Habari za Punde

SMZ Imefutia Waraka wa Umiliki Heka Tatu Borafia Silima Juma Kwa Kukiuka Masharti ya Mkataba..

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif akitoa Tamko la kufutwa  kwa umiliki wa Matumizi ya Eka Tatu kwa Bwana Borafia Silima Juma aliyekiuka Mkataba wa Matumizi ya Eka hizo.kwa matumizi ya Kilimo kulia Mkuu wa Wiaya ya Kaskazini B Unguja. Ndg.Rajab Ali Rajab, wakiwa katika eneo la heka hiyo wakati wa ziara ya Balozi Seif.
Baadhi ya Minazi 30 iliyokatwa ndani ya Eka Tatu zilizopo katika Kijiji cha Matetema Mkoa Kaskazin  Unguja  ambapo Mmiliki wa Eka hizo kwa ajili ya kuendeleza Kilimo  ameamua kupima Viwanja na kuuza kwa ajili ya ujenzi wa Nyumba za Kudumu.

Na.Othman Khamis.OMPR. 
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imemfutia Waraka Bwana Borafia Silima Juma kuanzia leo wa umiliki wa Matumizi ya Eka Tatu alizopewa na Serikali kwa ajili ya kuendeleza shughuli za Kilimo katika Kijiji cha Matetema Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Hatua hiyo ya Serikali Kuu inaunga mkono  maamuzi yaliyochukuliwa na Uongozi wa Serikali ya Wilaya ya Kaskazini “B”  ya kumzuia Mmiliki huyo kuendelea na matumizi ya Eka hizo baada ya kubaini amekiuka masharti ya Mkataba wa matumizi ya Eka alizopewa na Serikali.     
Uamuzi huo wa kufuta Waraka huo umekuja baada ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kufanya ziara fupi ya kukagua uharibifu mkubwa uliofanyika wa Eka hiyo kwa kukatwa Minazi, Miembe na Mti wa Mzambarau  na kuridhika na hatua iliyochukuliwa na Serikali ya Wilaya ya Kaskazini “B”.
Balozi Seif  alisema kwa sasa Serikali Kuu itasubiri mapendekezo yatakayoainishwa na Serikali ya Wilaya ya Kaskazini B ya namna itakavyopaswa kuchukuliwa juu ya matumizi ya Eka hizo kwa hatua za hapo baadae.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema maamuzi yaliyochukuliwa na Serikali ya Wilaya ni sahihi kwa vile baadhi ya Watu katika Jamii tayari wanaonekana kupuuza sheria zilizowekwa na Serikali kwa makusudi jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa hapo baadae.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Sera na Ilani ya Chama cha Afro Shirazy Party {ASP} iliamua kugawa ardhi eka tatu tatu iliyokuwa ikimilikiwa na mabwannyenye mara baada ya Mapinduzi ya Mwaka 1964 ili kuwapa fursa Wananchi kuendeleza kilimo kwa lengo la kuhuisha Maisha ya Familia zao.
Balozi Seif alitahadharisha wazi kwamba Ulimwengu  hivi sasa umebadilika sana kutokana na baadhi ya Watu kufanya hujuma za uchafuzi wa makusudi wa mazingira unaopelekea hata kina cha maji kupungua na kuleta majanga kwa viumbe vilivyomo ndani ya Dunia hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa agizo kwa Uongozi wa Serikali zote za Wilaya Unguja na Pemba kuendelee kufanya uhakiki wa Eka Tatu Tatu walizopewa Wananchi kwa shughuli za Kilimo na kuchukuwa hatua zinazofaa dhidi ya Watu watakapobainika wamevunja Sheria na Taratibu zilizowekwa za matumizi ya Eka hizo.
Balozi Seif alionya kwamba Mtu ye yote atakayebainika kwenda kinyume na Mkataba aliyopewa wa umiliki wa matumizi ya ardhi kwa Kilimo Serikali haitasita kumchukuliwa hatua za Kisheria ikiwemo kumnyang’anya Ardhi hiyo mara moja na kupewa yule atakayekubali kufuata muongozo na misingi sahihi ya matumizi hayo.
Mapema Mkuu wa Wilaya ya  Kaskazini “B” Nd. Rajab  Ali Rajab alisema Serikali ya Wilaya hiyo tayari imeshachukuwa hatua  zinazostahiki za kuiandikia barua Wizara inayohusika na usimamizi wa Ardhi kwa lengo la kumnyang’anya Mmiliki huyo.
Nd. Rajab alisema uamuzi huo umekuja baada ya Uongozi huo kujionea uharibifu wa mazingira uliofanywa na Mmiliki huyo aliyeamua kukata Minazi 30, Miembe Minne na Mzambarau Mmoja na kupima viwanja ambavyo baadhi yake ameshaviuza kwa ajili ya ujenzi wa Majengo ya kudumu.
Alisema yapo makosa mengi yaliyofanywa na Mmiliki huyo ikiwemo kukata Miti bila ya Kibali cha Taasisi inayohusika, kutumiwa misumeno wa Moto   iliyopigwa marufuku na Serikali pamoja na ukataji wa Viwanja kwenye Eka zilizotolewa na Serikali kwa kuendeleza Kilimo.
Alifahamisha kwamba hakuna kumbu kumbu zozote zinazoonyesha  uwepo wa maombi ya ujenzi kwa Watu waliouziwa Viwanja kwenye Eka hiyo ambazo zimeripotiwa ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kaszkazini “B” kitendo ambacho pia ni kosa kisheria.
Eka Tatu zilizopo katika Kijiji cha Matetema chini ya umiliki wa awali wa Matumizi ya Kilimo wa Bibi Mtumwa Omar ambae kwa sasa ni Marehemu ulitoa nafasi ya kuombwa upya naa mmiliki wa sasa baada ya Watoto wa Marehemu kutoandika Barua ya Maombi ya kuendelea kumiliki Eka hizo kwa mujibu wa Sheria zilizopo.

1 comment:

  1. Kuna wakati Rais wa Zanzibar wa awamu ya tano Dk. Salmin Amour Juma katika kusisitiza umuhimu wa sheria alikua akilirudia neno hilo mara tatu ili watu walielewe. Niwapongeze viongozi kwa hatua walizochukua ila niwaombe kuendelea na kazi ya kytoa elimu kwa umma juu ya matumizi sahihi ya ardhi zilizotolewa kwa matumizi maalum.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.