Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, Akijumuika na Wananchi Katika Mazishi ya Marehemu Juma Ali Juma,




Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dk. Ali Mohamed Shein, akijumuika na Wananchi katika Sala na Dua ya kumuombea Marehemu Juma Ali Juma, aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar, iliofanyika katika Masjid ya Kijichi Wilaya ya Magharibi A Unguja leo. 


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein  leo ameongoza mazishi ya marehemu Juma Ali Juma yaliyofanyika Mwanakwerekwe, Wilaya ya Magharibi ‘B’, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Viongozi mbali mbali wa vyama na serikali pamoja na kutoka sekta binafsi wakiwemo wananchi, ndugu na jamaa walihudhuria  katika mazishi hayo.

Mapema asubuhi Alhaj Dk. Shein alifika nyumbani kwa marehemu Kijichi, Wilaya ya Magharibi A, Unguja na kuipa pole familia ya marehemu na kuwaomba wawe na moyo wa subira katika kipindi hichi kigumu cha msiba na baadae aliungana na viongozi, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi mbali mbali katika sala ya kumsalia Marehemu Juma Ali Juma huko katika Msikiti wa Ijumaa  Kijichi.

Akisoama Wasfu wa Maremu Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda Ali Khamis alieleza kuwa Marehmu Juma Ali Juma alizaliwa tarehe 15 Mei, 1964 Ole Mivumo Ishirini Kisiwani Pemba.

Marehemu alipata elimu ya Msingi katika Skuli ya Ziwani na Ole kuanzia mwaka 1972 hadi 1978 na elimu ya Sekondari ‘O’ level na ‘A’ level amepata katika skuli ya ‘Fidel Castro’ mwaka 1979 hadi 1985.

Kwa upande wa elimu ya Juu marehemi alipata Shahada ya Kwanza katika Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) mwaka 1987 mpaka mwaka1990. Mwaka 1994 mpaka mwaka 1995 alisomea Shahada ya Uzamili katika fani ya Kilimo katika Chuo Kikuu cha East Anglia nchini uingereza.

Marehemu alikuwa katika hatua za mwisho za kumaliza Shahada yake ya Uzamivu katika fani ya Kilimo Hai nchini Ujerumani kwa utafiti wa zao la karafuu.

Maisha yake katika Utumishi wa Umma yalianza mwaka 1990 alipoajiriwa kama Afisa wa Kilimo Daraja la Pili katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Maliasili.

Mwaka 1996 mpaka mwaka 2000 aliteuliwa kuwa Katibu Mtendaji Kamisheni ya Mazao ya Biashara na Matunda na kuanzia mwaka 2006 mpaka 2008 alikuwa Mtaalamu mkaazi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) hapa Zanzibar.

Mwaka 2010 mpaka mwaka 2016 alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili na baadae mwaka 2016 mpaka mwaka 2017 aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi na kuanzia mwezi Septemba 2017 hadi mauti yalipomfika alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar.

Akwia Naibu  Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Malisili Marehemu Juma alisimama kidete kumuomba Mkurugenzi Mtendaji wa TAHA Tanzania kuileta TAHA Zanzibar na wmaka 2012 alifanikiwa na TAHA ilisajiliwa rasmi Zanzibar ikiwa ni Taasisi isiyo ya Kiserikali ya kuamsha ukulima wa mboga, matunda na viungo.

Alipokuwa Katibu Wizara tya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya TAHA Arusha, vile vile alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mradi wa TAHA hapa Zanzibar.

Marehemu Juma alikuwa ni kiongozi aliyeheshimika sana makao makuu ya TAHA kwa mawazo na mipango ya kuendeleza Kilimo.

Marehemu Juma alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Kuandaa Mkakati wa Pili na wa Tatu wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA II na III). Pia Marehemu aliongoza Kazi Maalum ya Maabara ya utafiti ambayo matokeo yake yalikuwa ni Mkakati wa Kitaifa uliojulikana kama Matokeo kwa Ustawi R4P”.

Aidha Marehemu Juma alishiriki kuandaa Sera mbali mbali za Zanzibar ikiwemo Sera ya Mazingira na Sera ya Masoko ya Mazao ya Kilimo na Chakula ambapo pia, alikuwa Mjumbe wa kufuatilia matokeo ya Ziara za Rais wa Zanzibar nchini Abudhabi na Indonesia.

Sambamba na hayo, hivi karibuni aliongoza Kamati ya Kuandaa Mpango wa Utekelezaji wa Mfuko Maalum wa Msaada kutoka Falme  za Kiarabu (Khalifa Fund) wa kuwasaidia wajasiriamali wa Zanzibar.

Katika kipindi chote cha utumishi wake marehemu  alikuwa mchapa kazi wa mfano kwa kujituma, kutumia elimu na uzoefu wake  kwa wananchi wa Zanzibar na mwenyewe kufanya kazi kwa mashirikiano makubwa na wenzake.

Wakati wote hakusita kutaka ushauri kutoka wa wafanyakazi wenzake hata katika ngazi ya chini, na kumshauri vyema Waziri wa Biashara na Viwanda.

Marehemu Juma Ali Juma ataendelea kukumbukwa kutokana  na ubunifu na uweledi wake katika kazi na mashirikiano makubwa na ucheshi kwa wenzane na watu mbali mbali.

“Mauti nifaradhi kwetu viumbe. Pengo la utendaji na uwezo wa Marehemu Juma Ali Juma litachukua muda mrefu kuzibika” ilieleza sehemu  ya wasfu huo.

Marehemu ameacha vizuka, watoto na mama mzazi tunamuomba MwenyeziMungu amlaze mahala pema Peponi Amin.

Kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Serikali inawapa pole familia ya marehemu na wafiwa wote na kumuomba Mwenyezi Mungu awajaalie subira katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza kwa kuondokewa na mzee, ndugu, rafiki. Amin.

Rajab Mkasaba, Ikulu


Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.