Habari za Punde

Waumini wa Dini ya Kiislam Watakiwa Kuelewa Msikiti ni Nyumba ya Mwenyenzi Mungu.Inayowakutanisha Kuteleleza Dini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Sheikh Abdullah Talib alipofika Maungani Wilaya ya Magharibi “B” kuufungua Msikiti Salama { Masjid Salama } wa Kijiji hicho.Kulia ya Sheikh Talib ni Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikha Fadhil Suleiman Soraga.

Mjumbe wa Kamati ya Msikiti Salama wa Maungani Dr. Ali Uki akisoma Risala kwenye hafla ya Ufunguzi rasmi wa Masjil Salama Maungani Wilaya ya Magharibi “B”.
Waumini wa Dini ya Kiislamu wakimsikiliza  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hayupo pichani wakati akiufungua rasmi Msikiti Salama wa Maungani.

Waumini wa Dini ya Kiislamu wakimsikiliza  Sheikh Khalid Ali Mfaume kutoka Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar hayupo pichani wakati akitoa risala ya umuhimu wa msikiti katika Uislamu. Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewakumbusha Waumini wa Dini ya Kiisalamu kuelewa kwamba Msikiti ni nyumba ya Mwenyezi Mungu inayowakutanisha kutekeleza Nguzo ya Pili ya Dini hiyo inayojumuisha pamoja na mambo mengine Ibada ya sala, Elimu, Maarifa  pamoja na Malezi kwa Watoto.
Alisema katika kutekeleza hayo Waumini hao wanapaswa kuwa madhubuti katika kuilinda Misikiti  kutokana na madarasa ya uchochezi yaliyoibuka katika baadhi ya sshemu Nchini ambayo huwa na muelekeo wa kuwagawa Waumini Kibadhehebu au Kisiasa.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kumbusho hilo wakati wa hafla ya Ufunguzi wa Msikiti Salama { Masjid Salama } uliojengwa kwa nguvu za Waumini wenyewe wa Dini ya Kiislamu pamoja na misaada ya Wahinsani katika Mtaa wa Maungani Wilaya ya Magharibi “B” Mkoa Mjini Magharibi.
Alisema Jamii imekuwa ikishuhudia ongezeko kubwa la dhulma na mmong’onyoko wa Maadili unaochangiwa na vitendo vya Ubakaji, Ulawiti, udhalilishaji wa Watoto Wadogo, Utumiaji wa Dawa za Kulevya kwa kiwango cha kutisha mambo yanayosababishwa na upungufu wa Maadili yanayopaswa kutiliwa mkazo hasa kwenye madarasa Misikitini.
Balozi Seif aliwaomba Waumini na Wananchi wote Nchini kuendelea kushirikiana kwa pamoja katika kuondosha maasi hayo yaliyokithiri na kutishia Imani za waja ambayo tayari yameshakemewa na Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Mtume Muhammad {SAW}.
“ Masheikh wetu wajitahidi kuielimisha Jamii juu ya athari ambazo Mja anaweza kuzipata kwa kuendeleza vitendo viovu”. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Alieleza kwamba Msikiti ni Nyumba isiyo na mbadala kutokana na utukufu wake. Hivyo aliwanasihi  Wana Maungani kutumia Mali na nguvu zao zote katika kuutunza ili ubakie Mpya, wakupendeza ili uendelee kuhudumia kazi ya mola ya kuabudiwa na Viumbe vyake.
Balozi Seif alisema zipo Hadithi zinazohimiza juu ya wajibu wa kuishughulikia Misikiti na kuitumikia ili wale waliokuwa mstari wa mbele  kwa jambo hilo wazidi kuongeza harakati na wale waliowazito kutoa mali zao washajiike kutoa msukumo huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Mwenyezi Mungu ameamrisha Waja wake kutoa sehemu ya Mali zao ili ziwanufaishe wengine katika Jamii na kuahidi kuwalipa Waja hao watakaotoa kwa ajili ya fisabili – llahi.
