Habari za Punde

Balozi Seif: Serikali zote zinaendelea kutimiza wajibu wake kuwatumikia wananchi pande zote

 Balozi Seif akikabidhi Mashine  Sita za kusagia Nafaka zitazogaiwa kwa Wialaya sita  za UWT zilizomo ndani ya Mkoa wa Arusha zilizotolewa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoani Humo Mh.Catherine Magige.
 Balozi Seif akizindua Tovuti ya Jumuiya ya Wanawake Tanzania {UWT} itakayoweka wazi kazi na majukumu ya Jumuiya hiyo kwenye Mtandao utakaoweza kusoma mahali popote Duniani.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizundua Kitabu Maalum kinachoelezea muelekeo wa Uchumi katika Jumuiya ya Waynawake Tanzania {UWT} kwenye Kongamano lililoandaliwa na Jumuiya hiyo kumpongeza Rais wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kutimia Miaka Minne ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM
Viongozi wa Jumuiya ya Wanawake UWT wakicheza Wimbo Maalum wa Jumuiya hiyo uliopigwa kwenye Kongamamo la Jumuiya hiyo kumpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwahutubia Viongozi wa Jumuiya ya Wanmawake Tanzania  kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha kwenye kongamano la kumpongeza Dr. John Pombe Magufuli kutimiza Miaka Mmne ya Utawala wake kwa mafanikio makubwa.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania {UWT} Bibi Gaudentia Kabaka akitoa maelezo na kumkaribisha Balozi Seif kulifungua Kongamano la UWT Tanzania Mkoani Arusha.
Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis/ Rashida Abdi, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali zote mbili Tanzania ile ya Jamuhuri ya Muungano na ya Mapinduzi ya Zanzibar zinaendelea kutimiza wajibu wake kwa kuwatumikia Wananchi wa pande zote kama zilivyoahidi wakati wa Kampeni ya uchaguzi wa Urais, Wabunge, Wawakilishi pamoja na Madiwani Mwaka 2015.
Alisema Wananchi pamoja na Jamii yote imekuwa ikishuhudia  mambo mengi yanayosimamiwa na kutekelezwa na Serikali hizo  mbili chini ya Uongozi imara wa Viongozi wake shupavu na Majemedari Dr. John Pombe Joseph Magufuli na Dr. Ali Mohamed Shein.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo kwenye Kongamano la UWT la kumpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kwa kutimiza Miaka Minne ya utendaji tokea achaguliwe na kuunga mkono Agenda ya Ukombozi wa Mwanamke lililofanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Mjini Arusha.
Alisema Tanzania hivi sasa imekuwa ikiheshimika katika Mipaka ya Nchi kwa kasi ya mabadiliko makubwa ya Kimaendeleo yanayopelekwa kwa Wananchi wake kasi inayowashawishi Viongozi wa Mataifa ya Kigeni yakiwemo yale ya Afrika Mashariki kuvutiwa na kasi hiyo ya Maendeleo.
Balozi Seif  aliwaeleza akina Mama hao wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania         { UWT} kwamba kasi kubwa ya Maendeleo iliyoambatana na hali ya Amani na utulivu  Nchini inaonyesha wazi kabisa kuwavutia Wageni na Wawekezaji kutaka kuanzisha miradi yao ya Kiuchumi Nchini Tanzania.
Alisema umakini wa Serikali katika kusimamia  ukusanyaji wa mapato kutoka asilimia 5.1% hadi asilimia 7.5%  na kupambana na ufisadi kwa kuanzisha Idara ya Mahakama ya Mafisadi  kwenye Mahakama Kuu inaendelea kupunguza kasi kubwa ya Wananchi wachache wenye nafasi Serikalini au uwezo kibiashara kupora na kujilimbikizia mali ya Watanzania walio wengi.
Balozi Seif  alifahamisha kwamba yapo matumaini makubwa kwa chaguzi zinazokuja kupunguwa kwa kiasi kikubwa suala la Rushwa kutokana na jitihada zilizofanywa na Serikali katika kupiga vita mdudu huyo mbaya katika Jamii ambaye aliwahi kushamiri ndani ya Serikali na hata Vyama vya Siasa na kupelekea baadhi ya Watu kukosa haki zao.
Alieleza kwamba Sekta ya Kilimo imefanyiwa mageuzi makubwa kama ilivyoainishwa ndani ya Chama cha Mapinduzi tokea kuasisiwa kwake kuwa ni Chama cha Wakulima ili kuhakikisha Kilimo kinawanufaisha Wakulima  waweze kustawisha Maisha yao.
Balozi Seif alisema kwa nyakati tofauti Serikali ya Awamu ya Tano imeshughulikia bei elekezi za mazao tofauti kama vile zao la Korosho na Pamba ili wakulima wa mazao hayo wapate bei nzuri kutoka kwa wanunuzi na wafaidike na Kilimo chao.
Alitoa Wito kwa Watanzania kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa  na Rais Dr. John Pombe Magufuli na Rais Dr. Ali Mohamed Shein  kwa kufanya kazi kwa budii, uadilifu, uaminifu, kuwajali wengine katika kuwasikiliza kero zao kwa nia ya kuzipatia ufumbuzi.
Alisema Watanzania lazima waendelee kulipenda Taifa lao lililobarikiwa kuwa na Rasilmali nyingi za kuvutia kwa kuwajibika ipasavyo bila ya kusukumwa ili kuujenga Uchumi imara unaoendelea kukuwa siku hadi siku.
Akizungumzia suala la Ukimwi, Balozi Seif aliwakumbusha Akina Mama hao pamoja na Watanzania wote kwa ujumla kuelewa kwamba maradi ya Ukimwi bado yanaendelea kuwa tishio la maisha ndani ya Dunia hii ikiwemo Tanzania.
Hivyo aliwaomba Wananchi waendelee kuchukuwa tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya maradhi hayo thakili kwa kupima afya zao pale wanapopata fursa za kufanya hivyo ili wajue Afya zao vilivyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM aliwapongeza Viongozi wa Jumuiya ya Wanawake wa Tanzania {UWT} kwa ubunifu wao wa kuandaa Makongamano kama hayo ambayo tayari yameshafanyika katika ngazi za Wilaya.
Aliwashauri waendelee na Makongamano hayo katika Mikoa iliyobakia ili Wananchi wapate fursa ya kusikia Taarifa za Utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi inayosimamiwa na Serikali kupitia Mawaziri na Watendaji wote wa Taasisi za Umma.
Wakitoa muhtasari wa mchanganyuo wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 215 hadi 2020 Mawaziri na Manaibu Mawaziri wa Wizara za SMT walisema yapo mabadiliko makubwa kwa Uchumi wa Taifa na Ustawi wa Wananchi katika maeneo tofauti Nchini.
Wamesema Sekta ya Madini iliyopewa mambo 15 kuyatekeleza imefanikiwa kukusanya mapato kutoka shilingi Bilioni 175 hadi Bilioni 335.5 baada ya marekebisho kadhaa yaliyopelekea kuundwa kwa Kamati nyingi kuliko Sekta nyengine Nchini lengo ni kuchangia Uchumi wa Taifa.
Wameeleza kwamba maeneo ya uchimbaji Madini yameongezeka kutoka 25 hadi 175Nchi nzima kwa lengo la kuwapa fursa zaidi wachimbaji wadogo kujipatia kipato na kuondokana na ukali wa maisha.
Kwa upande wa sekta ya Elimu Mawaziri na Manaibu Mawaziri hao walisema kwamba matokeo ya Kidato cha Sita Mwaka huu ya asilimia 99% yamefikiwa na Wanafunzi wanawake na kuthibitisha uimarikaji wa Elimu chini ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.
