Habari za Punde

Wafanyabiasha Zanzibar Waashwa Kutopandisha Bidhaa Katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani Unaotarajiwa Mwezi Ujao.

Wafanyabiashara Zanzibar wametakiwa kuutumia mwezi Mtukufu wa Ramadhan, kwa kushusha bei za bidhaa zao, ili kuweza kupata fadhila za mwezi huo na kuacha kupandisha vitu  kiholela wakiamini kwamba ni lazima wananchi watanunua kutokana na umuhimu wake.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa Mufti Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Suraga, wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi, ofisini kwake Mazizini Mjini Unguja.
Alisema, wafanyabiashara walio wengi huweka bidhaa zao ndani na kusubiri kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, ili kuziuza kwa bei ya juu bila ya kujua kuwa wakifanya hivyo wanapata dhambi kubwa kwani mwezi wa ramadhani ni mwezi wa kutoa sadaka.
Alisema, ni madhambi makubwa sana kwa wafanyabiashara kupandisha bei katika kipindi cha mwezi wa Ramadhan, kwani ikumbukwe kwamba maswahaba wa mtume Muhammad (SAW) walikuwa wanapigania katika kutoa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
Sheikh Soraga, amewataka wafanyabiashara kuwa na huruma kwa watu ambao wamefunga, kwani ni haramu kungojea mwezi wa Ramadhan ndipo wawaumize wananchi kwa kupandisha bei ya bidhaa na kuwauzia wananchi bidhaa ambazo zilizokuwa mbovu.
Aidha, aliwataka waislamu kuacha kufanya mambo maovu kwa mwezi huu wa Shaaban, na badala yake kuweza kuzidisha ibada zaidi ili kuweza kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Alifahamisha kuwa, maandalizi ya kuukaribisha mwezi Mtukufu wa Ramadhan ni kuanza kufanya ibada kwa wingi na sio kama ambavyo watu wakifanya kwa kuanza kuchangishana kwa ajili ya michezo kama karata na bao.
Aidha, alieleza kuwa, ibada kubwa ya mwezi mtukufu wa Ramadhan ni kuweza kuswali sana swala za jamaa, kufunga mwezi wa Ramadhan, na kusoma sana Quran.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.