Dk. Shein aliyasema hayo
leo wakati alipokutana na uongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioongozwa na Waziri wa Wizara hiyo Kangi
Alphaxard Lugola uliofika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha kwa
Rais ambapo viongozi wengine waliofutana na Waziri Lugola ni Meja Jenerali
Jacob Gideon Kingu, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara
Kailima Ramadhan.
Katika maelezo yake Rais
Dk. Shein aliueleza uongozi huo kuwa Zanzibar iko salama hali ambayo imeweza
kuwapelekea wananchi wake waendelee kuishi kwa amani na utulivu mkubwa.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa hatua hiyo inatokana na juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na vikosi
vyote vya Idara zilizomo katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi likiwemo Jeshi
la Polisi, Uhamiaji pamoja na Idara ya Vitambulisho vya Taifa.
Alieleza kuwa kupungua
kwa vitendo vya uhalifu kwa asilimi 34 pamoja na makosa madogo kwa asilimi 57
kwa kipindi cha Januatri hadi Oktoba mwaka huu, kumeonesha wazi kuwa mafanikio
makubwa yanaendelea kupatikana katika kudumisha amani, utulivu na usalama hapa
Zanzibar.
Aidha, Rais Dk. Shein
alisema kuwa kazi imefanywa vizuri sana hadi kufikia hatua hiyo ya mafanikio na
kueleza imani yake kubwa aliyonayo kutokana na uongozi wa Wizara hiyo ambao
umeanza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Alieleza kuwa viongozi hao
wameingia na rekodi nzuri hatua ambayo imepelekea kuendelea kuimarika kwa hali
ya utulivu amani na usalama kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo
Zanzibar.
Rais Dk. Shein
alisisitiza haja kwa uongozi wa Wizara hiyo kuzitumia vyema Idara zake katika
kutekeleza majukumu yao kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ili malengo ya waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaweze kufikiwa.
Dk. Shein aliueleza uongozi
huo juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilizozichukua katika
kuhakikisha vitendo vyote vinavyohatarisha amani na usalama vinadhibitiwa
ipasavyo kwa kuandaa mikakati maalum ili wananchi na mali zao pamoja na wageni
wanaoitembelea Zanzibar wakiwemo watalii wanakuwa salama kwa kuweka vifaa
maalum vya kisasa vya ulinzi.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba sifa njema ya Zanzibar kuwa ni
sehemu salama yenye utulivu inabakia na inakuwa ya kudumu na inaendelea kuwa ni
kichocheo cha kuongeza kasi ya maendeleo ya nchi katika nyanja zote ikiwemo
sekta ya utalii.
Alieleza kuwa Serikali
imeamua kuweka vifaa hivyo kwa lengo la kuimarisha usalama katika mji wa
Zanzibar kwani vinauwezo mkubwa wa kuwabaini wahusika wa matukio mbali mbali
kwa haraka na ufanisi mkubwa pamoja na kuyabaini matukio ya magendo ya bidhaa
kadhaa kwa kuwepo ulinzi katika maeneo ya baharini na angani kupitia vifaa
hivyo maalum vya kisasa.
Mapema Waziri wa Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi Kangi Alphaxard Lugola alimueleza Rais Dk. Shein
mikakati maalum iliyowekwa na Wizara yake katika kuhakikisha ulinzi, amani na
usalama inakuwa ya kudumu hapa Zanzibar.
Waziri Lugola alimueleza
Dk. Shein kuwa kwa kipindi cha muda wa kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu
matukio ya uhalifu hapa Zanzibar yamepungua kwa asilimia 34 na makosa madogo
yamepungua kwa asilimia 57 ukiwemo ukiwemo udhibiti wa dawa za kulevya.
Waziri Lugola alitoa
shukurani kwa Dk. Shein kwa kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanaendelea kuishi
kwa amani, utulimu na usalama mkubwa na kumuhakikishia kuwa vikosi vyake vya ulinzi
vinasimama imara ili dira ya Zanzibar ya kudumisha amani inafikiwa.
Aidha, Waziri Lugola
alieleza kuwa bado changamoto ya magendo wanaendelea kupambana nayo kwani
anatambua kuwa magendo yanahujumu mapato na uchumi wa Serikali.
Alisema kuwa Idara zilizomi
katika Wizara hiyo ambazo ni za Muungano zimekuwa zikifanya juhudi kubwa katika
kutekeleza majukumu yake likiwemo Jeshi la Polisi, Uhamiaji na Mamlaka ya Vitambulisho
vya Taifa (NIDA).
Waziri huyo alieleza
kuwa Idara ya Uhamiaji imekwua ikifanya kazi kubwa ya kuwadhibiti wageni
wanaoingia nchini na wanaotoka ili waingie na kutoka kihalali pamoja na kutumia
pasi za kusafiria kwa njia ya elektroniki, visa na vibali vya kazi.
Aliongeza kuwa Mamlaka
ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ina kazi kubwa ikwia ni pamoja na kuwatambua
wananchi, kuwasajili sambamba na kuwatambua wageni wanaokaa kihalali sambamba
na kwuapatia wakimbizi vitambulisho kwa wale waliotimia kuanzia umri wa mika
18. Alieleza kuwa tayari hadi Oktoba mwaka huu Mamlaka hiyo imeshasajili wananchi
wapatao 652,000 na asilimia 90 wameshapatiwa vitambulisho vyao vya Taifa hapa
Zanzibar.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment