Habari za Punde

Zanzibar 24 watoa msaada wa chakula kwa Detroit Sober House Mchina mwanzo

 Mtendaji Mkuu wa Zanzibar 24 Suleiman Juma Is-haka akimkabidhi Mkuu wa Soba House ya Detroit Rashid Kassim msaada wa chakula katika hafla iliyofanyika katika nyumba hiyo iliyopo Kwamchina mwanzo.
 Baadhi ya vijana wanaoishi nyumba ya kurekebisha tabia ya Detroit iliopo kwa Mchina mwanzo wakifuatilia kukabidhiwa msaada wa chakula uliotolewa na Mtandao wa Kijamii wa Zanzibar 24.
 Mkuu wa Sober House ya Detroit  Rashid Kassim akitoa shukrani zake mbele ya waandishi wa habari wa Zanzibar 24 baada ya kupokea msaada wa chakula katika hafla iliyofanyika kwenye nyumba hiyo Kwamchina mwanzo.
Mmoja wa vijana wanaoishi nyumba ya kurekebisha tabia ya Detroit Alawi Abdalla akizungumza na waandishi wa habari  wa Zanzibar 24 Amina Omar (kulia) na Fat-hiya Shehe katika hafla iliyofanyika Kwamchina mwanzao.
Picha na Ramadhani Ali  Maelezo Zanzibar.

Na Ramadhani Ali – Maelezo 
Waathirika wa dawa za kulevya wanaoishi katika nyumba ya kurekebisha tabia (Soba House) ya Detroit iliyoko Kwamchina mwanzo wameiomba Serikali kuendeleza mapambano ya kupiga vita uingizaji na utumiaji wa dawa hizo nchini.
Vijana hao walitoa ombi hilo baada ya kupokea msaada wa chakula uliotolewa na Mtandao wa Kijamii Zanzibar 24 ikiwa ni miongoni mwa maadhimisho ya kutimia miaka mitatu tokea kuanzishwa mtandao huo.
Kijana Alawi Abdalla anaeishi nyumba hiyo alisema ikiwa Serikali haitaongeza nguvu za kuwatafuta na kuwakamata waingizaji wakubwa wa dawa za kulevya vijana wengi wataendelea kuathirika.
Aliwashauri vijana ambao bado hawajaanza kutumia dawa za kulevya wasijaribu kuzionja  kwani sio kitu cha kuonja na nihatari kwa usalama wa afya zao.
Alawi aliishauri Serikali kuwatafutia msaada wa nyenzo za kufanyia kazi vijana waliopita Soba House na kufanikiwa kurekebisha tabia zao ili watakapo rejea katika jamii waweze kujitegemea.
‘’Baadhi yetu tunaopita Soba House tunaporejea ndani ya jamii na kukosa kitu cha kufanya tunajikuta tunarejea kutumia dawa za kulevya, ni msiba mkubwa,’’ alilalamika Alawi.
Mtendaji Mkuu wa Zanzibar 24 Suleiman Juma Is-haka alisema katika kuadhimisha miaka mitatu tokea kuanzishwa mtandao huo wameamua kutoa  msaada wa chakula ili kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Serikali na Taasisi za kiraia kuwahudumia vijana wa Soba House.
Aliahidi kuwa Zanzibar 24 itaendelea kutoa msaada kwa jamii zinazoishi katika mazingira magumu kila uwezo utakapowaruhusu pamoja na uwezo mdogo walionao.
Mkuu wa Soba House ya Destroit Rashid Kassim aliwashukuru Zanzibar 24 kwa kuona umuhimu wa kuwasaidia chakula na kuzitaka Taasisi nyengine kujitokeza kusaidia kwasababu kazi ya kurekebisha tabia kwa waathirika wa dawa za kulevya sio jambo rahisi.
Alisema Soba House ya Destroit inakabiliwa na changamoto nyingi kwa vile vijana wanaoishi hapo wanatafautiana tabia na baadhi yao wanakabiliwa na matatizo ya akili.
Mtandao wa Zanzibar 24 ulikabidhi msaada wa mchele, unga wa ngano, unga wa sembe, sukari, mafuta ya kupikia, sabuni na dawa ya meno.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.