Habari za Punde

Maafisa Udhamini Taasisi za Umma watakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kujiamini

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akisikiliza michango na changamoto wanazopambana nazo Maafisa Wadhamini Kisiwani Pemba alipokutana nao kwenye Ukumbi wa Tasaf Chake chake Pemba.
Kushoto ya Balozi Seif ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma N’hunga, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Nd. Shaaban Seif Mohamed na kulia ya Balozi ni Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Mh. Hemed Suleiman Abdulla na wa Kaskazini Pemba Mh. Omar  Khamis Othman.
Baadhi ya Maafisa Wadhamini wa Wizara za Seriali Pemba wakifuatilia maagizo ya Balozi Seif hayupo pichani wakati alipofanya nao mazungumzo ya kubadilishana uzoefu wa kazi.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis, OMPR
Maafisa Wadhamini wa Taasisi za Umma Kisiwani Pemba wameagizwa kutekekeleza majukumu yao ya kazi kwa kujiamini katika misingi na taratibu za Sheria kwa lengo la kuwahudumia vyema Wananchi pamoja na Watendaji wa Taasisi za Umma Kisiwani humo.
Agizo hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  alipokuwa akizungumza na Waafisa Wadhamini hao katika Kikao cha kubadilishana uzoefu wa kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Jengo la Tasaf liliopo katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Chake Chake Pemba.
Balozi Seif alisema tatizo la Mwananchi au Mfanyakazi wa Umma Kisiwani Pemba lazima limalizike na kupata ufumbuzi chini ya usimamizi wa Afisa Mdhamini wa Wizara inayohusika badala ya kuliacha likawasilishwa Makao Makuu ya Wizara hiyo Unguja.
Alisema Viongozi Wakuu hawana miujiza ya kutanzua tatizo la mtendaji au Mwananchi ambalo linaweza kupata ufumbuzi ndani ya mamlaka ya Afisa Mdhamini aliyepewa jukumu la kusimamia changamoto na matatizo yanayowakabili wahusika hao.
Balozi Seif aliwaeleza Maafisa Wadhamini hao kuelewa kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliamua kuweka muongozo na Utaratibu wa uwepo wa Nafasi hiyo iliyokuwa ikihudumiwa na Manaibu Mawaziri wa Serikali katika Miaka ya nyuma ili kurahisisha upatikanaji wa huduma pamoja na kutanzua matatizo kwa haraka.
“ Maafisa Wadhamini Pemba wana dhamana kubwa ya kusimamia shughuli za Serikali kazi ambayo ilikuwa ikisimamiwa na Manaibu Mawaziri katika kila kitu Kisiwani Pemba”. Alisema Balozi Seif.
Alitahadharisha kuwa  Mwananchi au Mtumishi wa Umma anapoamua kwenda ngazi ya juu ya Uongozi kupelekea malalamiko yake ni kusema kwamba  Afisa Mdhamini anayepaswa kulishughulikia lalamiko la Mtu huyo maana yake ni kuwa ameshindwa kuwajibika ipasavyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza kwamba Mwananchi au Mtumishi wa Umma lazima asikilizwe changamoto zinazomkabili hasa masuala ya migogoro na ardhi na upatikanaji wa huduma za Afya na Maji ili zipatiwe ufumbuzi unaostahiki.
Balozi Seif alifafanua wazi kwamba ipo migogoro ya Wananchi inayoshindwa kupatiwa ufumbuzi wake Kisiwani Pemba na kupelekwa Makao Makuu Unguja lakini utanzuki wake wakati mwengine hurejea kule kule Kisiwani Pemba jambo ambalo ni kupoteza muda sambamba na kuwasumbua Wananchi.
Aliwahimiza Viongozi hao Wakuu wa Taasisi za Umma Kisiwani Pemba kuepuka tabia ya kubakia Maofisini kipindi kirefu na badala yake wafuatilie changamoto zinazowakabili Wananchi na Watendaji wa Umma katika maeneo yao ili ile imani ya wanaowatumikia irejee kama kawaida.
Balozi Seif alisema kwamba mfumo huo wa uwajibikaji utamfikisha mahala Afisa Mdhamini husika kujinasibu kwamba eneo analofanyia kazi Wananchi walio wengi hawalilalamikii kwa chochote kile.
Wakichangia mawazo kwenye Kikao hicho baadhi ya Maofisa Wadhamini wa Wizara za Serikali Kisiwani Pemba walieleza kwamba yapo mafanikio makubwa ya uwajibikaji yaliyofikiwa na Taasisi zao yanayotokana na ushirikiano mkubwa uliopo kati yao, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wafanyakazi wa Taasisi za Umma pamoja na Wananchi.
Hata hivyo Maafisa Wadhamini hao walisema zipo baadhi ya changamoto zinazowasumbua katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku zikiwemo pia nyengine walizozirithi kutoka kwa Maafisa Wadhamini waliowatangulia.
Afisa Mdhamini anayesimamia Ardhi na huduma za Maji Nd. Juma Bakari alisema ipo miongozo inayoelekeza matumizi sahihi ya Ardhi tokea Mwaka 1964 lakini baadhi ya Watu hujitokeza kulalamikia maeneo yao kwa hati zilizofutwa mara baada ya Mapinduzi jambo ambalo huleta matatizo katika utendaji wao.
Alisema matukio hayo mara nyingi hujitokeza pale yanapotokea mabadiliko ya Uongozi katika Taasisi za Umma ambapo baadhi ya walalamikaji hao huhisi kwamba wakati huo ndio muwafaka wa kupenyeza malalamiko yao yasiyostahiki kushughulikiwa kisheria.
Akizungumzia changamoto ya upatikanaji wa huduma za maji safi na salama Afisa Mdhamini huyo wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Nd. Juma alisema pampu 22 za kusukumia Maji zinazotoa huduma ndani ya Kisiwa cha Pemba zimeharibika kutokana na upelekaji huduma hiyo kwenda kwa Wananchi isiyo rafiki.
Nd. Juma alisema ukosefu wa matangi ya kuhifadhia Maji ambayo ujenzi wake huhitaji gharama kubwa ndio unaopelekea pampu hizo kutumika kwa muda mrefi bila ya mapumziko.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.