Habari za Punde

Kikosi cha Timu ya Malindi Chaibuka Kidedea Michuano ya Ligi Kuu ya Zanzibar Kwa Kuifunga Timu ya KMKM Kwa Bao 1-0.

Na Hawa A Ally
TIMU ya Soka ya Malindi imefanikiwa kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya mabaaria wa KMKM mchezo uliopigwa hapo jana katika Dimba la Amaan katika mfululizo wa liggi kuu ya Zanzibar.
Bao Pekee la Timu ya Malindi lilipachikwa na mchezaji Ibrahim Abdalla dakika ya 24 ya  kipindi cha kwanza baada ya kutokea vuta nikuvute katika lango la mabaaria wa KMKM.
Kwa matokeo hayo kwa Upande wa Malindi imefanikiwa kutinga nafasi ya 4 ikitokea  nafasi ya  6 kwa alama zake 66. Huku mabaaria hao wa KMKM wameshuka  hadi nafasi ya 5 wakitokea nafasi ya 4 na  alama zake  65.
Aidha Katika Uwanja wa Mau majira hayo ya saa kumi Maafande wa Polisi wamefanikiwa kutoka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya timu ya Chuoni kwa matokeo hayo maafande wa polisi wamefikisha alama 46 na kuendelea kubaki nafasi ya 9, huku Chuoni wakiendelea kubaki nafasi ya 10 na alama zake  43.
Kwa upande wa Viwanja vya kisiwani wa Pemba Timu ya Jamuhuri na Kizimbani zimetoka sare ya bao 1-1 mchezo uliopigwa katika dimba la Gombani majira ya  saa kumi alasiri,  ambapo majira ya saa nane  katika Uwanja huo Timu ya  Mwenge ilifanikiwa kutoka ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Hard Rock.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena  April 13 kwa kupigwa  michezo mitatu, katika Uwanja wa  Amaan saa nane KVZ watavaana na zimamoto, huku majira ya saa kumi katika Uwanja huo  Polisi wataumana na Mlandege, na katika Uwanja wa Mau ze dong majira ya saa kumi Chuoni watapepetana na Malindi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.