Habari za Punde

Utoaji wa elimu ya maandalizi kuimarika

Afisa Maandalizi Idara ya Maandalizi na Msingi Bi Fatma Mode Ramadhani akimkaribisha Mkurugenzi Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ Nd. Abdulla Issa Mgongo katika ufunguzi wa mafunzo ya siku tano kwa wasaidizi wa vituo vya Tucheze Tujifunze.
 Mkurugenzi Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ Nd. Abdulla Issa Mgongo akizungumza na Wasaidizi wa Vituo vya Maandalizi vya  Tucheze Tujifunze wakati akifungua mafunzo ya siku tano katika ukumbi wa Skuli ya Maandalizi Madungu.

Wasaidizi wa vituo vya Tucheze Tujifunze wakiwa katika Ukumbi wa Skuli ya Maandalizi Madungu Chake Chake Pemba katika ufunguz wa Mafunzo ya Siku tano ya kuwajengea uwezo.





Na Ali Othman

Wasaidizi wa vituo vya maandalizi vya “Tucheze Tujifunze” kisiwani Pemba wametakiwa kuzingatia na kuyafanyia kazi  mafunzo wanayoyapata ili waweze kuwaandaa vyema watoto katika kuikabili elimu ya msingi.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ Nd. Abdulla Issa Mgongo wakati akifungua mafunzo ya siku tano katika ukumbi wa Skuli ya Maandalizi Madungu Chake Chake Pemba.

Akifafanua umuhimu wa mafunzo hayo, Nd. Mgongo amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wasaidizi wa vituo hivyo na hivyo kutambua kwamba wanawajibu mkubwa wa kuhakikisha kwamba watoto wanapata elimu bora.

Akielezea malengo ya kuanzishwa kwa vituo hivyo Nd. Mgongo amesema kuwepo kwa vituo hivyo kumesaidia kutatua tatizo la upatikanaji wa elimu ya maandalizi katika maeneo na vijiji ambavyo viko mbali na Skuli za Msingi.

Aidha Mkurugenzi huyo amesema, mbali na kuwapunguzia masafa watoto wadogo,  kuwepo kwa vituo hivyo katika maeneo  mbali mbali vijijini, kumesaidia kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji kwa watoto.

Awali Afisa Maandalizi Idara ya Maandalizi na Msingi Bi Fatma Mode Ramadhani akimkaribisha Mkurugenzi Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ Nd. Abdulla Issa Mgongo amesema kuwepo kwa vituo vya Tucheze Tujifunze “TUTU” kunasaidia kutekeleza lengo la Serikali la kuhakikisha kwamba kila mtoto mwenye umri wa miaka mine anapata elimu ya maandalizi.

Katika kuhakikisha kwamba mafunzo hayo yanafikia Ufanisi Mkurugenzi Idara ya Maandalizi na Msingi Bi Safia Ali Rijali kwa mashirikiano na Mkurugenzi Ofisi ya Rais TAMISEMI Nd. Abdulla Issa Mgongo wamekua wakifuatilia kwa karibu ili kuhakikisha kwamba mafunzo hayo yanatoa elimu bora kwa watoto.

Jumla ya vituo 344 vya Tucheze Tujifunze “TUTU” vimeanzishwa Zanzibar ambapo vituo 162 vipo Unguja na vituo 182 vipo kisiwani Pemba.




No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.