Habari za Punde

Kesi za uharibifu wa mazingira hazisaidii kulinda rasilmali kwa kucheleweshwa kwake

Na Masanja Mabula -PEMBA .
IDARA ya Misitu na Maliasili zisizorejesheka Zanzibar  imesema  utaratibu wa mahakama wa usikilizaji wa mashauri na kesi  za uharibifu wa mazingira kwenye misitu ya hifadhi  hausaidii kulinda rasilimali   kutokana na kuchelewa kukamilika kwa upelelezi wa mashauri hayo.
 Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na maliasili zisizorejsheka Soud Mohd Juma baada ya kukagua uharibifu uliofanyika kwenye msitu wa Ngezi.
Uharibifu uliofanyika ndani ya hifadhi hiyo ni kukatwa mti aina ya Mvule ambapo walifanikiwa kuyakamata magogo yakiwa  ambayo yalisafirishwa hadi Chake Chake.
Mkurugenzi Soud  amesema utaratibu wa mahakama wa uendeshaji wa kesi hizo sio salama kwa hifadhi ya maliasili na wanyama pori.
Amesema kesi nyngi ambazo zimekuwa zikitokea  ,ndani ya hifadhi hiyo na kuripotiwa kwenye vyombo vya sheria na watuhumiwa kupatikana , hatuoni kinachoendelea.
‘’Pamoja na uchache wa walinzi ndani ya hifadhi hii, lakini sina budi kwapongeza kutokana na juhudi wanazochukua, lakini tunarudishwa nyuma na vyombo vya sheria’’alisema.
Aidha amesema Idara inaendelea kuzifanyia mapitio kamati za hifadhi katika vijiji vinavyozunguka msitu wa ngezi, na kwama hatasita kuzivunja ambapo zitabainika kushindwa kuwajibika.
‘’Kwa mujibu wa sheria namba 10 ya mwaka 1996 , imempa uwezo Mkurugenzi kuvunja kamati ya hifadhi , na tayari kamati ya Mgelema nimeivunja baada ya kushindwa kuwajibika’’alifahamisha.
Akizungumzia suala la ukataji wa miti ndani ya hifadhi hiyo, Soud ameitaka  jamii  pamoja na uongozi wa serikali za mitaa , kushirikiana katika kulinda raslimali na maliasili ili  zisiendelee kuhuumiwa.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Misitu Pemba Mussa Said Bakar amesema wamefanikiwa kuwakamata vijana pamoja na  gari za ng’ombe ambazo zilitumika kubeba magogo kutoka ndani na hifadhi ambapo vijana hao walitoa ushirikiano.
Amesema  tayari vijana hao wameshiriki utoa taarifa juu ya watu walioshiriki kukata mvule huo na  kwamba wao wamesaidia kuutoa ndani ya hifadhi kwa kutumia gari zao za ng’ombe.
‘’Tumefanikiwa kukamata gari mbili za Ng’ombe pamoja na vijana walioshiriki kuupakia magogo hayo , kwa kweli tumewafikisha polisi na wametoa ushirikiano’’alieleza.
Mkuu wa msitu wa hifadhi Ngezi , Salim Mohammed Said amesema tukio hilo limetoa somo kwa jamii kushirikiana na watendaji wa walinzi wa msitu huo katika kuulinda dhidi ya vitendo vya hujuma.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.