Habari za Punde

Serikali kuweka mashine ya ukaguzi Bandari ya Mkoani Pemba

Na Takdir Ali-Maelezo Zanzibar 15.02.2019
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Shirika la Bandari limeanza kuweka Mashine ya ukaguzi katika Bandari ya Mkoani Pemba na inategemea kuweka katika Bandari zote zilizobakia.
Hatua hiyo ina lengo la kuendeleza kuimarisha ulinzi na usalama kwa kuwakagua Abiria na Mizigo yao ili nchi iendelee kuwa salama.
Naibu Waziri wa Ujenzi,Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Muhammed Ahmada Salum ametoa kauli hiyo alipokuwa akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Chake chake Suleiman Sarahan Said katika Kikao cha Baraza kinachoendelea.
Amesema kwa mujibu wa Kanuni za Kimataifa za ulinzi na usalama “International Ships and Port Facility Security Code” (ISPS Code), maeneo ya kuingia na kutoka nchini kama bandarini kunatakiwa kukaguliwa abiria na mizigo yao ili kuhakikisha abiria, mizigo na miundombinu ya bandarini pamoja na meli zipo hali ya usalama.
Naibu Waziri huyo ameeleza kuwa Wizara kupitia Shirika la Bandari imeanza kutekeleza kanuni hizo kwa kuweka mashine za ukaguzi wa Abiria na Mizigo kwa Bandari ya Unguja kwa abiria wanaotoka na kuingia Unguja na Dar es salaam na kwa upande wa Pemba wameweka katika Bandari ya Mkoani.
Amefahamisha kuwa utaratibu wa zoezi hilo umeleta mafanikio ya uhakika katika ulinzi na usalama kwa abiria na mali zao katika vyombo wanavyopanda.
Hata hivyo amesema Serikali inaandaa mikakati ya kuweka Mashine katika Maeneo yote ya Bandari kwani mashine moja iliyopo katika Bandari ya Mkoani haitoshelezi kulingana na wingi wa abiria.
Hivyo Naibu Waziri huyo amesema kutokana na abiria wanaosafiri kuwa wengi kwa wakati mmoja Shirika la Bandari limedhamiria kuweka Mashine ya pili ili kuondosha msongomano wa abiria wakati wa kupanda na kushuka Meli.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.