Habari za Punde

Mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wanawake katika kunufaika na fursa zilizopo katika sekta ya utalii






Na. Is-haka Omar -,Zanzibar.
MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud amesema muelekeo wa Zanzibar kwa sasa ni kwenda katika uchumi wa Utalii.

Kauli hiyo ameitoa wakati akifunga mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wanawake katika kunufaika na fursa zilizopo katika sekta ya utalii zikiwemo kuongoza Watalii, yamefanyika Hoteli ya Zanzibar Paradase International iliyopo Amani Wilaya ya Mjini Unguja.

RC Ayoub amesema licha ya uwepo rasilimali mbali mbali zenye uwezo wa kukuza uchumi wa nchi ambazo ni Mafuta na Gesi Asili, uchumi endelevu wa bahari lakini kwa mazingira ya Zanzibar uchumi wa utalii ndio pekee utakaoweza kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Amesema takwimu za mwisho zinaonyesha kuwa sekta ya utalii inachingia pato la taifa kwa asilimia 27 pamoja na kuchangia fedha za kigeni kwa asilimia 80, kiwango ambacho RC Ayoub amekitaja kuwa ni kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

"Zamani zao la Karafuu ndio lililokuwa likichangia kwa asilimia kubwa pato la taifa lakini kwa sasa Utalii ndio unaoongoza lakini pia hata hizi rasilimali nyingine hatutakiwi kuziacha kwani nazo zinachangia kwa njia mbali mbali ukuaji wa uchumi wetu.", amesema Mhe. Ayoub.

Ameongeza kuwa idadi ya ajira 25,000 zimeongezeka kwa vijana kupitia uchumi wa utalii na zipo ajira ambazo bado hazijaratibiwa zinaenmdelea kuongezeka kila mwaka.

Amesema lengo la serikali katika ukuaji wa utalii kama ilivyotajwa katika  Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 inayokwenda sambamba na mpango wa Taifa wa kukuza uchumi Zanzibar MKUZA awamu ya tatu dhamira serikali ni kufikia idadi ya watalii 500,000 ifikapo mwaka 2020  ambapo kwa mujibu wa takwimu za kamisheni ya utalii kwa sasa wapo zaidi ya watalii 400,000 hivyo kabla ya 2020 malengo yakafikiwa kwa ufanisi.

Ameeleza kuwa kwa kasi hiyo ya ongezeko la watalii nchini pia itatoa fursa ya kuongeza kwa ajira zikiwemo huduma za kusambaza vyakula, kuongoza watalii, soko la bidhaa za ndani pamoja na fursa mbali mbali za kijamii.

Amesema Serikali imeimarisha ulinzi kupitia kikosi maalum cha ulinzi wa uwekezaji kupitia JKU lakini mbali na hilo tayari kuna ulinzi wa kielectironiki kupitia camera za kisasa, ikiwa ni kuwaweka tayari wananchi na kuhakikisha uchumi wa utalii unabaki salama wakati wote.

Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wanawake ili wajikwamue kiuchumi huku akitolea mfano kwamba kwa upande wa Tanzania bara zimetengwa asilimia 10 za pato la ndani za kuwawezesha vijana na wanawake, na kwa Zanzibar nayo imepiga hatua ya kuanza kwa asilimia mbili ya fedha za makusanyo ya ndani ya Manispaa ya Mjini  inatoa kwa vijana wa kiume na wa kike.

Amewasisitiza washiriki wa Mafunzo hayo kuyatumia kwa vitendo na kuhakikisha wanaongeza idadi ya watembeza watalii wanawake na kufikia kiwango kinachoridhisha ambapo kwa sasa Zanzibar nzima yupo mwanamke mmoja anayefanya kazi hiyo.

Ametoa Wito kwa Jumuiya ya Watembeza Watalii Zanzibar(ZATOGA) kuhakikisha kila kampuni ya watembeza watalii inakuwa na mwanamke mmoja wa kutembeza watalii kwani tayari wamehitimu mafunzo hayo na wana uwezo wa kufanya kazi.

Ameipongeza NVCT kwa juhudi zao za kubuni mafunzo yaliyokuwepo katika soko la ajira nchini yenye lengo la kuinua uwezo wa wanawake nchini katika kuchangamkia fursa katika sekta ya utalii.

Awali akizungumza Mkurugenzi wa NVCT Pili Khamis amesema washiriki wa mafunzo hayo walikuwa na hamasa ya kujifunza kwa bidii sambamba na kudadisi masuala mbali mbali yaliyotolewa ufafanuzi wa kitaalamu na wakufunzi.

Akizungumza Meneja Masoko wa NVCT Abdulkarim Ali Abdulla, amefafanua kwamba mafunzo hayo yamefungua milango ya fursa kwa wanawake kuajiriwa na kujiajiri wenyewe.

" Wazazi na walezi wengi bado wana fikra za kuwa mwanamke akimaliza shule kinachofuata ni kuolewa, huku wakisahau kuwa kuna jambo jingine muhimu la mwanamke kuwa na kazi halali ya kujipatia kipato.", ameeleza Abdulkarimu.

Ameleza kuwa baada ya mafunzo hayo NVCT itaendelea kufuatilia kwa kina washiriki wote waliopewa mafunzo hayo kwa lengo la kujua ni washiriki wangapi wameyafanyia kazi kwa vitendo na watakaokuwa wameshindwa wajengewe uwezo.

Akizungumza mshiriki wa mafunzo Zawadi Pandu Haji,amesema taaluma waliyopewa ameipokea vizuri kwani itamwezesha kujiajiri mwenyewe.

Naye mshiriki Ishra Seif, amesema ni wakati mwafaka wa wanawake kuacha utegemezi na kubagua ajira bali wajitume kwa bidii ili wafikie malengo ya kujiongezea kipato sambamba na kukuza uchumi wa nchi.

CAPTION 

Picha no. 0112- MKUU wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Ayoub Mohamed Mahmou akiwahutubia na kufunga Mafunzo ya  kuwajengea uwezo wanawake kuzitambua furza zilizomo katika sekta ya utalii Zanzibar, yameandaliwa na NVCT Zanzibar.
Attachments area

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.