Habari za Punde

Rais Magufuli Atoa Agizo Kero Ucheleweshaiji Vibali NEMC Itatuliwe

Na: Frank Shija – MAELEZO
Rais John Pombe Magufuli metoa agizo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Goerge Simbachawene  kushughulikia kero ya ucheleweshwaji wa vibali kwa wawekezaji ili kuendana na kasi ya uchumi wa viwanda.
Amelitaka  Baraza la  la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kutochelewesha utoaji wa vibali kwa wawekezaji ili kuongeza ufanisi katika ukuaji wa uchumi wa viwanda.
“Pasiwe na ucheleweshwaji wa vibali vya NEMC kwa viwanda vyetu, sisi tunataka kuwa na viwanda vya kutosha na wawekezaji wasiwekewe vikwazo kwa visingizio vya NEMC, vibali hivi vitoke kwa sababu tunahitaji viwanda, ikiwezekana wawekeze kwanza vibali vya NEMC vitafuata baadae,”alisema Dkt. Magufuli.
Rais Magufuli amemtaka Simbachawene kusimamia kwa karibu suala hilo la ucheleweshwaji wa vibali vya Tathmini ya uharibifu wa Athari ya Mazingira vinavyotolewa na NEMC.
Rais Magufuli ameongeza kuwa fedha nyingi zinatolewa na wafadhili kwa ajili ya miradi ya mazingira lakini kumekuwa hakuna matokeo ya kuridhisha hivyo ametaka kuwepo usimamizi madhubuti wa rasilimali fedha inayoelekezwa katika miradi ya mazingira.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amempongeza Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Mohamed Bashe kwa uchambuzi mzuri wa masuala ya kilimo aliokuwa anaufanya akiwa bungeni na kuongeza kuwa hiyo ndiyo sababu ameamua kumteua ili akayatekeleze kwa vitendo kwa ajili  ya kukwamua kilimo.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), George Boniphace Simbachawene amesema kuwa shughuli zote za kiuchumi zinategemea sana mazingira  hivyo atashirikiana na wataalamu wa wa ofisi yake kumshauri vyema Makamu wa Rais katika namna bora ya kutatua changamoto zitokanazo na uharibifu wa mazingira.
Ameongeza kuwa fedha zinazotajwa kuingia katika nchi kwa ajili ya mazingira ni nyingi lakini zimekuwa zinatumika zaidi katika masuala ya kiutawala badala ya kuelekezwa katika miradi ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
“Nataka nikuhakikishie Mhe. Rais kuwa nitamsaidia Makamu wa Rais katika Ofisi yake, kwanza natambua lakini pili mimi kwa kushirikiana na wenzangu nitakaowakuta pamoja na walaalamu nitajitahidi kutoa mawazo yangu ili tuone ni namna gani tunaokoa mazingira,” alisema Simbachawene.
Akizungumzia masuala ya Muungano, Waziri Simbachawene amesema kuwa anafahamu kuwa msingi wa Muungano wetu siyo tu yaliyoandikwa katika Katiba na kufafanuliwa katika sheria bali ni wa kihistoria ambao unajengeka katika maelewano zaidi badala ya maandishi.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Mohamed Bashe amesema kuwa anafahamu changamoto zinazowakabili wakulima wa nchi hii hasa ukizingatia kuwa ndiyo sekta inayowagusa asilimia kati ya 60-70 ya watanzania wote, wengi wao ndiyo wanyonge ambao Rais Magufuli ndiye mtetezi wao.
Amesema kuwa atajitahidi kadri ya uwezo wake kwa mamlaka atakayopewa kuhakikisha anamsaidia Mhe. Rais katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ili kukwamua sekta ya Kilimo nchini.
Hafla hii ya uapisho imefanyika kufuatia Mhe. Rais kufanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri kwa kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Januari Makamba na nafasi yake kuchukuliwa na Waziri George Simbachawene, huku Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akijaza nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. Innocent Bashungwa ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara..

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.