Alisema kwa bahati mbaya wapo Waumini wachache miongoni mwao wanaoelewa umuhimu wa kutoa mali zao kwa ajili ya kumtakasa Mwenyezi Muungu katika maamrisho aliyowaelekeza waja wake kumtakasa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Waumini wa Maungani pamoja na maeneo jirani waliotoa wazo na kuanza kufikiria ujenzi wa Jengo hilo la Ibada wazo lililopokewa na Muumini aliyejitolea kutumia mali zake kumaliza ujenzi wa Msikiti huo.
“ Ye yote anayekufanyieni mambo mema, basi mlipeni na mtakapokosa cha kumlipa basi muombeeni dua kwa Mwenyezi Mungu”. Balozi Seif alisisitiza hilo wakati akikariri Maneno ya Nabii Muhammad {SAW}.
Akisoma Risala kwa niaba ya Wamini wa Dini ya Kiislamu wa Masjid Salama Dr. Ali Uki alisema baadhi ya  Waumini wa Kijiji cha Maungani walilazimika kufanya Ibada zao ndani ya Majumba yao hasa kwa ile Sala ya Alfajiri kutokana na umbani wa Msikiti uliopo kwenye eneo hilo kwa kuhofia kiza kilichotanda katika eneo hilo.
Dr. Uki alisema usumbufu huo uliwapa fikra iliyozaa maarifa ya kuanza ujenzi wa Jengo lao la Ibada ili kuondokana na kadhia hiyo iliyopelekea jitihada zao kuzaa matunda ya kuanza ujenzi ndani ya kipindi cha Miaka Mitano iliyoanzia Mwezi Mei Mwaka 2014.
Alisema Ujenzi huo ulioanzishwa kwa nguvu za Waumini wenyewe ulipata baraka za kuunga mkono na Taasisi moja ya Kiserikali iliyojitolea kusaidia Mabati 100 pamoja na Waumini wawili wa Dini ya Kiislamu Mume na Mkewe mwenye asili ya Zanzibar wanaoishishi Nchini Oman.
Dr. Uki aliiambia hadhara hiyo iliyohudhuria ufunguzi wa Masjid Salama kwamba harakati za ibada ya sala zilianza Rasmi mnamo Tarehe 29, Januari Mwaka 2018 wakati jengo hilo tayari limeshapata usajili Mwezi Juni Mwaka 2016 kutoka Taasisi husika na masuala ya Kiislamu Nchini.
Alifahamisha kwamba wakati Msikiti huo ukifanikiwa kuwa na uwezo wa kusaliwa na Waumi ni wapatao 250 kwa wakati Mmoja umejengwa kwa Gharama inayokadiriwa kufikia zaidi ya Shilingi za Kitanzania Milioni 200,000,000/- .
Dr. Uki alisema Jengo hilo la Ibada  lina Sehemu za kusaliwa kwa Wanaume, Wanawake, Madrasa sambamba na Sehemu Maalum ya kuoshea Maiti pale inapotokezea Fardhi ndani ya Mtaa huo uliopo Magharibi mwa Mji wa Zanzibar.
Mjumbe huyo wa Kamati ya Msikiti Salama aliwaomba radhi kwa niaba ya wenzake baadhi ya Mafundi kwa hitilafu zilizojitokeza wakati wa Ujenzi wa Msikiti huo ambapo Kamati ya usimamizi ililazimika kuwa kali ili ujenzi huo ufikie kiwango kinachokubalika.
Akitoa Mawaidha kuhusu umuhimu wa Msikiti Sheikh Khalid Ali Mfaume kutoka Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar alisema kuimarisha Msikiti maana yake Waumini wasali sala Tano na kwa wakati wake mahsusi.
Sheikh Khalid alisema kazi hiyo inakwenda sambamba na kazi ya Mwenyezi Muungu Mola wa Viumbe vyote aliyeumba Mbingu na Ardhi anayeshusha utulivu kwa  Waumini wanaoamini kubakia Msikitini baada ya Sala wakisoma Quran na kufundishana maamrisho yake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.