Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Amekutana na Mwakilishi Mkaazi wa WHO Nchini Tanzania Dkt. Tigest Ikulu Zanzibar leo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Kimataifa la Afya Duniani (WHO) Nchini Tanzania Bi.Dkt.Tigest Ketsela Mengestu, alipofika Ikulu Zanzibar,kwa mazungumzo na kujitambulisha leo kwa Rais wa Zanzibar. 


Rais Dk. Shein alikutana na Dk. Tigest Ketsela Mengestu, Mwakilishi Mkaazi mpya wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania na kulipongeza Shirika hilo kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa Shirika la (WHO),lina historia ya miaka mingi  katika kuiuinga mkono na kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kusaidia katika maradhi mbali mbali yakiwemo Kipindupindu yalivyotokea hapo siku za nyuma katika historia ya Zanzibar.

Alieleza kuwa mbali ya maradhi hayo, (WHO) imekuwa ikisaidia kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na maradhi mbali mbali pamoja na kushirikiana na Zanzibar katika kuwasomesha wataalamu wa afya.

Pia, Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa Shirika hilo la (WHO) kuendelea kufanya kazi na Wizara ya Afya huku akiahidi kuwa Serikali anayoiongoza itaendelea kushirikiana na viongozi hao wote wapya wa Mashirika ya (UN) watakaofanya kazi za hapa nchini.

Nae Dk. Tigest Ketsela Mengestu, ambaye alifika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais wa Zanzibar alipongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein katika kuimarisha sekta ya afya na kuahidi kuwa  Shirika la (WHO) litaendelea kuisadia na kuiunga mkono Zanzibar.

Kadhalika, Dk. Mangestu alimpongeza Rais Dk. Shein kwa juhudi zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi katika kuhakikisha mapambano ya maradhi ya Malaria yanapungua na kuondoka kabisa katika visiwa vya Zanzibar na kuwa kigezo kwa nchi nyengine duniani.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.