Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Ujumbe wa Madaktari kutoka Nchini Norway wa Chuo Kikuu cha "Houkeland University Hospital " ukiongozwa na Katibu Mtendaji Mr. Eivind Hamsen,kushoto wa kwanza.
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein amesema misaada
mbali mbali iliyotolewa na Chuo Kikuu ‘Houkeland University Hospital’,
imekwenda sambamba na dhamira ya muda
mrefu ya Serikali ya kutoa huduma bora za tiba ya akili kwa wananchi wake.
Dk. Shein amesema
hayo leo Ikulu mjini Zanzibar, alipozungumza na ujumbe wa Madaktari wanne
kutoka chuo kikuu cha ‘Houkeland University Hospital’ cha nchini Norway,
ukiongozwa na Katibu Mtendaji Eivind Hamsen.
Alisema kwa
nyakati tofauti Serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo imekuwa
ikifanya kila juhudi kuhakikisha inaimarisha upatikanaji wa huduma za tiba ya
akili katika Hospitali yake iliopo Kidongochekundu mjini hapa na kuondokana na
dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii kuwa eneo hilo ni ‘jela’ ya wagonjwa hao.
“Serikali imekuwa
ikifanya kila juhudi kuimarisha Hospita hiyo, ili ionekane ni kituo cha tiba ya
akili, sio tena jela ya wendawazimu kama ilivyokuwa ikitambulika mara baada ya
kuanzishwa kwake”, alisema.
Alisema juhudi
hizo ziliambatana na uanzishaji wa sera mpya
na sheria za uendeshaji wa hospitali hiyo, zikilenga kuleta mageuzi
makubwa katika suala la upatikanaji wa huduma bora kwa wagonjwa.
Alisema tayari
kuna mafanikio makubwa yaliofikiwa, katika upatikanaji wa huduma za tiba ya
akili, huku mkazo ukielekezwa kukiimarisha zaidi.
Katika hatua
nyengine Dk. Shein alisema Zanzibar
imepata mafanikio makubwa katika sekta ya Afya, kwa kuiimarisha Hospitali kuu
ya Mnazi mmoja, Hospitali za Wilaya pamoja na vituo vya Afya Unguja na Pemba,
kwa kuvipatia vifaa vya kisasa na mafunzo kwa madaktari wake.
“ Kwa kushirikiana
na washirika wa maendeleo tumeimarisha Hospitali kuu ya Mnazi mmoja na zile
zilioko Wilayani, huduma mbali mbali zinapatikana kwa urahisi na bila ya malipo
yoyote; kama vile MRI, watu wamekuwa
wakitoka nje ya Zanzibar kufuta matibabu hapa”, alisema.
Nae, Kiongozi wa
ujumbe huo kutoka ‘Houkeland University Hospital’ COE Elvind Hamsen, alisema
wameridhishwa na juhudi kubwa zilizochukuliwa na Serikali katika kuiendeleza
Hospitali hiyo, sambamba na huduma bora zinazotolewa na wafanyakazi wake.
Alisema Chuo
hicho kitaendeleza ushirikiano uliopo ili kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa
maslahi ya jamii ya Wazanzibari.
“Hatuhesabu
kiwango gani cha fedha zimetumika, bali tunazingatia vipi upatikanaji wa huduma
zitakavyoimarika”, alisema Hamsen.
Aidha, kiongozi
huyo alimhakikishia Rais wa Zanzibar kuwa Chuo hicho kitasaidia uanzishaji wa
Hospital kuu ya kisasa, inayotarajiwa kujengwa katika eneo la Binguni, Mkoa
Kusini Unguja.
Chuo kikuu cha
Houkeland University Hospital, kimekuwa na mradi wa kuisaidia Hospital ya
Wagonjwa wa Akili, Kidongochekundu kupitia Nyanja mbali mbali ikiwemo kuboresha
kitengo cha Pathology,ecology pamoja na
kutoa mafunzo mbali mbali kwa watendaji katika masuala ya tiba ya akili.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822
E-mail: abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment