Habari za Punde

Vifungashio Vya Kisasa Vya Blista Vyarahishisha Kazi ya Ugawaji Dawa Kwa Wagonjwa.


Mganga Mfawidhi wa Zahanati  ya Kata ya Nyakabonga katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Fausta Rugalinda, akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu upatikanaji wa dawa katika zahanati hiyo pamoja na vifungashio vya dawa.

 Mkazi wa Kata ya Nyakabonga, Agnes Mganga, akiishukuru Serikali kwa kuwapelekea dawa katika zahanati hiyo.


Wananchi wa Kata ya Nyakabonga wakiwa wamesimama jirani ya kibao cha zahanati
 Ofisa Mauzo wa MSD Kanda ya Mwanza, Conoria Godfrey (kulia), akimuelekeza jambo Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo,Fausta Rugalinda wakati alipokuwa akikagua dawa zilizohifadhiwa kwenye stoo ya zahanati hiyo.

Na Dotto Mwaibale, Muleba
WATENDAJI wa Vituo vya kutolea huduma za afya wilayani Muleba mkoani Kagera wamesema vifungashio vya dawa za serikali viliboreshwa kutoka kwenye makopo kwenda kwenye Blister pack vina uhakika wa kubakiza dawa katika ubora unaohitajika pamoja na kurahisisha kugawa dawa kwa wagonjwa.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti mkoani Kagera, watendaji hao wamesema hata kwa upande wa watumiaji ambao ni wagonjwa vifungashio vya blister hata wakiangusha ama bahati mbaya zikamwagikiwa na maji hazitaathiriwa wala kupoteza ubora wake.

"Kupima dawa kwa kijiko kwa ajili ya kuziweka kwenye bahasha wakati wa kuwahudumia  wagonjwa kulituchukulia muda sana na mara nyingine unakuta kopo linakaa wazi hadi msururu mzima unaohitaji aina hiyo ya dawa uishe"

Kwa upande mwingine wananchi wa Kata ya Nyakabango wilayani Muleba mkoani Kagera wameipongeza serikali kwa kufanikisha kuwapelekea dawa kwa wakati kupitia Bohari ya Dawa (MSD).

Julius Kamuhaba alisema hivi sasa hali ya upatikanaji wa dawa katika zahanati hiyo ni nzuri na hakuna mtu atakayekwenda kupata matibabu akatoa malalamiko ya kukosa dawa.

"Naipongeza serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa jitihada inayoifanya ya kuhakikisha wananchi wake tunapatiwa dawa kwa wakati kupitia MSD" alisema Agnes Mganga mkazi wa kata hiyo.

Alisema kila anapokwenda kupata matibabu katika Zahanati ya Nyakabango amekuwa akipata dawa tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo walikuwa wakiandikiwa kwenda kuzinunua.

Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo, Fausta Rugalinda alisema kuwepo kwa mawasiliano mazuri na ushirikiano baina ya MSD na watendaji wa sekta ya afya wilayani humo ni moja ya sababu kubwa ya kupatikana kwa dawa kwa wakati katika vituo vya afya na zahanati.

"Tunaomba dawa kila baada ya miezi mitatu na dawa zinapokuwa zimepungua katika stoo yetu tunapopeleka maombi ya dharula wahusika wamekuwa  wakiwasiliana na dawa kuletewa kwa wakati na MSD" alisema Rugalinda.

Rugalinda aliongeza kuwa mara ya mwisho kupata dawa walizoomba MSD katika mwaka huu wa fedha 2017/2018 ilikuwa ni Julai 24 na kwamba maombi mengine wanatarajia kuyafanya mwezi ujao na kuwa bado wana dawa za kutosha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.