Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Ziarani Nchini Cuba leo.

Waziri wa Fedha na Mipango wa SMZ Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa akimtakia safari njema Balozi Seif  kwenye ziara yake Maalum anayokwenda Nchini Jamuhuri ya Cuba.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiagana na baadhi ya Watendaji Waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar wa Abeid Aman Karume akielekea  Nchini Cuba kwa ziara Maalum. 
Wafanyakazi wa Wakala wa Ndege za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wakimkaribisha Balozi Seif  kwenye Ndege hiyo kuelekea Mjini Dar es salaam kwa safari ya Cuba.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameondoka Zanzibar leo mchana kupitia Jijini Dar es salaam kuelekea Nchini Jamuhuri ya Cuba kwa ziara Maalum.
Balozi Seif  Ali Iddi katika safari hiyo Maalum anafuatana na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi pamoja na baadhi ya Wasaidizi wake  wa kazi.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliagwa na Viongozi mbali mbali wa Serikali, Vyama vya Siasa pamoja na baadhi ya Maafisa Waandamizi wa Serikali wakiongozwa na  Waziri wa Fedha Zanzibar Balozi Mohamed Ramia.
Pamoja na mambo mengine  akiwa Nchini Cuba Balozi Seif amealikwa na Serikali ya Nchi hiyo kupitia Wizara ya Kilimo kuhudhuria Maonyesho ya 40 ya Kimataifa ya Kilimo yanayotarajiwa kufanyika katika Mji mkuu Havana.
Katika maonyesho hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ataambatana pia na Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar Mh. Mmanga Mjengo Mjawiri na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Bibi Asha Ali Abdulla.
Fursa hiyo itamuwezesha  kufanya mazungumzo na baadhi ya Viongozi Wakuu wa Taasisi zinazosimamia Sekta za Kilimo na Afya katika azma ya kuonyesha uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Zanzibar na Cuba.
Balozi Seif  na Ujumbe aliofuatana nao anatarajiwa kurejea Nyumbani  Zanzibar Tarehe 25 Machi  Mwaka 2019.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.