Habari za Punde

Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein Ametowa Mkono wa Eid El Hajj Kwa Wazee wa Sebleni,Welezo na Watoto wa SOS na Mazizini Zanzibar.


Waziri wa Kazi Uwezeshaji wa Wazee Wanawake na Watoto Zanzibar Mhe. Maudline Castico akitowa Mkono wa Eid El Hajj kwa Wazee wa Nyumba ya Wazee ya Sebleni Zanzibar , akimuwakilisha Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein.


MKE wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein amesema suala la matunzo ya wazee na ulezi wa watoto linaendana na utekelezaji wa Sera na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Amesema hayo katika hafla ya utoaji wa zawadi ya sikukuu ya Eid El Hajj kwa Wazee na Watoto wanaoishi katika nyumba za Wazee Welezo na Sebleni pamoja na vituo vya kutunzia Watoto vya SOS na Mazizini, alizozianda kwa kushirikiana na Mke wa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Idd.

Akizungumza kwa niaba ya Mama Mwanamwema Shein, Waziri wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Zanzibasr Mhe. Moudline Castico alisema katika kufanikisha malengo hayo Serikali inatumia zaidi ya shilingi Milioni 200 kwa mwezi, ikiwa ni malipo ya Pensheni Jamii kwa Wazee wenye umri wa miaka 70 na kuendelea.

Sambamba na hilo, alisema Serikali inaendelea kuyafanyia matengenezo majengo ya makaazi ya Wazee wasiojiweza ili kuleta ustawi bora wa maisha yao, pamoja na kuwapatia huduma bure za afya ikiwa nikuthamini mchango mkubwa walioutowa wakati wa ujana wao.

Aidha alisema Serikali inakusudia kuifanya sheria dhana ya Pensheni jamii, ili kuepuka athari za mabadiliko ya uongozi hapo baadae.

Alisema viongozi hao wameamuwa kutowa zawadi hizo ili kuhakikisha wazee na watoto hao wanafurahia na kujumuika pamoja na wananchi wengine.

Waziri Castico, aliwataka wazee hao kupitia sikukuu hiyo kuendelea kuliombea dua Taifa, ili liweze kuepukana na athari zitokazona majanga mbalimbali.

Aidha, aliwataka wazazi na walezi kuzingatia malezi bora na maadili ya watoto wao kwa kujiepusha na vitendo vya kikatili na udhalilishaji.

Alisema tukio la hivi karibuni la utupaji wa mtoto Kisiwani Pemba na hatimae kuokotwa na mbwa, linathibitisha kwa kiasi gani jamii isivyojali na kuthamini malezi na mtunzo ya watoto.

Alieleza kuwa Serikali imefanya juhudi kufanikisha upatikanaji wa Mashine ya uchunguzi wa Vinasaba (DNA) ili kukabiliana na wimbi la matukio mbali mbali ya udhalilishaji.

Mapema, Mkurugenzi wa kituo cha Kulelea watoto cha SOS, Bi.Asha Salim aliwashukuru viongozi hao kwa muendelezo wao wa kila mwaka na kuwatakia kheri na afya njema katika maisha yao.

Alisitiza umuhimu wa wazazi na walezi katika utunzaji wa watoto wao na kuviomba vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na taasisi nyengine zinazohusika na haki za watoto kuwachukulia hatua wote watakaobainika kuhusika na vitendo vya udhalilishaji na utupaji watoto.

Nae, mtoto Salama Abdalla Ali wa kituo cha kulelea watoto Mazizini, kwa niaba ya watoto wenzake aliwashukuru viongozi kwa imani na mapenzi makubwa kwao na kuwakumbuka mara kwa mara, hatua aliyosema inawapa faraja.

AbdiShamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
 E-mail: abdya062@gmail.com


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.