Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Atembelea Mradi wa Ujenzi wa Hoteli ya Kitalii Nungwi

Muonekano wa haiba ya Baadhi ya Majengo mapya ya vyumba vya kulala wageni ya Hoteli ya RIU Palace Zanzibar yaliyopo Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kushoto akisalimiana na Meneja Mkuu wa Hoteli ya Kimataifa ya RIU Palace Zanzibar iliyopo Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja Bwana Luis Sanchez Sarda alipofika kukagua maendeleo ya ongezeko la ujenzi wa vumba vya kulala wageni. 
Balozi Seif  akiupongeza uongozi wa Hoteli ya Riu Palace Zanzibar kwa kujikita katika uwekezaji ndani ya Sekta ya Utalii na kuwatahadharisha kuepuka ujenzi wa majengo yao kutumia makuti.Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja Mh. Vuai Mwinyi Mohamed na Meneja Mkuu wa Hoteli ya Kimataifa ya RIU Palace Zanzibar Bwana Luis Sanchez Sarda.(Picha OMPR)
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewashauri Wawekezaji wa Mahoteli katika Sekta ya Utalii Nchini kuzingatia umuhimu wa kutoa fursa za ajira kwa Wazawa ili kudumisha mahusiano mema katika uendelezaji wa Miradi yao.
Alisema hatua hiyo itakwenda sambamba na azma ya Serikali Kuu katika kufungua Milango ya Uwekezaji itakayoshajiisha fursa zaidi za ajira hasa kwa Vijana itakayosaidia kupunguza msongamano wa makundi yasiyo na Kazi Mitaani.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa ushauri huo wakati wa ziara yake ya kuangalia maendeleo ya ongezeko la Ujenzi wa vyumba vya kulala Wageni katika Hoteli ya RIU Palace Zanzibar iliyopo Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unaguja.
Alisemaongezeko kubwa la Vijana wanaomaliza Masomo yao limekuwa kubwa mno na kulazimika Serikali kubuni mbinu za kupambana na changamoto hiyo iliyoenea hata katika Mataifa makubwa yaliyoendelea kiuchumi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameupongeza Uongozi mzima wa Hoteli ya Kimataifa ya RIU Palace Zanzibar kwa uamuzi wake wa kutanua Mradi wao jambo ambalo litaongeza mapato ya Taifa na kukuza fursa zaidi ya Ajira.
Balozi Seif ameutaka Uongozi huo kuepuka uwezekaji wa makuti kwenye majengo yao ili kujikinga na jaribio lolote linaloweza kusababishwa na majanga ya moto hasa wakati wa kiangazi.
Alisema ipo miradi mingi ya Mahoteli iliyowahi kutumia mfumo huo wa makuti kwa dhana ya kuridhisha Wateja wao lakini hatma yake imepunguza uzalishaji na mengine kufungwa kabisa baada ya kupata majanga ya moto.
Mapema meneja Mkuu wa Hoteli ya Kimataifa ya Rui Palace Zanzibar Bw. Luis Sanchez Sarda alisema Uongozi wa Hoteli hiyo umelazimika kuongeza idadi ya vyumba vya kulala wageni ili kukidhi mahitaji ya Wateja wao wa naoongezeka kila kukicha.
Alisema ongezeko la ujenzi huo utafikia vyumba 100 vya kulala wageni vinavyojengwa katika mfumo wa vyumba 50 kwa kila awamu vitakavyoiwezesha Hoteli hiyo kufikia idadi ya vyumba Mia 200.
Meneja Mkuu huyo wa RIU Palace Zanzibar alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba ujenzi wa vyumba hivyo uliofikia asilimia 85% sasa utakamilika rasmi ifikapo Mwezi Novemba Mwaka huu na kuongeza idadi ya Wafanyakazi Wazawa 40.
Kwa upande wake Mkurugenzi Uwezeshaji na Miradi ya Uwekezaji kutoka Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar {ZIPA} Shariff  Ali Shariff alisema mabadiliko ya Sheria ya Uwekezaji yaliyofanywa na Serikali hivi karibuni inaelekeza Muwekezaji ye yote analazimika kuwekeza Mradi wake Nchini usiopungua thamani ya Dola za Kimarekani Milioni Mia Moja.
Shariff alisema uamuzi huo wa mabadiliko ya Sheria ya Uwekezaji umezingatia umuhimu wa kuimarisha Miradi ya Kudumu ya Uwekezaji itakayoendelea kutoa ajira kubwa, kuongeza mapato na kuimarisha Uchumi wa Nchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.