Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia wakati wa Maadhimisho ya Miaka 50 ya Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) hafla hiyo ya maadhimisho hayo imefanyika katika viwanja vya Hoteli ya Kitalii ya Verde Mtoni Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ameitaka Wizara ya Biashara na
Viwanda pamoja na uongozi wa Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC), kufanya
utafiti wa mimea na mazao ya kibiashara, ili kuyaongezea thamani na kuimarisha
uchumi wa taifa.
Amesema utafiti unapaswa
kufanyika ili kupanua wigo wa matumizi ya bidhaa zinazozalishwa, ikiwemo
karafuu.
Dk. Shein amesema hayo jana
katika viunga vya Hotel Verde iliyoko Mtoni mjini hapa, katika maadhimisho ya
miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Shirika la ZSTC.
Maadhimisho hayo yaliwashirikisha viongozi wa Serikali,
wafanyakazi pamoja na wadau mbali mbali wa mazao ya biashara yatokanayo na
kilimo, ikiwemo wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Alisema wakati umefika kwa ZSTC
kuwa na kitengo maalum kitakachojitegemea na kufanya kazi za utafiti, kwa
kushirikiana na Wizara za Kilimo, maliasili, mifugo na uvuvi na taasisi nyenginezo
za utafiti, ikiwemo COSTECH ili kuziongezea thamani ya bidhaa zinazotengenezwa.
Alisema mafuta yatokanayo na mimea
hiyo, hususan karafuu ni nyenzo kuu ya kiwanda cha makonyo, na kubainisha haja
ya kuendelezwa mazao mengine ya biashara yatakayoleta tija kwa Taifa.
“Napenda kutowa wito maalum
kwenu uongozi wa Wizara Biashara na Viwanda pamoja na ZSTC kutilia maanani
suala la kufanya utafiti ili kupanua wigo wa matumizi wa mazao tunayozalisha ,
sote tunaelewa karafuu ina matumizi mengi ikiwemo utenegenzaji wa dawa za
meno,dawa za tiba lakini pia huongeza ladha katika sigireti, wakati mafuta
yatokanayo na mimea hutumika kwa masaji
na kuongeza ladha ya chakula”, alisema.
Alipongeza juhudi
zinazoeendelea kuchukuliwa na Shirika hilo katika kuwahudumia vyema wakulima wa
karafuu pamoja na kuwahamasiha katika kilimo cha mazao ya viungo, hivyo akaitaka Wizara ya Biashara na Viwanda
kusimamia dhamira ya Serikali ya kuitaka ZSTC kufanya biashara nyengine na
kujiimarisha.
Dk. Shein alipongeza juhudi
zilizonyika za kukiimarisha kiwanda cha uzalishaji wa mafuta ya makonyo na mime
mingine kiliopo Wawi Pemba, kwa kupata Mwekezaji na kuongeza uzalishaji, hatua
aliyosema inaendeleza sekta ya uwekezaji pamoja na ukuaji wa sekta ya viwanda.
Aidha, Dk. Shein alipongeza
mafanikio makubwa yaliopatikana katika uimarishaji wa zao la Karafuu, hatua
aliyosema inatokana na mageuzi makubwa ya Shirika la ZSTC.
Alieleza kuwa uamuzi huo wa
Serikali ulitokana na Ilani ya CCM (2010-2015), kwa kubadilisha muundo na mfumo
wa uendeshaji wa shirika pamoja na sera ya malipo kwa wakulima wa zao hilo.
“Mnamo mwaka 2011 Serikali
ilitunga sheria mpya ya ZSTC namba 11 ya mwaka 2011, inayoipa mamlaka makubwa
zaidi ZSTC kulisimamia,kulihudumia,kuliimarisha na kuhakikisha zao hilo linapata
maendeleo endelevu kwa maslahi ya wakulima wetu”, alisema.
Alisema miongoni mwa mafanikio yaliopatikana kutokana
na hatua hiyo ni pamoja na kuimarisha na kulinda ubora wa Karafuu za Zanzibar,
kuongeza kiwango cha uzalishaji, sambamba na upandaji wa mikarafuu mipya.
Alibainisha kuwa utafiti wa
‘Zanzibar Woody Biomass Survey’, uliofanyika Novemba, 2013 umeonyesha mafanikio
makubwa ya kiwango cha mikarafuu kuongezeka hapa nchini hadi kufikia 6,554,587,
huku mikarafuu 2,700,000 iliyopandwa ikiainishwa kustawi na kuanza kuzaa.
Aidha, Dk. Shein alisisitiza
ahadi ya serikali ya kuendelea kuwanufaisha wakulima wa zao hilo kwa kuwalipa
asilimia themanini ya bei ya soko la Dunia, katika mazingira yote, iwe kupanda
bei ama kushuka.
Alisema Serikali itaendelea na
juhudi zake za kuwaondolea usumbufu wakulima katika usafirishaji wa zao hilo
kuelekea vituo vya ununuzi kwa kuimarisha miundo mbinu ya barabara.
Alisema tayari Serikali imetowa
agizo kwa kwa shirika la ZSTC, Wizara inayoshughulikia miundombinu, Ardhi na
Kilimo kuchukuwa hatua za kuanzisha barabara zinazokwenda kwenye maeneo inayolimwa
kwa wingi mikarafuu kisiwani Pemba.
Katika hatua nyengine, Dk.
Shein alitowa wito kwa uongozi wa ZSTC
kuhakikisha inautumia ipasavyo muundo mpya wa Utumishi wa Shirika katika
upandishaji wa madaraja (promotion) ya wafanyakazi, sambamba na kulitaka kubuni
utaratibu wa kuwazawadia wafanyakazi wake (bonus) pale wanapofanya vizuri na
kuvuka malengo waliyowekewa.
Mapema, Waziri wa Biashara na
Viwanda Amina Salum Ali, alisema wakati Shirika la Biashara likiadhimisha miaka
50 ya kuanzishwa kwake, kuna umuhimu wa kufanya tathmin na kupanga mikakati
mipya ya kuliendeleza, sambamba na kuwa na kauli moja na wadau wa biashara ya
karafuu Duniani kote.
Alisema katika kipindi hicho,
Shirika limepata mafanikio makubwa na hivyo kuwa na uwezo mkubwa wa kuchangia
utoaji wa huduma za kijamii pamoja na kuimarisha uchumi wa taifa.
Nae, Mwenyekiti wa Bodi ya
ZSTC, Kassim Ali alitowa pongezi kwa awamu zote saba za Uongozi wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, kwa kulishughulikia vyema zao la karafuu pamoja na mazao
mengine ya viungo, na hivyo kuleta ustawi wa kiuchumi.
Shirika la ZSTC lilianzishwa
kwa sheria ya mashirika ya umma namba 1 ya mwaka 1968, likiwa miongoni mwa
mashirika ya mwanzo ya serikali kuanzishwa baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya
1964.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024
2231822
E-mail:
abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment