Habari za Punde

Mwakilishi Pangawe awahakikishia wajasiriamali kuwatafutia masoko ya uhakika

Wilaya ya Magharibi B.                     13-03-2019.
Mwakilishi wa Jimbo la Pangawe Khamis Juma Maalim amesema atahakikisha anafanya ushawishi kwa Viongozi wa Wizara ya Biashara na Masoko na ile ya inayohusiana na Wanawake ili kubuni mbinu zitakazosaidia Wajasiriamali Wanawake katika Jimbo la Pangawe kuweza kupata Masoko ya uhakikika ya kuuza bidhaa wanazozizalisha.
Ameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati Kamati ya mfuko wa maendeleo ya Mwakilishi Jimbo La Pangawe ilipofanya ziara ya kuangalia vikundi vya Ujasiriamali katika Jimbo hilo.
Amesema katika ziara hiyo wamebaini matatizo mabali mbali kama vile uhaba wa masoko,mali ghafi na baadhi kutokuwa na usajili mambo ambayo yanarudisha nyuma ustawi na maendeleo ya vikundi hivyo.
Aidha amewataka Wanachama hao kutovunjika moyo kutokana na matatizo hayo na badala yake wazidishe bidii ya kufanya kazi ili matatizo hayo yaweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Hata hivyo amewashauri wanavikundi hao kufanya ziara katika vikundi vyengine ili kubadilishana mawazo na kupata ujuzi utakaviwewezesha vikundi hivyo kufanya kazi kwa ufanisi na kufikia malengo ya kuanzishwa kwa Vyama vya ushirika Zanzibar.
Kwa upande wake Mjumbe wa kamati ya mfuko wa maendeo ya Mwakilishi Jimbo la Pangawe Issa Mohamed Zonga amesema lengo la kufanya ziara hiyo ni kuweza kubaini mapungufu yaliopo katika vikundi vya ujasiriamali vya akinamama na kuweza kuyapatia ufumbuzi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.