Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akifuatilia maelezo ya ripoti ya Utekelezaji ya Mpango Kazi ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, ikiwasilishwa na Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Haji Omar Kheri, katika ukumbi wa Ikulu Ndogo Kibweni Zanzibar.
RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein,ameeleza
haja kwa Baraza la Manispaa Mjini
kuweka mikakati maalum katika kuendelea kuuweka Mji wa Zanzibar kuwa safi ili
kufikia malengo ya kuufanya mji huo kuwa Jiji.
Hayo aliyasema katika ukumbi wa Ikulu ndogo
Kibweni mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa,
Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ wakati ulipowasilisha taarifa ya
utekelezaji wa Mpango Kazi wa Wizara hiyo kwa Kipindi cha Julai 2018 hadi Machi
2019.
Dk. Shein alieleza kuwa mji wa Zanzibar hivi sasa
una wakaazi wengi sana hiyo ni kutokana na kuongezeka kwa mahitaji hali
inayosababisha kuwepo kwa ongezeko kubwa la taka.
Hivyo, Rais Dk. Shein alieleza umuhimu kwa Ofisi
hiyo kuweka mikakati maalum ya kuhakikisha Mji wa Zanzibar unakuwa safi na wa kuvutia
ili kuurejesha katika haiba yake ya asili na hatimae kufikia lengo la kuwa Jiji.
Alieleza kuwa mji wa Zanzibar unatambulikana
kitaifa na Kimataifa hivyo malengo ya kuufanya mji huo kuwa Jiji yatakapofikiwa
hivi karibuni itazidisha hamu kwa wageni kuja kulitembelea kutokana na vivutio
vyake mbalimbali vilivyomo ndani yake.
Hata hivyo, Rais Dk. Shein alieleza juhudi
mbalimbali za makusudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika kuhakikisha mji wa Zanzibar unaimarika kwa usafi pamoja na kuwa salama
kwa kuendeleza miradi kadhaa ukiwemo mradi wa Huduma za Miji (ZUSP).
Aidha, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo
kuupongeza uongozi wa Ofisi hiyo kwa juhudi zake katika Idara zake zote
sambamba na mashirikiano yaliopo kwa uongozi pamoja na watendaji wa Ofisi hiyo.
Rais Dk. Shein pia, alisisitiza kuwa ugatuzi
umeleta mabadiliko makubwa hivyo ni vyema kwa Ofisi hiyo kuendelea na mikakati yake
ili kufikia malengo yaliokusudiwa.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza
kufurahishwa kwake na juhudi zilizochukuliwa na Wizara husika zilizopewa kazi
za kupeleka huduma za jamii katika kijiji cha Mgonjoni huku akieleza hatua
zitakazochukuliwa katika kurekebisha barabara ya kuelekea kijijini huko baada
ya mvua kuleta athari.
Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza Wizara hiyo kwa kuwasilisha
vyema Mpango Kazi wake huku akisisitiza haja ya utekelezaji katika suala zima
la ugatuzi katika sekta zake zilizogatuliwa ikiwemo sekta ya afya, elimu na
kilimo.
Nao Washauri wa Rais kwa upande wao walipongeza
utekelezaji wa Mpango kazi huo na kusisitiza haja kwa Ofisi hiyo kupitia
Mabaraza yake ya Manispaa kuendelea kusimamia vyema masuala ya usafi hasa
katika mji wa Zanzibar.
Aidha, walieleza umuhimu wa kuangalia taratibu
nzima za uendelezaji wa masoko makuu kutokana na kuonekana kuwa masoko hayo
yamezidiwa na mahitaji ya wananchi wanaofuata huduma likiwemo soko la mboga
Mombasa, soko la Darajani na soko la Mwanakwerekwe.
Mapema, Waziri wa Wizara hiyo Haji Omar Kheri akiwasilisha
muhtasari wa Mpango kazi huo alieleza kuwa Serikali za Mikoa zimeendelea
kudhibiti na kuitafutia ufumbuzi migogoro ya ardhi iliyopo kwa mujibu wa sheria,
kanuni na taratibu zinazohusika na masuala ya ardhi.
Alieleza kuwa katika kipindi ha miezi tisa iliyopita idadi ya
migogoro ya ardhi ilioripotwa ni 119 kati ya hiyo migogoro 57 sawa na asilimia
48 ya migogoro yote ilioripotiwa tayari imepatiwa ufumbuzi.
Aliongeza kuwa Serikali za Mikoa na Wilaya na Mamlaka za
Serikali za Mitaa kwa kushirikiakana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
zimefanya juhudi kubwa ya kuihamasisha jamii katika suala zima la uandikishaji
wa wanafunzi wa maandalizi na msingi.
Pamoja na hayo, Waziri Kheri alisema kuwa Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa ma Idara Maalum za SMZ imeendelea kuchukua
hatua mbalimbali za kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa
wanawake na watoto.
Katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato katika Serikali za
Mitaa, alisema kuwa Ofisi kwa kutumia wataalamu wa ndani imesimamia kwa
kuhakikisha kila Manispaa, Baraza la Mji na Halmashauri zinakusanya mapato
kutoka vyanzo vyake vya mapato katika mfumo wa kielektroniki.
Hivyo, alisema kuwa hadi kufikia Machi 2019, Halmashauri
zote zimeunganishwa katika mfumo wa pamoja na ukusanyaji mapato na kuanza
kutumia mashine maalum za kukusanyia mapato katika maeneo ya maegesho, masoko
na vituo maalum vya ukusanyaji wa ada zitokanazo na maliasili zisizorejesheka.
Aidha, alisema kuwa katika kuimarisha taarifa za usajili wa
matukio ya Kijamii, Ofisi imesimamia zoezi la uandikishaji wa vitambulisho
vipya vya Mzanzibari Mkaazi ambalo lilifanyika katika Shehia zote 388 za
Zanzibar.
Sambamba na hayo alieleza kuwa Ofisi imeendelea kuzifanyia
matengenezo makubwa barabara za ndani katika kiwango cha lami, barabara zenye
urefu wa kilomita 2.98 zimefanyiwa matengenezo kwa kiwango cha lami.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment