Habari za Punde

Tanzania Kukaribisha Wawekezaji wa Nje Kutumia Fursa Ziliopo.



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Sif Ali Iddi akiingia kwenye Ukumbi wa Mikutano ndani ya Viwanja vya Maonyesho ya Kimataifa ya 15 ya Biashara Mjini Nanning Guanxi Nchini China kuzungumza na Wawekezaji na Wafanyabishara wa Taifa hilo.
Balozi Seif akizungumza kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Wawekezaji na Wafanyabiashara ulioandaliwa na Tanzania kwa ajili ya kutangaza  fursa za vivutio ilivyonavyo ndani ya  Sekta ya Uwekezaji katika Maonyesho ya Biashara ya 15 ya Biashara yanayoendelea kwenye Mji wa Nanning Jimboni Guangxi Nchini China.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanda Tanzania { Tan Trade } Ndugu Edwin Rutageuka Akitoa Taarifa ya hali za Biashara Nchini Tanzania kwenye Mkutano wa Wawekezaji na Wafanyabiashara.
Meneja huduma na mawasiliano wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar { ZIPA } Bibi Nasria  Mohamed akielezea fursa za uwekezaji zinazopatikana Zanzibar mbele ya Wawekezaji na Wafanyabiashara wa China.
Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa Wawekezaji na Wafanyabiashara ulioandaliwa na Tanzania kwenye Maonyesho ya Biashara ya 15 ya Biashara yanayoendelea kwenye Mji wa Nanning Jimboni Guangxi Nchini China.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema sababu kubwa inayoifanya Tanzania kukaribisha wawekezaji wa nje kutumia fursa zilizopo inatokana na hali ya Utulivu na Amani  inayoambatana na uwepo wa vivutio vya Utalii kama fukwe pamoja na mbuga za Wanyama. 


Alisema Serikali zote mbili za Tanzania Bara na Zanzibar zimekuwa na Katiba zinazotekelezeka ambazo huzipa muongozo Sheria katika kuweka miongozo inayotoa fursa kwa Wawekezaji wa Kimataifa kutumia fursa za Uwekezaji zilizopo Nchini Tanzania.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Wawekezaji na Wafanyabiashara ulioandaliwa na Tanzania kwa ajili ya kutangaza  fursa za vivutio ilivyonavyo ndani ya  Sekta ya Uwekezaji katika Maonyesho ya Biashara ya 15 ya Biashara yanayoendelea kwenye Mji wa Nanning Jimboni Guangxi Nchini China.

Alisema harakati za kimaisha zinawapa muda wananchi, Wawekezaji, sambamba na wageni mbali mbali wanaopendelea kutembelea Tanzania Taifa liliopo Mashariki ya Bara la Afrika kufanya shughuli zao kama kawaida bila ya bughudha yoyote.

Balozi Seif alisema  Tanzania imelenga kuwa na Uchumi wa kati na kati ifikapo Mwaka 2025, na hii itaimarika na kupatikana iwapo hali ya amani itaendelea kuwepo kitu kinachozingatiwa na Serikali zote mbili kwa gharama yoyote ile.

Alieleza kwamba Serikali kupitia Taasisi zake inaendelea kujenga mazingira bora  ili kuwatengenezea njia Wawekezaji wenye nia ya kulitumia soko la Tanzania akiwahamasisha wale watokao China hata kama watakuwa na mawazo ya kuwekeza katika mfumo wa Ubia.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  aliwahakikishia Wawekezaji na Wafanyabiashara wa China kupewa ushirikiano wa karibu katika masuala ya Uwekezaji.

Aliushukuru na kuupongeza Ubalozi wa Tanaznia Nchini Jamuhuri ya Watu wa China Chini ya Kiongozi wao Balozi Mberwa Kairuki kwa jitihada na kazi nguvu walizochukuwa za kuhakikisha kwamba Mkutano huo wa wafanyabiashara unafanikiwa vyema.

Akitoa Taarifa ya hali za Biashara Nchini Tanzania Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanda Tanzania { Tan Trade } Ndugu Edwin Rutageuka aliwashauri  na kuwaomba Wafanyabiashara  na Wawekezaji Nchini china kushiriki Maonyesho ya Kimataifa ya Saba Saba yanayofanyika Kila Mwaka Dar es salaaam Tanzania.

Nd. Edwin alisema Maonyesho hayo licha ya kuwepo kwa Makampuni kadhaa ya China lakini bado wale ambaoi hawajawahi kushiriki wana fursa ya kujiandikisha kwa ajili ya kusherehekea kutimia kwa Miaka 43 ya Maonyesho hayo ambayo yameshapata umaarufu ndani ya Mataifa ya Nchi za Kusini na Mashariki ya Bara la Afrika.

Mapema Meneja huduma na mawasiliano wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar { ZIPA } Bibi Nasria  Mohamed alisema Taasisi hiyo imeundwa kwa lengo la kuwajengea mazingira mazuri Wawekezaji  na Makampuni ya Biashara ndani na nje ya Nchi.

Bibi Nasria  alisema  Miradi ya Uwekezaji inazidi kuimarika iliiliyolengwa kutoa huduma mbali mbali ili ikidhi mahitaji halisi ya soko la Afrika Mashariki hasa ikizingatiwa ongezeko la idadi kubwa ya Watu wake wanaokadiriwa kufikia Milioni 96,000,000.

Wakati wa Usiku Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi na Ujumbe wake alipata nafasi ya kutembelea eneo la Utamaduni wa Kiasia uliobeba Mataifa yote ya Jumuiya ya Asean.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.