Habari za Punde

Kampuni ya ZTE Kuongeza Miradi Yake ya Mawasili Nchini Tanzania.


 Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Teknolojia ya Mawasiliano ya kisasa ya ZTE ya Nchini China Bwana Wang Yiwen Kushoto akimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi azma ya Kampuni yake  kuongeza miradi yake Nchini Tanzania kwa lengo la kuimarisha Sekta ya mawasiliano. Mazungumzo yao yaliyojumuisha pia Ujumbe wa Balozi Seif yalifanyika katika ukumbi Mdogo wa Majengo ya Maonyesho ya Kimataifa ya 15 ya Biashara ya China – Asean Expo 2018 Mjini Nanning Nchini Jamuhuri ya Watu wa China.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akiishauri Kampuni ya Kimataifa ya uzalishaji wa Umeme iitwayo Green Giant Energy Co. LTD yenye Makao Makuu yake Mjini Shanghai Nchini China alipofanya mazungumzo na wa Kampuni hiyo Bwana William Lee.
Picha na – OMPR – ZNZ. 

Na.Othman Khamis OMPR.
Uongozi wa Kampuni ya Kimataifa ya Mtandao wa Kisasa wa Mawasiliano ya ZTE yenye Makamo Makuu yake katika Mji wa Shengzhen Nchini Jamuhuri ya Watu wa China umepanga kuongeza miradi yake Nchini Tanzania kwa lengo la kuimarisha Sekta ya mawasiliano.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Kampuni hiyo Bwana Wang Yiwen wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyeuongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye Maonyesho ya Kimataifa ya 15 ya Biashara ya China – Asean Expo 2018 yaliyofanyika katika Nyumba ya Wageni Mashuhuri wa Kimataifa
kwenye Mji wa Nanning.

Bwana Wang Yiwen alisema uwamuzi wa Uongozi wa Kampuni yake kuongeza Miradi ya Uwekezaji Nchini Tanzania umekuja kutokana na mazingira bora ya uwekezaji pamoja na rasilmali za asili za maumbile zilizotoa kigezo  kikubwa kwa Kampuni hiyo.

Alisema hatua hiyo  pia inakwenda sambamba na utafiti wa Wataalamu wake waliobaini bado upo upungufu wa upatikanaji wa huduma sahihi za Mawasiliano ya Teknolojia yanayohitaji kuwafikia sio Watanzania pekee, bali  hata Watu wa Afrika ya Mashariki nzima yenye Wakaazi wasiopungua Milioni 196,000,000.

Bwana Wang Yiwen alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Dunia hivi sasa inazungumzia mfumo wa Mawasiliano ya Kisasa yanayoufanya Ulimwengu kuwa Kiganja badaya ya Kijiji masuala ambayo ndio Dira ya Kampuni hiyo katika kusimamia kazi za kufanikisha Teknolojia hiyo.

Makamu wa Rais huyo wa Kampuni ya ZTE alimuhakikishia Balozi  Seif  kwamba Taasisi yake itasaidia kuitangaza Tanzania katika Vivutio ilivyonavyo kama Mbuga za Wanyama na Fukwe za Kuvutia katika Mitandao yao ili Watalii wengi wa China wanaopendelea zaidi kutembelea Nchi za Afrika Kuisni na Mauritius wazuru pia Tanzania kujionea maumbile mazuri ya kuvutia.

Bwana Wang  alifahamisha kwamba Kampuni ya ZTE iliyoasisiwa mwaka 1985 na kuendelea kutoa huduma kwa takriban Miaka 14 sasa Barani Afrika tayari imeshawekeza miradi yake katika Mataifa 60 ulimwenguni na kupata tuzo tofauti katika ubora wa utoaji huduma zake katika kiwango kinachokubalika Kimataifa.

Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishukuru na kuipongeza Kampuni ya ZTE kwa kasi kubwa ya uwajibikaji wa watendaji wake  katika mfumo wa Teknolojia ya kisasa ya mawasiliano unaoonekana kukubalika na Mataifa mengi Duniani zikiwemo pia Nchi za Bara la Afrika.

Balozi Seif  alisema Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania sambamba na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinaendelea kuipa fursa zaidi Kampuni ya Teknolojia ya Mawasiliano ya Kisasa ya ZTE katika mtazamo wake wa miradi ya maendeleo inayoendelea kutekeleza kila siku.

Alimueleza Makamu wa Rais wa ZTE  kwamba hatua hiyo ya Serikali imekuja kutokana na Uongozi wa juu wa Kampuni hiyo kuonyesha juhudi kubwa za kuendelea kuunga mkono harakati za kuimarisha miradi ya Maendeleo zinazotekelezwa na Serikali zote mbili Nchini Tanzania.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya Kimataifa ya ZTE zimewahi kutiliana saini Mkataba wa ushirikiano katika uendelezaji wa miradi itakayotumia mfumo unaokubalika Kimataifa kwa hivi sasa wakati wa ziara ya Kiserikali ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  aliyoifanya Mwezi Novemba Mwaka 2016 Nchini China.

Mkataba huo uliolenga kwenye Miradi itakayotumia  mfumo waTeknolojia ya Kisasa { TEHAMA } ni pamoja na ule  wa Mawasiliano Serikalini { E Goverment } huduma za umeme, usafiri, miji mipya, afya pamoja na huduma za Kijamii ikiwemo utaratibu wa udhibiti wa ukusanyaji wa Mapato ya Serikalini.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifanya mazungumzo na Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya uzalishaji wa Umeme iitwayo Green Giant Energy co.LTD Bwana William Lee yanye Makao Makuu yake Mjini Shanghai Nchini China.
Katika mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi Mdogo wa Majengo ya Maonyesho ya Kimataifa ya 15 ya Biashara ya China – Asean Expo 2018 Balozi Seif aliushauri Uongozi wa Kampuni hiyo kuwekeza Miradi yake Nchini Tanzania kwa vile huduma wanazofanya bado
zinahitajika katika baadhi ya Sehemu hasa Vijijini.

Balozi Seif  alitolea mfano Visiwa vya Zanzibar hivi sasa vinavyotegemea mfumo mmoja tu wa huduma ya Umeme kitu ambacho si sahihi endapo itatokezea mabadiliko au kuharibika kwa mfumo uliopo wa usambazaji wa huduma hiyo.

Naye Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya uzalishaji wa Umeme iitwayo Green Giant Energy co.LTD Bwana William Lee alisema Kampuni yake inajaribu kuangalia uwezekano wa njia itakayowawezesha kuangalia mazingira ya Afrika ili waanzishe miradi yao ya Nishati. 

Bwana William Lee alisema njia hiyo itawapa uwezo zaidi wa kutanua wigo utakaowawezesha kujitangaza na kukubalika kwa Mataifa ya nje badala ya kutegemea China ambayo kwa kipindi hichi imeshajitosheleza vya kutosha kwa huduma hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.