Habari za Punde

Idara ya Makumbusho na mambo ya Kale yawaaga watumishi wake wanaostaafu

Wafanyakazi walioagwa baada ya kumaliza utumishi wao wa kazi katika Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale Zanzibar
Mkurugenzi  Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale Zanzibar Salum Kitwana Sururu akitoa shukurani zake kwa Wafanyakazi hao (hawapo pichani) na kuwatakia kheri katika maisha yao
 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar  anaeshughulikia masuala ya Habari  Dkt. Saleh Yussuf Mnemo akimkabidhi cheti maalum Bi. Jokha Ali Simba mmoja ya wafanyakazi waliostaafu Idara ya Makumbusho ya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Katibu Mkuu Chama cha Wafanyakazi Zanzibar (ZAPSU) Mwatumu Khamis Othman akimkabidhi saa ya ukutani mzee  Mussa Vuai Pakia  katika khafla ya kuwaaga wafanyakazi hao iliofanyika  ukumbi wa Palace Museum Forodhani Mjini Zanzibar.
 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utalii na Mambo ya Kale  anaeshughulikia masuala ya Habari Dkt. Saleh Yussuf Mnemo akizungumza katika khafla ya kuwaaga wafanyakazi hao iliofanyika  ukumbi wa Palace Museum Forodhani Mjini Zanzibar.
 Baadhi ya Wafanyakazi wa  Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale waliohudhuria katika ghafla ya kuwaaga wafanyakazi wenzao waliomaliza muda wa kufanya kazi katika Idara hiyo.
Picha na Abdalla Omar Habari  -  Maelezo Zanzibar.

Na Khadija Khamis  - Maelezo  Zanzibar   28/11/2018.

Naibu  Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utalii na Mambo ya Kale  anaeshughulikia  Habari  Dkt Saleh Yussuf Mnemo amewataka wafanyakazi wa Idara ya Makumbusho na mambo ya kale  kufuata nyayo za wafanyakazi wazoefu ili  kufanyakazi kwa bidii na uadilifu.

Alisema kufanya kazi kwa uadilifu kunaleta  uzoefu  pia kunasaidia kuibua mbinu kiutendaji pamoja na kujiamini  kutekeleza vyema majukumu ili kuweza kupata taaluma zaidi.

Hayo aliyasema huko katiKa Ukumbi wa Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale ( Palace Museum ) Forodhani wakati akiwatunuku vyeti na zawadi wafanyakazi wanne waliostaafu wa  Idara hiyo .

Aidha alisema Serikali itaendelea kuzithamini taaluma zao na kuzidi kuendelea kuzitumia kwa muda wote ili  kuhakikisha kuwa  wafanyakazi watazidisha kuufanyia kazi uzoefu huo .

“Wafanyakazi ambao tupo iko haja kuufanyia kazi uzoefu huo wa taaluma na kuiga mfano kutoka kwao pia kuzingatia  heshima na maadili ya kazi, na  tunatakiwa tusiusahau ujuzi waliotupa katika taasisi zetu.”Alisema Naibu Katibu Mkuu .

Alifahamisha kuwa wastaafu hao walikuwa na kazi kubwa ambayo  waliweza kukabiliana nazo pamoja  na changamoto ambazo ni nzuri na sio nzuri  hadi leo wanamaliza muda wao wa utumishi Serikalini..

Aidha Dkt. Mnemo alieleza kuwa Serikali hautausahau mchango wao kutokana na juhudi kubwa waliyoifanya wakati wa utumishi katika kuleta maendeleo ya  Taifa.

Nae Mkurugenzi wa Idara ya Makumbusho na Mambo ya 
Kale  Salum Kitwana Sururu alisema uzoefu, uaminifu na uchapakazi ndio hazina waliyoiacha wastaafu hao ni vyema kuziheshimu na kuzitekeleza .

“Hakuna kitu kibaya na chenye majonzi ya kuwa watu wamekaa pamoja kwa muda mrefu  kutengana  ni majonzi makubwa ila  faraja kwa kumaliza muda wao wakazi wakiwa wazima kiafya”Alisema Mkurugenzi huyo.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Umma ( ZAPSU) Mwatum Khamis Othman aliwataka  wafanyakazi kujiunga katika vyama vya wafanyakazi kwani vimekuwa vinasaidia  kutetea haki zao wakati wanapopata matatizo.

Nae mmoja wa wastaafu hao Jokha Ali Simba amewaomba wafanyakazi wa Idara ya Makumbusho kufanya kazi kwa uadilifu kupendana, kuweka heshima kwa viongozi  wao pamoja na kuwa waadili katika utendaji  wa kazi.


Pia alisisitiza kuwa wafanyakazi ambao wamemaliza kutumikia muda wao wa kazi kupatia haki zao mapema ili watekeleze malengo ambayo wamejiwekea na wasiwasubiri hadi kufariki kwa kurithiwa na wengine .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.