Habari za Punde

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Mwakyembe : Serikali Itaendelea Kushirikiana na Wadau wa Sekta ya Utangazaji Tanzania.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dkt. Ayoub Rioba akizungumza jambo wakati wa kikao baina ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) na wadau wa sekta ya habari wakiwemo watayarishaji wa vipindi vya televisheni vyenye maudhui ya ndani wakati wa mkutano wake uliofanyika jana 
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe (mbele) akizungumza  na wadau wa sekta ya habari wakiwemo watayarishaji wa vipindi vya televisheni vyenye maudhui ya ndani wakati wa mkutano wake

uliofanyika jana Alhamisi 

 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati) akibadilishana mawazo na Kaimu Mkurugenzi wa Utangazaji wa TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka pamoja na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Patrick Kipangula wakati wa mkutano baina ya Waziri na Wadau wa sekta ya habari wakiwemo watayarishaji wa vipindi vya televisheni vyenye maudhui ya ndani
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe (aliyekaa) akiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano wake baina yake na wadau hao uliofanyika jana Alhamisi Julai 25, 2019.
 (Na.Mpiga Picha Wetu)

Na Mwandishi Wetu  - Maelezo .Dar -26.JULAI, 2019
WAZIRI wa Habari, Utamadani, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amewahakikishia wadau wa sekta ya utangazaji nchini ikiwemo waandaaji na wazalishaji wa vipindi vya televisheni vya maudhui ya ndani kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao na kuwajengea mazingira wezeshi ili kuwawezesha kutimiza wajibu wao wa msingi katika  jamii na Watanzania kwa ujumla.
Akizungumza katika kikao maalum baina yake watayarishaji wa vipindi vya maudhui ya ndani jana Alhamisi (Julai 25, 2019) Jijini Dar es Salaam, Dkt. Mwakyembe amesema malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa tasnia ya habari inapiga hatua kubwa za maendeleo na kutoa mchango unaostahiki katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Waziri Mwakyembe alisema Serikali inatambua wajibu na umuhimu wa tasnia ya habari nchini, na hivyo imetunga sheria na kanuni mbalimbali zinazoongoza vyombo vya habari ikiwemo televisheni, ambapo vimewekwa utaratibu wa kurusha na kuandaa vipindi mbalimbali kupitia miongozo inayotolewa mamlaka husika ikiwemo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
“Tunatambua kuwa kuna baadhi ya vifungu vya kisheria vinavyoongoza maudhui ya vituo vya utangazaji vimekuwa changamoto, kwa kuwa Sheria hizi sio biblia au msahafu takatifu, tunaweza kuzifanyia marekebisho kila baada ya kipindi cha miaka 3-4 ili kuona ni namna gani inasaidia sekta ya utangazaji sambamba na kutumia fursa mbalimbali zinazojitokeza” alisema Waziri Mwakyembe.
Aidha Waziri Mwakyembe alisema Wizara yake ipo tayari kupokea aina yoyote ya ushauri, mapendekezo na maoni ya wadau wa wazalishaji na waandaji wa vipindi vya Televisheni hususani masuala yote ambayo yamekuwa yakiwaletea changamoto katika utekelezaji wa majukumu yao ya kuhabarisha umma kupitia vipindi mbalimbali ambavyo vimekuwa daraja la kuwaunganisha Watanzania.
Akifafanua zaidi Dkt. Mwakyembe alisema Serikali itahakikisha kuwa waandishi wa vyombo vya habari kutoka sekta ya umma na binafsi ikiwemo waandaaji wa vipindi vya maudhui ya ndani wanajengewa uwezo ikiwemo kuwapatia mafunzo ya muda mfupi, ya kati na mrefu, hatua inayolenga kuwaongezea weledi, ujuzi na maarifa na hivyo kutimiza wajibu wao wa msingi katika jamii.
Dkt. Mwakyembe alisema katika mfumo uliopo sasa wa kutangaza maudhui ya ndani kumekuwepo na changamoto mbalimbali katika kanuni, sheria na taratibu ambazo zimekuwa zikileta malalamiko kutoka kwa wadau, na hivyo Serikali itahakikisha kuwa vipengele hivyo vinafanyiwa kazi kwa kuwa Serikali na vyombo vya habari vyote kwa pamoja vimekusudia kujenga msingi imara wa ushirikiano baina yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Matukio wa Shirika la Utangazaji Nchini (TBC) Martha Swai amesema TBC imekuwa mstari wa pembe katika kutangaza vipindi vyake vya Televisheni katika maudhuo ya ndani, ambapo asilimia 82 vimegusa masuala ya elimu, biashara na kuburudisha, na asilimia 18 ikijikita katika masuala ya muziki.
Anaongeza kuwa Shirika hilo limekuwa likiatangaza matangazo yake ya Televisheni katika chaneli kubwa tatu ambazo ni  TBC 1,   TBC 2 na Tanzania Safari ambazo zote kwa pamoja vimekuwa na mchango mkubwa katika kutangaza habari na matukio ya vipindi mbalimbali vyenye kuakisi maudhui ya ndani.
Naye Meneja Vipindi wa Kampuni ya Tumaini Media, Paul Mabuga amesema kwa sasa kumekuwepo na changamoto kubwa ya ukosefu wa matangazo ya biashara katika vituo vya Televisheni kwani wafanyabiashara wengi wamekuwa wakitumia zaidi mitandao ya kijamii ili kuweza kufikisha ujumbe wananchi kwa njia ya kisasa na haraka zaidi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.