Habari za Punde

Rais wa Liberia George Weah Akicheza Mechi ya Kirafiki Akiwa na Miaka 51.

Rais wa Liberia Mhe. George Weah alichezea Monaco, Paris St-Germain na AC Milan - akikaa muda mfupi Chelsea na Manchester City, akishiriki katika mchezo wa kirafiki wa Kimataifa. 

Rais wa Liberia George Weah alicheza mechi ya kirafiki ya kimataifa kwa nchi yake siku ya Jumanne akiwa na miaka 51.
Weah ambaye ni mchezaji wa kwanza wa soka kutoka Afrika kushinda tuzo la mchezaji bora wa Fifa, alicheza dakika 79 kwenye mechi ambapo walishindwa na Nigeria kwa mabao 2-1 nyumbani Monrovia.
Liberia ilipanga mechi hiyo ya kirafiki kupumzisha shati namba 14 ambalo lilitumiwa na Weah wakati wa kilele cha taaluma yake.
Mchezaji huyo wa zamani wa AC Milan, ambaye aliapishwa kuwa Rais mwezi Januari, alishangiliwa wakati akitolewa uwanjani wakati wa mabadiliko.
Nigeria ilikuwa na kikosi kikali akiwemo Wilfred Ndidi wa Leicester na mwenzake Peter Etebo wa Stoke City.
Etebo alipiga kona ambayo Simeon Nwankwo aliitumia kuiweka Nigeria kifua mbele kwa mabao 2-0 baada ya Henry Onyekuru ambaye yuko kwa mkopo huko Galatasaray kutoka Everton kufunga bao la kwanza. Liberia walifunga bao lao kwa njia ya penalti iliyopigwa na Kpah Sherman.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.