Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein,akizungumza na Bodi ya Shirika la Utangazaji Zanzibar ZBC na Uongozi wa Shirika hilo Ikulu Zanzibar.kulia Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee na kushoto Waziri wa Habari Utalii na Mambo ya Kale Mhe. Mahmoud Thabit Kombo.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameeleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya
kuendelea kuliimarisha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) ili liweze kwenda
na wakati uliopo.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo Ikulu mjini Zanzibar, wakati alipokutana na Uongozi wa Wizara ya
Habari, Utalii na Mambo ya Kale, uongozi wa (ZBC) pamoja na Bodi ya Shirika la Utangazaji
Zanzibar (ZBC) kwa lengo la kuliimarisha Shirika hilo.
Katika maelezo yake Rais
Dk. Shein alieleza kuwa (ZBC) ni Shirika la Utangazaji ambalo lina historia ya
muda mrefu hivyo linapaswa kufanya shughuli zake kulingana na wakati uliopo
bila ya kupoteza malengo ya kuanzishwa kwake.
Rais Dk. Shein
alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweza kulibadilisha Shirika
hilo kwa kununua vifaa mbali mbali vya kisasa vyenye uwezo mkubwa wa kurusha
matangazo na utengenezaji wa vipindi na hivyo kuliwezesha Shirika kumudumu
ushindani katika tasnia ya habari na mawasiliano.
Aliongeza kuwa juhudi
za makusudi zimeendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuhakikisha Shirika hilo
linaimarika na linarudi katika uhalisia wake kama ilivyokuwa hapo siku za nyuma
ambapo taasisi nyingi za habari za ndani na nje ya Tanzania zilijifunza kupitia
Shirika hilo kongwe na lenye uzoefu mkubwa.
Dk. Shein amesisitiza
haja kwa Shirika hilo kuandaa Mpango wa kuendeleza wafanyakazi wake ili liweze
kuendelea kufanya kazi zake kwa ufanisi kulingana na mabadiliko ya sayansi na
teknolojia yanayoendelea kukua kwa kasi ulimwenguni.
Rais Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Shirika hilo kwa kufanikisha vyema Sherehe
za Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 mwaka huu ambazo kilele chake
kilifanyika huko uwanja wa Gombani Chake Chake Pemba hivi karibuni.
Aidha, Rais Dk. Shein
alisisitiza haja ya kuyaendeleza malengo ya Shirika hilo la (ZBC )ikiwa ni pamoja
na kutoa taarifa, kuelimisha na kuiburudisha jamii.
Alifahamisha kuwa
pamoja na kuwa Shirika hilo linapaswa kujiendesha kibiashara pia, ni vyema kuwa
na mpango mkakati utakaozingatia malengo pamoja na vipaumbele katika
utekelezaji wa shughuli zake.
Akizungumzia maendeleo
ya Shirika hilo, Rais wa Zanzibar amesema kuwa (ZBC) imekuwa ikifanya vizuri
hasa baada ya kupatiwa vifaa vya kisasa licha ya changamoto ndogo ndogo ambazo zimekuwa
zikikabiliana nazo.
Nae Waziri wa Habari,
Utalii na Mambo ya Kale Mahamoud Thabit Kombo alitoa pongezi zake kwa Rais Dk.
Shein kwa juhudi zake anazozichukua katika kuhakikisha Shirika hilo linaimarika
na linazidi kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Waziri Kombo alieleza
kuwa licha ya kuwepo baadhi ya changamoto ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi
Shirika hilo limekuwa likifanya kazi zake vizuri na kuweza kutoa elimu ya
televisheni na taarifa mbali mbali kwa jamii.
Nae Katibu Mkuu wa
Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee
alisisitiza haja kwa wafanyakazi wa Shirika hilo kufanya kazi kwa mashirikiano
ili kuweza kutekeleza malengo yaliowekwa.
Alieleza kuwa kutokana
na wakati uliopo suala la teknolojia sambamba na kuwepo kwa mpango maalum wa
kuliendesha Shirika hilo haliepukiki hivyo mashirikiano yanahitajika kati ya
wafanyakazi, uongozi wa (ZBC), Bodi ya (ZBC) pamoja na uongozi wa Wizara.
Mapema uongozi wa (ZBC)
ulieleza mafanikio na changamoto walizonazo na jinsi zinavyofanyiwa kazi kuzitatua
hivi sasa huku wakitumia fursa hiyo
kutoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais
Dk. Shein kwa kuliendeleza na kuliimarisha Shirika hilo ikiwa ni pamoja na
kulipatia vifaa vya kisasa.
Uongozi huo ulieleza
juhudi zinazoendelea kuzichukua katika kuhakikisha malengo yaliyowekwa
yanafikiwa na kueleza jinsi walivyofanikiwa katika utendaji wao wa kazi ikiwa
ni pamoja na kuzalisha vipindi mbali mbali vya redio na televisheni kwa mwaka
huu ikilinganishwa na mwaka jana.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment