Habari za Punde

WATUMISHI OFISI YA WAZIRI MKUU WAASWA KUZINGATIA MAADILINa.Mwandishi Wetu.
Watumishi Ofisi ya Waziri Mkuu Waaswa Kuzingatia Maadili ya  Utumishi  wa Umma katika kutekeleza majukumu yao ili kuiwezesha Serikali  kufikia malengo  ya Serikali ya Awamu ya Tano  kutoa huduma Bora kwa wananchi.

Akizungumza na watumishi wa Ofisi hiyo leo (22 Juni, 2019) Jijini Dodoma , Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inasisitiza uwajibikaji, uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa katika utumishi wa umma ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali.

“Kuna umuhimu mkubwa kwa watumishi wa umma katika Ofisi yetu kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa kuwa jambo hilo halikubaliki kamwe kwani vitendo hivyo vinazorotesha juhudi za Serikali kuwaletea wananchi maendeleo “ Alisisitiza Mhe. Mhagama

Akifafanua amesema kuwa mafunzo yaliyotolewa  na Serikali  kwa watumishi hao ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma yalijikita katika mada mbalimbali ikiwemo  Rushwa mahala pa kazi , haki na wajibu wa watumishi wa umma.

Aliongeza kuwa kwa sasa Serikali  inaweka mkazo katika kuhakikisha kuwa wananchi wanahudumiwa vizuri pale wanapohitaji huduma hivyo ni wajibu wa kila mtumshi katika Ofisi hiyo kuendelea kutoa huduma bora kwa wale wote wanaofika katika Ofisi hiyo na katika Taasisi zilizopo chini ya Ofisi hiyo.

Kwa upande wake Katibu Ofisi ya Waziri Mkuu  (Waziri Mkuu na Bunge) Bi. Maimuna Tarishi amesema kuwa watumishi wa Ofisi hiyo watazingatia maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Mhagama ili kuongeza tija katika kutoa huduma  kwa wananchi.

Aliongeza kuwa watumishi wa Ofisi hiyo wameadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma  kwa kushiriki mafunzo ya kuwakumbusha taratibu na kanuni za utumishi wa umma, mafunzo kwa watumishi wanaotarajia kustaafu hivi karibuni.

Ofisi ya Waziri Mkuu imeadhimisha wiki ya Utumishi ya Umma kwa kufanya shughuli mbalimbali na kuhitimisha kwa mafunzo ya siku moja kwa watumishi wote yakilenga kuwakumbusha wajibu wao katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku ili hatimaye kufikia malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano.Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka huu inasema;  "Uhusiano kati ya uwezeshaji wa Vijana na Usimamizi wa                                                                                                          
Masuala ya Uhamiaji; kujenga utamaduni wa utawala bora., Matumizi ya tehama na ubunifu katika utoaji wa huduma jumuishi"

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.