Habari za Punde

Uwekaji wa Jiwe la Msingi Majengo ya Skuli ya Msingi Kwarara ya Ghorofa Mbili


Rais wa Zanzibar na Mwenmyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akiwa na Mama Mwanamwema Shein wakimsikiliza Msanifu Majengo wa Kampuni ya SRAT Consuat ya Tanzania,inayosimamia Ujenzi wa Majengo ya Skuli ya Kisasa ya Msingi Kwarara Ndg. Salim Rajab Twakyondo, akitowa maelezo ya michoro ya ramani ya majengo ya Skuli hiyo wakati wa ziara yake na kuweka Jiwe la Msingi la Mradi huo leo, akiwa katika ziara yake katika Wilaya ya Magharibi B, Unguja.

Na.Abdi Shamnah.Ikulu Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar  na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein  amesema katika kutekeleza sera ya elimu bila malipo, Serikali inaendelea na juhudi za kuimarisha miundo mbinu ya kielimu ili kwenda sambamba na mahitaji yaliopo.
Dk Shein amesema hayo leo katika hafla ya  uwekaji wa jiwe la Msingi wa Skuli ya msingi Kwarara, Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja.

Amesema kutokana  na  ongezeko kubwa la wanafunzi hali inayotokana na kiwango kikubwa cha wakaazi wa Zanzibar hivi sasa, Serikali inalazimika kuongeza idadi ya madarasa ili kwenda sambamba na ongezeko la wanafunzi katika skuli za msingi na sekondari.

Alisema ongezeko la idadi ya watu kutoka 300,00 mwaka 1964 hadi kufikia Milioni moja na nusu hivi sasa imefanya kuwepo mahitaji makubwa ya madarasa , huku baaadhi ya skuli zikiwa na wanafunzi wanaofikia 234 katika darasa moja,

Alisema hivi karibuni Serikali  imeagiza madawati na vikalio 44,000 kutoka nchini China  na kubainisha kuwa nusu ya samani hizo zimewasili nchini na kugawiwa katika skuli za msingi na sekondari.

Dk. Shein alisisitiza azma ya serikali na kuwataka wazazi na walezi wa wanafunzi kutokuchangia huduma zote za kielimu katika skuli za msingi  na sekondari, ikiwemo vitabu madaftari

Alisema lengo la serikali ni kuwaandaa vijana wake kielimu ili kufanikisha azma ya kuwa an wataaalamu  katika fani mbali mbali ili kuliwezesha Taifa kupata maendeleo ya haraka.

Alisema uchumi wa Zanzibar umeendelea kuimarika kadri miaka inavyosonga hatua inayotokana an makusanyo mazuri ya mapato na kubainisha kuwa hivi sasa Serikali inakusanya kati ya  shilingi Bilioni 65 hadi 70 kwa mwezi, hivyo kumudu gharama za uendeshaji wa  miradi mbali mbali ya maendeeo, ikiwemo ya maji na barabara.

Alisema hali hiyo imechangia kufanikisha azma ya serikali ya kusomesha wataalamu wake katika fani tofauti, ikiwemo madaktari.

Akigusia historia ya elimu nchini, Dk. Shein alisema Mapinduzi ya 1964 yamekuja kuwakomboa watoto wa wanyonge kutokana an dhuluma ya kukoseshwa elimu.

Alisema wakati chama cha ASP kikipigania uhuru, kilibainisha wazi katika Ilani zake, dhamira ya kuipa kipaumbele elimu na kutolewa bila malipo.

Alisema elimu ina umuhimu mkubwa katika maisha ya binadamu, kama Mwenyezi Mungu alivyobainisha katika kitabu kitakatifu cha Qoraan.

Alisema ni lengo la Serikali katika siku zijazo kujenga skuli za msingi za ghorofa, ili kukidhi mahitaji kutokana na  ufinyu wa ardhi uliopo.

Dk. Shein alichukuwa fursa hiyo kuipongeza taasisi ya Good Neighbor kutoka Jamuhuri ya  Korea Kusini kwa msaada mkubwa wa kufanikisha ujenzi  wa skuli iyo.

Nae, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma amesema alisema Wizara hiyo kwa kushirikiana an Wizara ya Nchi (OR) Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa, Tawala za Mikoa, idara maalum  na Vikosi vya SMZ pamoja na Jamuhuri  ya Korea italiendeleza jengo hilo katika awamu inayofuata.

Waziri Pembe alimhakikishia Rais Dk. Shein kuwa huduma za kielimu pamoja na vitabu na madaftari zitaendelea kutolewa bure nchini kote ili kwenda sambamba na Sera ya Elimu,
Mapema,Naibu Katibu Mkuu Wizara ya elimu na maunzo ya Amali Madina Mjaka, alisema ujenzi wa skuli hiyo itawasogeza wanafunzi karibu  na makazi, kama ilivyoainishwa kwenye ilani ya CCM.

Aidha, alisema itapunguza mlundikano wa wanafunzi wa skuli za jirani, hususan Kijitoupele, ambapo kwa sasa darasa moja hujumuisha hadi wanaafunzi 100 – 120.

Alisema awamu ya kwanza ya ujenzi wa skuli hiyo umegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 1.5, ambapo skuli hiyo inatarajiwa kuchukuwa wanafunzi 3,780.

Aidha alisema katika kufanikisha ujenzi wa skuli hiyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetowa msamaha wa vifaa vya ujenzi pamoja na kuchangia samani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.