Habari za Punde

Serikali Yaitaka NIC Kuchangia Pato la Taifa Kwa Zaidi ya Asilimia Tano.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu (kushoto) na Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Bima la Taifa- NIC, Bw. Laston Msongole, wakishuhudia makabidhiano ya ofisi kati ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika  la NIC. Bw. Sam Kamanga na Mkurugenzi Mtendaji mpya waShirika hilo, Dkt. Elirehema Doniye.
Na. Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
Serikali imelitaka Shirika la Bima la Taifa- NIC kuhakikisha mchango wake unafikia zaidi ya asilimia tano katika pato taifa badala ya chini ya asilimia moja ya sasa ili kuweza kuchochea kasi ya ukuaji wa Sekta ya Fedha nchini. 
Hayo yamebainishwa Jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, wakati akishuhudia kukabidhiwa rasmi Ofisi Mkurugenzi mpya wa Shirika la Bima la Taifa- NIC, Dkt. Elirehema Doniye.
Dkt. Kazungu amesema kuwa Shirika la NIC, linatakiwa kujipanga kimkakati kuwa chanzo kizuri cha mapato na kuhakikisha linawafikia wananchi wengi zaidi hususani katika Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Aidha amelitaka Shirika la NIC kuhakikisha linajipanga kiushindani kutoa bima ya miradi yote mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya NIC, Bw. Laston Msongole, amesema kuwa Shirika hilo linawagusa watanzania wote kwa kuwa linatoa huduma zake Tanzania Bara na  Zanzibar.
Alisema kuwa Shirika la NIC, limeanza kufanya vizuri katika soko hivyo ni jukumu la Mkurugenzi mpya kuendeleza juhudi hizo kwa kuwa hapo awali lilikuwa miongoni mwa mashirika yaliyotakiwa kubinafsishwa, kwa kuona umuhimu wake Shirika hilo limebaki kuwa la wananchi na sasa linatakiwa kujiendesha kibiashara.
Naye Mkurugenzi mpya wa Shirika hilo Dkt. Elirehema Doniye, amesema kuwa anafanya jitihada kuhakikisha  Shirika hilo linaongeza ufanisi zaidi ili liweze kuchangia katika pato la Taifa kikamilifu kama alivyoelekeza, Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Kazungu.
Alisema kuwa Shirika hilo linajiendesha kibiashara hivyo ni lazima watendaji kufanya kazi kwa nidhamu ya juu, kuwafikia wateja wadogo na wakubwa  na kwenda na kasi ya Serikali ya awamu ya tano.
Aidha aliyekuwa Mkurugenzi wa NIC, Bw. Sam Kamanga, amesema kuwa amemkabidhi Mkurugenzi mpya Shirika ambalo limeanza kufanya vizuri, kwa kuwa tayari kuna bima ya Kilimo ambayo itawafikia wananchi wengi, lakini pia  NIC imepata tuzo mbalimbali hivyo ni jukumu la uongozi mpya kuendeleza mafanikio hayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.