Habari za Punde

Wakuu wa Mikoa na Wilaya Watakiwa Kutoa Elimu ya Vitambulisho vya Wajasiriamali Wadogo

Na Lilian Lundo  - MAELEZO, Dodoma.         
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa Mikoa na Wilaya kutoa elimu ya Vitambulisho vya Wajasiriamali wadogo nchini.
Agizo hilo limetolewa leo Bungeni Jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbozi, Mhe. Pascal Haonga kuhusu watu waliolengwa kulipia vitambulisho hivyo kutokana na wajasiriamali hao kuwa na viwango tofauti tofauti vya mitaji.
"Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kuwafanya wajasiriamali wadogo kuweza kuchangia Pato la Taifa, Mhe. Rais alibuni njia nzuri ambayo inawatambulisha wajasiriamali. Hata hivyo wajasiriamali hao tumewaweka kwa madaraja yao wako  wadogo, wakati na wakubwa. Mhe Rais na Serikali iliwalenga Wajasiriamali wadogo ambao kipato chao hakizidi shilingi milioni Nne kwa mwaka," amesema Waziri Mkuu.
Amesema kuwa lengo ni wajasiriamali hao kuchangia pato la Taifa na pia kuwaondolea usumbufu katika maeneo wanakofanyia biashara zao kwa kutozwa ushuru wa shilingi 200 au 500 kila siku ambayo  imekuwa ikiwapunguzia mapato wanayopata kwa mwaka.
Ameendelea kusema, vitambulisho vingi hutolewa kwa Wakuu wa Wilaya, na anatambua kuwa kuna baadhi ya maeneo ambayo hutoa vitambulisho kwa kuwalazimisha watu badala ya kuwaelimisha namna ya kupata vitambulisho hivyo. Vile vile, yapo maeneo yanatoa vitambulisho kwa wajasiriamali wakubwa ambao pato lao ni zaidi ya milioni 4 kwa mwaka ambao wanatakiwa kuchangia TRA moja kwa moja.
"Maelekezo tunayoyatoa tena kwa Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya watumie  muda wao kuelimisha nani anapaswa kuwa na kitambulisho badala ya kutumia nguvu au kwenda kulazimisha au kuwapa wajasiriamali wakubwa wenye mapato zaidi ya milioni  4 na kuondoa maana ya uwepo wa vitambulisho," amesema Waziri Mkuu.
Ameeleza kuwa, Mhe. Rais aliwalenga wafanyabiashara kama wauza maandazi, watembeza mahindi vituo vya mabasi  ili na wao waone uchangiaji wa uchumi na pato la nchi ni sehemu yao lakini waendelee kufanya biashara zao bila kusumbuliwa katika halmashauri zao.
Wakati huo huo  ameeleza kuwa Serikali ina mkakati wa kupunguza maambukizi ya ukimwi kupitia kampeni mbalimbali za kupambana na maambuki ya UKIMWI zinazoendeshwa na TACAIDS, Taasisi inayosimamiwa na  Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Wizara ya Afya.
Amesema lengo la Serikali ni kila Mtanzania awe amepima na kujua afya yake ifikapo mwaka 2020. Vile vile wale waliopima na kugundulika na UKIMWI wawe ameanza kutumia dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI ifikapo 2020.
Serikali imekuwa ikitoa huduma za Upimaji wa UKIMWI katika kila eneo ambalo wanakutana zaidi ya wananchi 100 ili kutoa fursa ya Watanzania kupima na kujua Afya zao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.