Walisema Sekya ya Elimu ambayo ndio sekya mama katika kuifinyanga Jamii kuelekea katika Maendeleo imetengewa Bajeti Kubwa Mwaka huu ikiwa ni ya Pili kwa Taasisi za Umma ili iandae Vijana watalaokuwa Wataalamu wa Taifa hili hapo baadae.
Wakielezea Uwezeshaji Kiuchumi kupitia Wizara inayosimamia Vijana, na Wanawake Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri hao walisema shilingi Bilioni 39 zilitolewa Mikopo kwa Wanawake katika Maeneo takriban yote Tanzania.
Mikopo hiyo iliwagusa zaidi akina Mama Laki 877,000 kupitia Mifuko 43 kupitia Mfuko wa WEF yakiwemo Makundi ya Saccos zaidi ya Mia Sita.
Akitoa salamu za Chama cha Mapinduzi Taifa Kaitu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho Nd. Hamphrey Polepole alisema Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli ni Ushindi wa CCM katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Baadae Mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.
Nd. Polepole alisema uchapakazi wa DR. Magufuli hasa katika uimarishaji wa Hospitali za Wilaya  Nchini kutoka 77 mwaka 1961 hadi 2015 na kuongezeka nyengine 67 2015 hadi 2018/2019 inatosha CCM kuendelea kupewa jukumu la Kuongoza Taifa hili.
Alisema Ujenzi wa Hospitali hizo chini ya usimamizi wa Dr. Magufuli umekwenda sambamba na ujenzi wa Vituo vya Afya kutoka 115 Mwaka 1961 hadi Vituo 350 kufikia Mwaka 2019.
Nd. Polepole akiwahakikishia Wana CCM na Watanzani wote kwamba wana haki ya kutembea kifua mbele kutokana na uimara wa CCM ulioziwezesha Serikali zote kutekeleza vyema majukumu yake ipasavyo hasa kutokana na jeshi kubwa ililonalo CCM kwa Kundi kubwa la Jumuiya ya Wanawake Tanzania.
Alisema hiyo inadhihirisha wazi kwamba ushindi wa Chama cha Mapinduzi kwa takwimu za haraka hara unaelekea kupanda Mwaka ujao kufikia zaidi ya asilimia 70% kutokana na ongezeko kubwa la wanachama wapya wanaojitokeza kujiunga na Chama cha Mapinduzi.
Akimkaribisha Mgeni rasmi katika Kongamano hilo Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania {UWT} Mh. Gaudentia Kabaka alisema Wanawake hawatoyumba,kutetereke, kubabaishwa katika kuona Tanzania inazidi kusonga mbele.
Mh. Kabaka alisema Wanawake ndio Walezi na wajenzi wa Familia inayojenga Taifa imara linaloweza kujitegemea bila ya kusubiri misaada ya nje yenye kuambatana na masharti yasiyotekelezeka.
Katika Kongamano hilo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akibabidhi Mashine Sita za kukobolea Nafaka kwa Wilaya Sita zilizomo ndani ya Mkoa wa Arusha zilizotolewa na Mbunge wa Viti Maalum Catherine Gagige  zenye thamani ya shilingi Milioni 24,000,000/-.
Balozi Seif  kuzindua Wabsite ya Jumuiya ya Wanawake, kuzindua Kitabu chenye kuelezea masuala ya Kiuchumi ya Jumuiya hiyo pamoja na Kukabidhi Hundi la Shilingi Lali moja moja kwa Akina Mama 100 wa Mkoa wa Arushwa zilizotolewa mkopo na Mfanyabiashara mashuhuri Mkoani humo Bwana Wibal Chambulo.
Kongamano linalofuata la Jumuiya ya Wanawake Tanzania {UWT} la kumpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tnaznia Dr. John Pombe Magufuli linatarajiwa kufanyika  siku chache zijazo Mkoani Kilimanjaro

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.