Habari za Punde

Kongamalo la UWT Hoteli ya Verde Mtoni Zanzibar.

Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan, akihutubia wakati akilifungua Kongamano la Umoja wa Wanawake Tanzania UWT, la kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, lililofanyika katika Viwanja vya Hoteli ya Verde Mtoni Zanzibar leo.

Na Mwashungi Tahir  - Maelezo.
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amesema anampongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein kwa kuwapa nafasi za uongozi wanawake wengi .
Ameyazungumza huko katika ukumbi wa Verde wakati alipokuwa akifungua Kongamano la Wanawake la kumpongeza Mhe  Dkt Ali Mohamed Shein Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kutimiza miaka mitatu ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi.
Amesema akina mama wamepata fursa nyingi walizopewa na Mh Rais ambazo amewateua  zikiwemo nafasi za siasa na uongozi Zanzibar , Wawakilishi, Mawaziri, Manaibu Waziri , Wakurugenzi , makatibu na Naibu katibu wakuu, Majaji, Naibu Spika ,Wakuu wa Wilaya  na Makatibu Tawala.
Pia alieleza kwamba wanawake hao walioaminiwa wanafanya kazi vizuri  na ni mfano wa kuigwa kwani wameiletea heshima kubwa sana katika utendaji na amewaomba wazidi kufanya kazi zao kwa kujiamini zaidi.
Aidha amesema Serikali ya Mapinduzi chini ya uongozi mahiri wa Dokta Shein imefanya kila linalowezekana  ili kuboresha hali ya maisha ya wananchi wake kwa kupitia miradi mbali mbali ya maendeleo katika sekta zote za kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Vile vile Mama Samia alisema Dkt Shein ameendeleza na kuimarisha kwa ufanisi mambo mengi ikiwemo uimarishaji wa huduma ya afya na kuweza kupatikana bure na  Elimu, ujenzi wa miundo mbinu, kilimo, ufugaji na ushirika  na kuwezesha wazee, wanawake na walemavu.
Akitoa wito kwa wana UWT na wanawake wote kwa jumla  na kuwafahamisha kwamba wao ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi  hivyo  kongamano hilo liwe chachu katika kuchapa kazi na kushikamana na kuleta mashirikiano kwa kuleta maendeleo mwa jamii nzima.
Nae Mwenyekiti wa UWT Taifa Gaudencia Kabaka  alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina mashirikiano makubwa na Chama cha Mapinduzi katika utendaji wa kazi na kuwataka wazidishe mashirikiano ili kazi ziendelee kwa vizuri na kuzidi kupatikana maendeleo.
Sambamba na hayo Manaibu Mawaziri wa sekta mbali mbali walitoa mafanikio  yaliofanywa na Dkt Shein katika kutekeleza ilani kwa vitendo na kumtakia kila la kheri kwa kuyafanya yale yote alojipangia kuyafanya katika uongozi wake kwa wananchi na kumpa pongezi wa uimarishaji wa sekta hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.