haujaweza kunufaisha Taifa.

Katani ambaye pia ni Mbunge wa Tandahimba mkoani Mtwara aliishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kufungua maduka yake ya zana za uvuvi ili kuwarahishia wavuvi kupata zana hizo kwa wakati na zenye ubora unaotakiwa kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Uvuvi-Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Rashid Tamatama alisema suala la ulinzi wa rasilimali za uvuvi litakuwa ni moja ya majukumu ya kila siku ya watumishi wa wizara hiyo ili kuhakikisha Taifa linanufaika vya kutosha na rasilimali hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.